Makala

Kampuni ya kuuza mafuta yapinga kuuzwa kwa ardhi yake

October 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAMPUNI inayosambaza mafuta ya petroli katika mataifa ya Afrika ya Mashariki na Kati yenye mtaji wa Sh14bilioni imefika katika mahakama kuu kupinga kuuzwa kwa mali zake na benki moja inayoidai mkopo wa Sh631milioni.

Mahadi Energy Limited (MEL) imepinga hatua ya Benki ya Premier (PBL) ambayo awali ilikuwa First Community Bank ya kuuza mali zake katika miji ya Nairobi na Mombasa.

Mahadi imefichua katika ushahidi iliyowasilisha mahakama kuu ya Milimani Nairobi kwamba mali zake zimeuzwa na dalali kinyume cha sheria.

Kupitia kwa mawakili Danstan Omari na  Stanley Kinyanjui, Mahadi imefichua kampuni iliyouziwa mali hizo zake kwa jina Shabeel Project Services Limited (SPSL) ilipotosha mahakama kuu ndipo ipewe idhini ya kuingia katika ardhi iliyoko jijini Mombasa.

Wakipinga kuuzwa kwa mali za MEL, Mabw Omari na Kinyanjui wamedokeza kwamba mkopo wa Sh Sh631,558,748 ulilipwa kabia lakini benki ya PBL haikuufuta katika vitabu vyake.

Mahadi ilipewa mkopo huo kati ya mwaka wa 2011  na 2017.

Bw Omari alieleza mahakama kwamba benki hiyo iliipa MEL mkopo huo kwa mujibu wa Sheria za Kiislamu almaarufu Sharia Laws.

Wakili huyo alifafanua kwamba chini ya sheria hizi za Kiislamu Benki haipasi kulipisha riba ya juu kwa lengo la kumlaghai mteja muhusika.

“PBL ambayo awali ilikuwa- First Community Bank Limited) iliipa MEL mkopo wa Sh631,558,748,” asema Bw Ibrahim Hussein Mahadi, meneja mkurugenzi wa MEL.

Adokeza zaidi Bw Mahadi:”Mikopo iliyotolewa kwa mujibu wa Sheria za Kiislamu maarufu kama Murabaha na Musharakah (haziruhusu Benki kumfilisi mteja kwa kumtoza faida(Riba) ya juu.”

Bw Omari amefafanua kwamba faida hii ya juu au Riba hutajwa kama ufujaji kwa mujibu wa Sharia.

Mahakama imeelezwa mikopo iliyopewa MEL ilitolewa baada ya hatimiliki za mashamba yaliyoko Mombasa Mainland na mitaa kadhaa iliyoko Nairobi.

Mahadi amefichua amelipa zaidi ya Sh530milioni lakini PBL haijaonyesha katika Stetimendi zake kama amelipa.

Mlalamishi huyo ameeleza kuwa MEL iko na yadi ya kuhifadhi Kontena nyingi za nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Bw Omari alisema kuwa mnada uliofanywa na PBL ulipelekea kampuni ya Shabeel Project Services Limited (SPSL) kununua yadi hiyo iliyoko Mombasa Mainland.

Yadi hii kwa mujibu wa MEL ndiyo ya tatu kwa ukubwa katika eneo hili.

Kufuatia kutwaliwa kwa njia ya mnada kwa Yadi hii sasa MEL haina mahali pa kuweka Kontena zake ambazo wakili alisema ziko na bidhaa ambazo zinawezaharibika.

Bw Omari amesema mtafaruku umetokea baada mahakama kuu kutoa maagizo tofauti.

Mombasa kuu Mombasaa ilikataa kuuzwa kwa Yadi ya Mainland lakini Mahakama kuu ya Nairobi ikaruhusu kutwaliwa kwa yadi hiyo.

Bw Omari amefichua Mahakama kuu ya Nairobi ilifichwa ukweli wa mambo ndipo ikaruhusu yadi kutwaliwa.

MEL inaomba mahakama kuu Nairobi ifutilie mbali agizo la kuruhusu kutwaliwa kwa yadi ya Mombasa Mainland kwa vile ushahidi wote haukutolewa.

Jaji Mohamed Kullow ameagiza Bw Omari awakabidhi washtakiwa nakala za kesi na kutenga Desemba 8,2025 siku ya kusikizwa kwa kesi hii.