Makala

‘Kiburi FC’ na Ten Hag wapumua Manchester United ikizima Brentford

Na GEOFFREY ANENE October 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MASHABIKI wa Manchester United sasa wanaweza kupumua na kujipiga kifua kuwa timu yao ni kubwa baada ya kutoka nyuma na kuliza Brentford 2-1 ugani Old Trafford mnamo Jumamosi, Oktoba 19, 2024.

Vijana wa kocha Erik ten Hag hawakuwa na ushindi katika michuano mitano mfululizo kabla ya kuzamisha Brentford kupitia mabao ya Alejandro Garnacho (dakika ya 47) na Rasmus Højlund (62).

United walijipata chini 0-1 sekunde chache kabla ya kipindi cha kwanza kukatika baada ya Ethan Pinnock kukamilisha kona ya Mikkel Damsgaard.

Lisandro Martinez, Garnacho na Christian Eriksen walipoteza nafasi kadhaa nzuri kwa kumjaribu kipa Mark Flekken katika kipindi hicho, huku kipa wa United, Andre Onana pia akilazimika kuondosha kombora la Christian Norgaard.

Ten Hag na beki wake Jonny Evans walionyeshwa kadi ya njano baada tu ya Pinnock kupachika bao kutokana na kona kwa kulalamika.

Rashford alichanjia Garnacho krosi safi iliyozalisha bao dakika ya pili ya kipindi cha pili.

Mashetani wekundu walizidisha kasi na mashambulizi wakimjaribu tena Flekken mara kadhaa kabla ya kuchukua uongozi kutoka kwa Holjund aliyepata bao lake la kwanza msimu huu wa 2024-2025 baada ya kukamilisha pasi ya nahodha Bruno Fernandes.

United walikuwa nafasi ya 14 kabla ya ushindi huo unaowapaisha hadi nambari 10 kwa alama 11 nao Brentford wameshuka nafasi moja hadi nambari 12 wakiwa na pointi 10.

Spurs wang’aa

Katika mechi nyingine zilizosakatwa, Tottenham walipepeta West Ham 4-1 baada ya kutoka nyuma.

Mohammed Kudus aliyefungia wageni West Ham dakika ya 18 alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 86 kwa utovu wa nidhamu.

Tottenham walipata mabao kutoka kwa Dejan Kulusevski, Yves Bissouma na Son Heung-min na pia kipa wa West Ham, Alphonce Areola kujifunga.

Fulham wajilaumu

Fulham pia walitupa uongozi wakichapwa na Aston Villa 3-1 kupitia mabao ya Morgan Rodgers, Ollie Watkins na bao la kujifunga kutoka kwa beki Issa Diop.

Andreas Pereira aliuza penalti ya Fulham dakika ya 26.

Fulham walicheza dakika 36 za mwisho wachezaji 10 baada ya beki Joachim Andersen kulishwa kadi kwa kutega mchezaji wa Villa iliyomaliza mchuano watu 10 Jaden Philogene alipoonyeshwa kadi nyekundu dakika ya mwisho.

Saints hawakuwa na lao

Southampton nao walikubali kichapo kutoka kwa wageni Leicester 3-2. Saints waliongoza 2-0 baada ya kupata mabao kutoka kwa Cameron Archer dakika ya nane na Joe Aribo (28), huku Facundo Buonanotte akiwapa Foxes matumaini kwa kurejesha goli moja dakika ya 65.

Southampton waliporomoka Ryan Fraser alipolishwa kadi nyekundu dakika ya 73.

Jamie Vardy alisukuma wavuni penalti iliyopatikana kabla ya Jordan Ayew kufunga bao la ushindi dakika ya nane ya majeruhi.

Ipswich yazimwa

Everton walichapa wenyeji Ipswich 2-0 kupitia mabao ya kipindi cha kwanza kutoka kwa Iliman Ndiaye na Michael Keane naye Danny Welbeck akazolea Brighton alama zote tatu alipofunga wenyeji Newcastle dakika ya 35.

Ratiba na matokeo ya EPL (Uingereza):

Oktoba 19 – Tottenham 4-1 West Ham (2.30pm), Ipswich Town 0-2 Everton (5.00pm), Manchester United 2-1 Brentford (5.00pm), Fulham 1-3 Aston Villa (5.00pm), Newcastle 0-1 Brighton (5.00pm), Southampton 2-3 Leicester (5.00pm), Bournemouth vs Arsenal (7.30pm);

Oktoba 20 – Wolves vs Manchester City (4.00pm), Liverpool vs Chelsea (6.30pm); Oktoba 21 – Nottingham Forest vs Crystal Palace (10.00pm)