Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Kiswahili kitafana iwapo wanahabari watazidisha utashi

May 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KEN WALIBORA

WIKI jana katika Taasisi ya Confucius, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kulifanyika kongomana la kihistoria.

Ni kongomano la kwanza kabisa la vyombo vya habari vinavyotumia Kiswahili kutoka pembe zote duniani.

Mgoda wa Kigoda cha Nyerere katika taasisi hiyo Prof Aldin Mutembei alikuwa ndiye mwandalizi mkuu akisaidiwa na Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Dkt Musa Hans na wengine.

Nilishtuka sana Prof Mutembei aliponiomba nitoe mada elekezi ya kongomano; nilihisi kanivika joho ambalo si makamo yangu kulivaa.

Ukumbi ulikuwa umejaa hakuna pahali pa kutema mate, umejaa wanahabari na wanahabari watarajiwa.

Nilifika nikaamka kutoa mada elekezi, nikisema, japo kwa kutetemeka.

Hata hivyo, ilikuwa furaha iliyoje kuwaona wanahabari kutoka pembe mbalimbali wakishauriana kuhusu utendaji wao wa kazi wanapofanya kazi yao kwa kutumia lugha adhimu ya Kiswahili!

Wanahabari hawa waliungamanishwa sio tu na taaluma yao bali na Kiswahili kama wenzo wao wa utendaji kazi.

Tulijadili mengi kuhusu hali ya awali, ya sasa na ya baadaye ya Kiswahili katika vyombo vya habari. Tulijaribu kujibu swali Kiswahili kilikuwaje, kikoje, na kitawakuwaje katika mustakabali wake.

Ucheshi

Midahalo ilikuwa wazi, nyeti na yenye ucheshi sawia.

Aghalabu kila mtu katika hadhira alivutiwa na hotuba kama ile ya Austere Malivika kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliyesimulia kwa kina kuhusu kuripoti kutoka uwanja wa vita. Aliwashtua wengi kwa ujasiri wake wa kutafuta habari katika mazingira hatarifu sana ambapo mpaka uliopo kati ya kufa na kuishi ni mdogo kabisa.

Naye Kauthar, mwanamke mzawa wa Pemba akawazuzua watu kwa utetezi wake wa wanawake wanahabari. Aliuponda sana mfumo wa ubabedume ulioshamiri hata katika vyombo ambavyo vinatumia Kiswahili.

Labda sasa unajiuliza nami nilitoa hoja zipi katika mada yangu elekezi? Nilitaka nikuambie kwamba usafiri wangu wa kwenda Dar ulikorofisha -nikaachwa na ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta. Kisa na maana? Sikusoma vizuri tiketi yangu na wakati ndege yangu inaondoka, nilikuwa Huduma Centre, Nairobi ninafuatia Namba yangu ya Huduma. Ila sasa utasema na hilo linahusu nini kongomano? Kwa hiyo acha nikupe muhtasri wa hotuba yangu.

Mada yangu ilikuwa “Tafakuri kuhusu mustakabali wa Kiswahili katika vyombo vya habari.”

Kwa kuchelewa kufika niliitoa Jumamosi badala ya Ijumaa. Ila muhimu ni kwamba nilisisitiza kwamba Kiswahili kitafana tu endapo wanahabari watakuwa na utashi wa kukiendeleza, wanahabari waliosimama kidete kukifia Kiswahili.

Nilitoa mifano ya mikota wa zamani wa tasnia hii ya uanahabari kama vile Salim Mbonde, Sera Ndumba, Abdul Ngalawa, Leonard Mambo Mbotela, Daniel Njuguna Gatei na Elizabeth Obege ambao walijitolea kusarifu lugha kwa ufasaha.

Nilikosoa tabia za watangazaji kupachapika ovyovyo maneno ya Kiingereza kama mtangazaji aliyesema nikiwa Dar: “Kipa Manulla ana-doubt marking ya Mohamed Hussein. Naam, baadhi ya wanahabari lao kubwa ni kukiua Kiswahili.