Makala

KANDY: Nalenga kumfikia Julia Roberts wa Marekani katika uigizaji

July 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

NI ndoto ya kila msanii kuona anaimarika katika kazi zake na kutambulika kote duniani. Nicholine Adhiambo Odhiambo aachwi nyuma ni miongoni mwa wanadada wanaolenga kujizolea umaarufu hapa nchini na kufikia viwango vya wasanii mahiri duniani.

Ingawa hajapata mashiko anapania kujituma kwa udi na uvumba ili kutinga upeo wa kimataifa. Anaamini anacho kipaji cha kufanya vizuri katika sekta ya maigizo.

Binti huyu maarufu kama Kandy anasema ”Binafsi napenda sana uigizaji maana ni talanta iliyo katika damu yangu ingawa sijasomea masuala hayo nakumbuka nilianza kushiriki maigizo tangu nikisoma shule ya Msingi.”

Kisura huyu anasema analenga kufuata nyayo za mwigizaji wa kimataifa, Julia Fiona Roberts mzawa wa Marekani. Anasema ingawa mwigizaji huyo amefanya kazi nyingi huvutiwa na filamu yake iitwayo Pretty Woman.

Kando na filamu hiyo mwigizaji huyu pia ameshiriki ‘Erin Brockovich,’ ‘Eat pray love,’ ‘Oceans Eleven,’ ‘Notting hill’ na ‘My best friends,’ kati ya zingine.

AUNITE BOSS

Dada huyu mwenye umri wa miaka 27 aliyedhamiria kuhitimu kuwa wakili alivutiwa na masuala ya maigizo miaka mitano iliyopita alipotazama mwigizaji Silprosa alivyoshiriki kwenye filamu ya Auntie Boss iliyopeperushwa kupitia runinga ya NTV.

Kandy anayemiliki brandi ya kuuza nguo kwa jina ‘Rock & Kandy Collection’ mtaani Kayole, Nairobi anajivunia kushiriki filamu kadhaa ikiwamo ‘Life Scar’ ‘Pima Weight’ iliyepeperushwa kupitia runinga ya K24.

Mwana dada huyo anayepania kuanzisha brandi ya kuzalisha filamu anasema angependa sana kukuza vipaji vya waigizaji wanaoibukia.

”Katika mpango mzima uigizaji ni ajira kama nyingine ambapo serikali inastahili kuwekeza zaidi ili kusaidia vijana wanaokuja kwa matarajio mengi tu ya mafanikio,” akasema.

Katika sekta ya uigizaji hapa nchini anawavulia kofia baadhi ya waigizaji wanaofanya kweli na kusema angefurahia sana kufanya kazi nao kama: Pascal Tokodi ‘Selina’ na Sandra Dacha ‘Auntie Boss.’ Kimataifa angependa kufanya kazi na wanamaigizo kama Mercy Johnson ‘Dumebii the dirty girl,’ ‘Heart of a fighter’ pia Jacky Aphia ‘4 Play’ na ‘Heart of men.’

PANDASHUKA

”Kusema kweli hakuna tansia isiona na changamoto. Binafsi nimekumbana na milima na mabonde katika safari yangu fupi katika uigizaji,” alisema na kuongeza kwamba wanawake nyakati nyingi hujikuta pabaya katika harakati za kusaka riziki. Binti huyu anasema mara zingine hufanya kazi na kukosa kulipwa kwa njia isioleweka.

Anakiri kuwa wakati fulani waliporwa simu na matafeli waliokuwa wamewahidi kazi ya kutengeneza filamu.

”Pia nakumbuka niliwahi kusafiri maeneo ya Magharibi mwa Kenya kwa mwezi mmoja lakini nililazimika kugharamia nauli ya kurudi jijini Nairobi baada ya viongozi wetu kusepa bila kutulipa,” alisema.

MAWAIDHA

Anashauri wana dada wanaoibukia anawaambia kuwa wasiwe na pupa ya kuibuka mastaa katika tasnia ya maigizo. Anasema itakuwa vyema kwa wanadada kuwakwepa wanaume ambao hupenda kuwashusha hadhi kwa kuwataka kimapenzi ili kuwapa ajira.

Aidha anawahimiza kuwa nyakati zote wanastahili kujiheshima pia kumweka Mungu mbele kwa chochote wanachofanya.