OBARA: Kaunti ya Mombasa inakosea kupuuza wawekezaji wadogo
Na VALENTINE OBARA
SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa kwa miezi kadhaa sasa imekuwa ikijivunia jinsi utalii unavyofufuliwa katika kaunti hiyo.
Sekta hiyo iliathiriwa sana tangu Kenya ilipokaza kamba kupambana na ugaidi na kutuma wanajeshi wake Somalia, hasa kuanzia mwaka wa 2011.
Katika kipindi hicho, magaidi wa kundi la Al-Shabaab walianza kutekeleza mashambulio humu nchini na kusababisha watalii kuepuka kuzuru Kenya kwa wingi ilivyokuwa awali.
Kaunti zilizo Pwani ambapo utalii umekuwa tegemeo kuu na kitega uchumi kwa miongo mingi ziliathiriwa mno, Mombasa ikiwa miongoni mwa zile zilizoathiriwa zaidi.
Lakini kwa miezi kadhaa sasa, kumekuwa na matumaini ya ufufuzi wa sekta hiyo. Matumaini hayo yametokana na makongamano makuu yanayoandaliwa katika kaunti hiyo karibu kila wiki, na pia ongezeko la mashirika ya ndege yanayoleta wageni kutoka maeneo mbalimbali nchini na hata kimataifa.
Unapotazama maendeleo haya yote, utatarajia kwamba mwananchi wa kawaida anayeishi Mombasa pia atanufaika kutokana nayo. Lakini ukweli ni kuwa hali ni tofauti.
Kwa kawaida dhana iliyopo ni kuwa ajira zinazopatikana moja kwa moja katika sekta ya utalii, kama vile nafasi za ajira hotelini, hutosha kuthibitisha kwamba utalii unaleta manufaa kwa wakazi.
Iwapo tunataka kuona mwananchi anayeishi Mombasa ananufaika kutokana na ustawishaji wa sekta ya utalii, ni sharti apewe uwezo wa kufanya hivyo bila kutegemea ajira za moja kwa moja.
Ushirikiano
Utalii unaweza kusaidia sana wakazi wakipewa nafasi za kushirikiana na mashirika ambayo yanahusika moja kwa moja katika sekta hiyo, kama vile hoteli.
Wakazi ndio wanapaswa kutegemewa kusambaza mahitaji muhimu ya mashirika hayo kama vile vyakula, vinywaji, huduma za usafiri na mengineyo.
Kinachosikitisha ni kwamba Serikali ya Kaunti ya Mombasa imezidi kufanya hali iwe ngumu mno kwa mwananchi wa kawaida kuendeleza biashara zake ndogo ndogo kwa njia itakayomletea faida.
Ada nyingi zinazotozwa na serikali ya kaunti hii, mbali na malalamishi ya baadhi ya wafanyabiashara kuhusu maafisa wa kaunti wapendao mlungula, ni masuala ambayo yanarudisha nyuma uwezo wa serikali hiyo kuondolea wakazi umaskini.
Serikali yoyote ile, iwe ni ya kaunti au kitaifa, huwa na jukumu kubwa la kuweka mandhari bora kuvutia wawekezaji.
Kwa bahati mbaya, Kaunti ya Mombasa inavyoonekana kwa sasa inajishughulisha zaidi kuweka mandhari bora ya kuvutia wawekezaji wakubwa, huku wale wajasiriamali wadogo wakibebeshwa mzigo mzito wa ada zisizo na maana.
Haitakuwa busara kuvutia wawekezaji wakubwa wachache ikiwa idadi kubwa ya wakazi, hasa vijana na wanawake, watasukumwa pembeni na kuachwa bila kazi wakilazimika kufunga biashara zao.
Serikali ya Kaunti ya Mombasa ikumbuke kuwa vijana wanaposhindwa kushughulika kazini au katika vibarua ndipo maovu tele huwakujia akilini na kuwalazimu kushiriki katika uhalifu ambao matokeo yake ni kuathiri uwekezaji huo mkubwa ambao kaunti inajaribu kuvutia.