ONYANGO: Kenya itakuwa jangwa tusipolinda misitu kwa makini
Na LEONARD ONYANGO
Kwa Muhtasari:
- Lori lililokuwa limebeba makaa kutoka Tana River kuelekea Nairobi liliteketezwa
- Gavana Ngilu amessisitiza ataendelea kutekeleza sheria inayopiga marufuku uchomaji wa makaa na uvunaji wa mchanga
- Msitu wa Mau huenda ukaangamia kutokana na uharibifu wa misitu kupitia uchomaji makaa
- Kuna uhaba wa mvua nchini na ikiwa serikali za kaunti na kitaifa hazitaingilia kati kuzuia ukataji wa miti, Kenya itakuwa jangwa
GAVANA wa Kitui Charity Ngilu amegonga vichwa vya habari katika siku za hivi karibuni kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya uchomaji wa makaa.
Hii ni kufuatia tukio la Alhamisi iliyopita ambapo lori lililokuwa limebeba makaa kutoka Tana River kuelekea Nairobi kuteketezwa na wakazi wa kaunti ya Kitui.
Baadhi ya wanasiasa kutoka Kiambu, hata hivyo, wametoa wito wa kutaka Bi Ngilu akamatwe kwa ‘kulenga’ jamii fulani katika vita dhidi ya uchomaji wa makaa.
Lakini Gavana Ngilu ameshikilia kuwa ataendelea kutekeleza sheria inayopiga marufuku uchomaji wa makaa na uvunaji wa mchanga kiholela kwa lengo la kulinda mazingira.
Tatizo sugu
Japo ni kinyume cha sheria kujichukulia sheria mkononi na kuteketeza mali ya watu, tukio hilo la Kitui linafaa kuchochea mjadala kuhusu tatizo sugu la uchomaji wa makaa na umuhimu wa kutunza misitu nchini.
Kaunti ya Kitui inafaa kuwa kichocheo kwa kaunti nyingine nchini kubuni sheria kali za kudhibiti uchomaji wa mkaa unaosababisha uharibifu wa misitu na mazingira.
Kwa mfano, wanaharakati wa kutetea mazingira wanakadiria kuwa zaidi ya magunia 1,000 ya makaa yanasafirishwa kila siku kutoka msitu wa Nyakweri, Kaunti ya Narok kuelekea miji ya Nairobi, Kisii, Narok, Kisumu na hata katika taifa jirani la Sudan Kusini. Hiyo inamaanisha kuwa msitu huo utasalia jangwa ikiwa hali hiyo itaendelea kwa miaka michache ijayo.
Wataalamu pia wanaonya kuwa Msitu wa Mau ambao ni chanzo cha maji nchini pia huenda ukaangamia kutokana na uharibifu wa misitu kupitia uchomaji makaa.
Hatari ya kuwa jangwa
Takwimu za Umoja wa Mataifa (UN) zinaonyesha kuwa maeneo yaliyofunikwa na misitu nchini Kenya yanapungua kwa kasi.
Ripoti ya UN iliyotolewa miaka mitatu iliyopita ilionyesha kwamba misitu imepungua kwa zaidi ya asilimia 20 ikilinganishwa na miaka ya tisini.
Uchomaji wa makaa ni hatari na Kenya iko katika hatari ya kuwa jangwa katika kipindi cha miongo miwili au mitatu ijayo. Hiyo inamaanisha kuwa kizazi kijacho kitarithi jangwa kutoka kwa kizazi cha sasa.
Tayari Kenya inakabiliwa na uhaba wa mvua na hali huenda ikawa mbaya zaidi ikiwa serikali za kaunti na kitaifa hazitaingilia kati kuzuia ukataji wa miti kiholela.
Ni kweli kwamba familia nyingi maskini zinategemea biashara ya makaa kujikimu kimaisha. Lakini serikali ina jukumu la kubuni njia mbadala za kuwaletea wakazi mapato bila kuharibu mazingira.