Makala

Kauli za kukanganya kuhusu padre aliyeuawa madai ya deni yakiibuka

Na WAIKWA MAINA, MERCY KOSKEI May 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KAULI zinazokinzana na usiri zinaendelea kuficha ukweli halisi wa matukio yaliyopelekea kifo cha Kasisi John Maina wa Parokia ya Igwamiti.

Kwa kukosekana kwa ripoti ya uchunguzi wa maiti itakayosaidia wachunguzi kubaini chanzo cha kifo chake, polisi sasa wanategemea maelezo ya watu waliowasiliana na kasisi Maina dakika za mwisho kabla ya kifo chake.

Vyanzo kutoka kwa timu ya wachunguzi katika kituo cha polisi cha Gilgil viliambia Taifa Leo kwamba padri huyo alidaiwa kupewa sumu, na alipofika Hospitali ya St Joseph huko Elementaita mnamo asubuhi Mei 15 kwa pikipiki, aliwaambia wauguzi kuwa alikuwa amepewa sumu.
Alifariki dunia alipokuwa akipokea matibabu.

Mhudumu wa boda boda ambaye hakutaka kutajwa jina alisema alikuwa anatoka Mji wa Gilgil kununua vipuri alipomwona mtu akiwapungia mkono kando ya barabara.

Alisema alisimama, na alipokaribia zaidi, alimuona mwanaume aliyekuwa katika hali ya dhiki akiomba msaada akidai kuwa alikuwa anahitaji huduma ya matibabu.

Alisema mtu huyo alimwambia kuwa alikuwa amepewa sumu bila kufichua ni nani aliyefanya hivyo na kwa nini.

Kwa msaada wa mwendesha boda boda mwingine aliyesimama eneo hilo pia, walimkimbiza mtu huyo hospitalini ambapo alipokelewa katika sehemu ya dharura.

“Nilikuwa tu ninamsaidia kama Msamaria Mwema kwani aliniambia anahitaji matibabu ya haraka. Hospitalini, wauguzi walimpokea, kisha tukaondoka. Baadaye, nilikuja kugundua kuwa mtu niliyemsaidia alikuwa padri na tayari alikuwa amefariki,” alisema boda boda huyo.

Kwa mujibu wa mwendesha boda boda huyo, Padri Maina alikuwa na jeraha la wazi upande wa kushoto wa kichwa.

“Alikuwa amevaa kandambili na koti la rangi ang’avu. Hakuwa na simu. Nilijaribu kumuuliza ili kuwasiliana na watu ambao tungeweza kupigia, lakini hakuwa anajibu. Hakuwa na majeraha mengine sehemu nyingine za mwili,” alisema wakati wa mahojiano ambapo aliomba jina lake lisitajwe kwa kuwa bado hajatambuliwa rasmi kama shahidi na kwa hofu ya kuathiri uchunguzi.

Ripoti ya awali, iliyotokana na mahojiano na maafisa wa upelelezi, kwa kuwa bado haijatolewa hadharani, ilipendekeza kuwa padri huyo alipigwa risasi mara kadhaa. Hata hivyo, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Jumanne ilisema padri huyo alipatikana na “majeraha ya wazi, ikiwemo michubuko upande wa kushoto wa kichwa, ambayo ilikuwa ikitoka damu,” alipopatikana na mwanabodaboda aliyempeleka hospitalini.

Maafisa wa upelelezi pia wanaamini kwamba Padri huyo aliwahi kumwambia rafiki yake kuwa maisha yake yalikuwa hatarini — madai ambayo familia yake na kanisa wanayakana vikali.

“Padri Maina alimwambia rafiki yake wa kike, ambaye walikuwa wamejuana kwa miaka minne, kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wakimfuatilia lakini hakufichua ni nani na kwa nini,” chanzo kilisema.

Polisi wanasema Padri Maina pia alimwambia rafiki huyo kuwa alipokea Sh400,000 kama zawadi kutoka kwa Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua, ambaye alimwalika wiki mbili kabla ya kifo chake.

“Alianza kufuatwa baada ya kile kinachodaiwa kuwa mchango uliotolewa katika sherehe za maadhimisho ya miaka 25 ya kanisa. Wavamizi walidai kwamba alikuwa amepewa Sh4 milioni Walitaka Sh 2 milioni,” alieleza mchunguzi.

Alipotoka nyumbani Mei 14, Padri Maina aliacha gari lake nyumbani.

Mjakazi wake alidai kwamba Padri aliondoka siku hiyo akisema alikuwa anakutana na marafiki mjini Nyahururu.

Rafiki huyo alieleza kwamba katika muda wa mwisho kabla ya Padri Maina kutoweka, alimwita akisema alikuwa na wasiwasi kwamba alikuwa anafuatwa na  walikuwa wakimtaka awe na pesa taslimu Sh 2 milioni  wakati wa kukutana nao.

Wachunguzi wanasema simu ya Padri Maina ilizimwa akiwa Nyahururu Mei 14, na kuna uwezekano mkubwa kuwa wavamizi waliichukua.

Polisi pia wanashuku kwamba Padri Maina alikuwa katika hali ya kutafuta pesa kwa haraka baada ya kuchukua Sh2 milioni  kutoka akaunti ya parokia bila saini ya wengine kununua gari, jambo ambalo liligonga mwamba.

Kwa hali ya kukata tamaa, alikuwa anatafuta njia ya kurudisha pesa hizo kwa kanisa; aliuza gari lake kwa Sh720,000 na rafiki yake akamkopesha Sh150,000 ili kulipia sehemu ya deni hilo.

“Alikuwa na mfadhaiko mkubwa  kuhusu jinsi ya kupata pesa ya kumaliza deni. Alikuwa na matumaini kuwa angepata pesa kutoka kwa shughuli ya kanisa,” rafiki huyo wa kike aliambia polisi.

Huko Nyahururu, Askofu Joseph Mbatia amekanusha madai ya Idara ya Upelelezi wa Jinai kuwa Padri John Maina wa Parokia ya Igwamiti aliwahi kusema kuwa maisha yake yalikuwa hatarini.

Katika mahojiano na Taifa Leo Askofu alisema hakuwahi kupokea malalamishi yoyote kutoka kwa padri huyo, na kwamba hakuwahi kuonyesha dalili zozote za hofu au msongo wa mawazo.