KILIMO: Ukiwa na kiini cha maji, kilimo kina faida tele
Na SAMMY WAWERU
KATIKA kipande kimojawapo cha shamba anachuma tunda linaloaminika kuongeza damu mwilini kwa Kiingereza tree tomato, analimenya na kumumunya juisi yake ya ndani kwa ndani.
Nje, matunda haya ni mekundu yanapoiva, na mengine manjano.
Ndani sharubati yake pia ni nyekundu na ya manjano. Moja linakadiriwa kuwa na zaidi ya mbegu 300.
David Karira ana kila sababu ya kutabasamu akiona fanaka yake katika kilimo.
“Utamu wa kilimo ni kuona mazao yaliyonawiri na kupamba shamba,” anasema mkulima wa Karatina, eneobunge la Mathira, Kaunti ya Nyeri.
Tree tomato kwa jina lingine tomarillo, mbali na kuyapanda katika shamba lake pekee, ameyapanda katika mikahawa.
“Matunda haya hayana kikwazo kwa kuyakuza kati ya mimea mingine,” athibitisha Bw Karira, ambaye ni baba wa watoto watatu.
Pembezoni mwayo, ana kifungulio (greenhouse), ambacho hapo ndani hukuza pilipili mboga (capsicum), zao analosema lina mapato ya kuridhisha.
Karira ambaye pia ni mwalimu wa shule moja ya msingi Mathira, aliwekeza katika kilimo 2011 ili kujipa kipato cha ziada. Kufikia sasa hajutii kamwe uamuzi huo, kwani ameonja matunda ya juhudi zake.
Hata hivyo, nyayo alizopiga mbele kizaraa anazionea fahari kwa kutafuta kiini cha maji. Kando ya kifungulio, ana shimo la maji lenye urefu wa zaidi ya futi 100.
Ameliimarisha kwa kulifunika kwa sarufi ili kuepuka hatari za yeyote kuangukia mle, haswa watoto. Juu yake, ameinjika tenki la maji, ambalo lina mifereji iliyotumbukizwa ndani kuunganishwa na nguvu za umeme, ili kuyapampu.
Kenya ni kapu la kilimo, na kinachozima ari ya wakulima wengi ni ukosefu wa maji. Kulingana na mkulima huyu ni kuwa kabla awazie kuchimba shimo la maji, alikuwa akikadiria hasara kila msimu kwani gharama ya uzalishaji ilikuwa juu kuliko mapato aliyopokea.
“Siri ya kufanikisha kilimo ni kuwa na kiini cha maji, na hivyo ndivyo usalama wa chakula utaafikiwa nchini,” anaeleza.
Sauti ya mtaalamu
Kauli yake inatiliwa mkazo na Lawrence Ngugi, mtaalamu wa kilimo kutoka Hygrotech, kampuni ya utafiti wa bidhaa za kilimo.
“Kwa kuwa mvua hunyea kwa misimu, kuwepo kwa kiini cha maji kama mashimo, mabwawa, vidimbwi na mito, itakuwa rahisi wakulima kukumbatia mfumo wa kulima kwa mifereji,” anasisitiza Bw Ngugi.
David Karira anatumia mfumo wa mifereji kuendesha shughuli za kilimo, na kila mwezi hakosi kufanya mauzo ya mazao.
Mwae Malibet, ni mkulima wa mboga Kiambu na ambaye hutumia maji ya shimo la maji alilochimba. Eneo la Gachie, barobaro huyu ndiye tegemeo la mboga.
“Ukulima ndio ofisi yangu. Nilipotatua ukosefu wa maji kwa kuchimba mashimo kadhaa, kilimo ninachofanya kiliimarika,” anaeleza Malibet.
Mojawapo ya nguzo kuu nne za Rais Uhuru Kenyatta ni kuhakikisha taifa lina chakula cha kutosha.
Ikizingatiwa kuwa uchimbaji wa mabwawa ni bei ghali, serikali inapaswa kutathmini suala hilo na kutumia fedha inazomudu kuchimba mashimo tele ya maji.
Mkulima huyu wa Nyeri aliambia Taifa Leo kwamba ilimgharimu karibu Sh200,000 kuchimba shimo lake la maji, na ambalo ni nadra kuisha maji hata msimu wa kiangazi. “Mbali na kutumia maji yake kufanya kilimo, huyatumia katika matumizi ya nyumbani,” anadokeza.
Ni muhimu vyanzo vya maji kama vile misitu kulindwa. Serikali inahimizwa isilegeze kama katika marufuku ya ukataji miti kiholela. Mito mingi nchini imekauka kwa sababu ya uharibifu wa misitu.