Makala

Jinsi ya kutumia Sh3,000 pekee kufanya Krismasi ya kufana jijini

Na SAMMY WAWERU December 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KWA Martha Wambui, Krismasi ya mwaka huu itakuwa tofauti.

Anasema kuwa amesitisha safari za kwenda mashambani eneo la Gatundu, Kaunti ya Kiambu.

Badala yake, mama huyo wa watoto watatu ataadhimisha sikukuu hiyo nyumbani kwake Roysambu, Nairobi, kwa bajeti ya Sh3,000 pekee.

“Nimepiga hesabu na kuona bado ninaweza kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo nikiwa hapa mjini. Nikisafiri, itakuwa baada ya shamrashamra za Krismasi,” anasema.

Kupanda kwa gharama ya maisha kumezilazimu familia nyingi za mijini kubadili mtazamo wao kuhusu Krismasi.

Chakula, nauli, ada za shule na matumizi ya kila siku vimefanya wengi wapange bajeti kwa umakinifu zaidi.Kwa Wambui, siri ni kutoa kipaumbele kwa vitu muhimu. Anasema lazima apike kuku siku ya Krismasi.

Katika masoko jijini Nairobi, kuku huuzwa kati ya Sh800 na Sh1,000.“Kwangu, kuku inatosha kuifanya Krismasi iwe ya kipekee. Sio lazima iwe ghali,” asema.

Chakula hicho kitaandaliwa pamoja na chapati. Mfuko wa kilo mbili wa unga wa ngano hugharimu kati ya Sh150 na Sh200.

Mafuta ya kupikia, lita moja ikiuzwa takribani Sh300, na mchele kilo mbili ni Sh200.Ili kukamilisha mlo, atanunua viazi kilo mbili kwa Sh150 na kabichi kwa Sh50.

Baada ya kujumlisha, anasema atabaki na takribani Sh1,000 kununua nyanya, vitunguu, viungo na soda ya lita mbili inayouzwa karibu Sh190.Kwa upande mwingine, Peninah Wairimu, mama wa mtoto mmoja anayeishi Nairobi, anasema hatasafiri Nyeri.

“Nitanunua nyama ya mbuzi nusu kilo na inanitosha mimi na mtoto wangu,” asema.

Naye Dennis Warui, dereva wa teksi mtandaoni, anasema pesa ya nauli ya kwenda Murang’a itatumika kulipia ada ya shule na kusaidia wazazi wake.

Kwa wanaobaki jijini, burudani itakuwa katika maeneo ya umma kama Uhuru Park na Jeevanjee Gardens.“Cha muhimu ni kuwa pamoja kama familia,” asema Wairimu.Kwa wengi, Krismasi haifai kuwa ya gharama ya juu, bali kujumuika na familia na kuwa na moyo wa shukrani.