Jinsi wadukuzi waliiba Sh2.2 bilioni kutoka Benki Kuu ya Uganda
WADUKUZI wa mitandao wameponyoka na shilingi bilioni 62 (sarafu ya Uganda) sawa na Ksh2.2 bilioni kutoka Benki Kuu ya Uganda.
Haya ni kwa mujibu wa ripoti katika gazeti la New Vision linalomilikiwa na serikali ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Wadukuzi hawa wanaojitambulisha kwa jina “Waste,” wanaripotiwa kufikia mfumo wa Teknolojia ya Mawasiliano (IT) ya benki hiyo na kuhamisha pesa hizo kiharamu mapema mwezi wa Novemba.
Kundi hilo linaloendesha shughuli zao Kusini Mashariki ya Asia, lilituma sehemu ya pesa hadi Japan.
Kidokezo hiki kilitolewa na New Vision bila kutaja wale waliofichua habari hii kutoka kwa benki ya taifa la Uganda.
Shirika la habari la Reuters lilijaribu kupata maoni kutoka Bank of Uganda na idara ya polisi.
Kulingana na Reuters, asasi hizi zilidinda moja kwa moja kujibu maswali kuhusu tukio hilo.
New Vision imeripoti kuwa benki hiyo imefaulu kupata zaidi ya nusu ya pesa hizo kutoka kwa wadukuzi.
Katika hatua ya kuangazia uingiliaji huu wa kimitandao, Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameamuru uchunguzi uanze mara moja.
Njama ya ndani
Gazeti huru ambalo ni maarufu zaidi nchini Uganda, Daily Monitor, liliripoti kuwa wizi huo unaweza kuwa ulihusisha njama na wafanyakazi wa benki.
Matukio ya wizi wa kimitandao katika benki na taasisi nyingine za huduma za fedha pamoja na mashirika ya mawasiliano, yametokea mara nyingi Uganda.
Hata hivyo, polisi wanasema kuwa baadhi ya maafisa wa benki hawajakuwa tayari kukubali waziwazi kuwa matukio hayo yametendeka kwa hofu ya wateja kujiondoa.