Kilio cha maji: Wakazi wa Garissa waandamana
WAKAZI wa mji wa Garissa wameandamana huku wakilalamikia ukosefu wa maji katika vijiji vyao na kuitaka serikali ya Kaunti na ya Kitaifa kuhakikisha matatizo yao yametatuliwa.
Wakazi wa vijiji vya Bula Quba, Sumeya, Forest, Burburis, Ifran na Qumujo walilalama kuwa serikali zote mbili zimewasahau kimaendeleo baada ya kupiga kura.
Wakiongozwa na Sheikh Hassan Amey, wakazi hao wameitaka serikali ya kaunti ya Garissa kuhakikisha kuwa sehemu zote zinapata maendeleo sawa.
“Tuko barabarani kwa sababu hatuna maji katika vijiji sita vya eneo hili. Kwa muda mrefu sana tumewasilisha malalamiko yetu kwa wakuu wa serikali ya kaunti na ile ya kitaifa lakini hatujapata suluhu,” Bw Amey alisema.
Bw Amey alidokeza kuwa wakazi wa wadi ya Galbet wamekuwa wakinunua maji kwa shilingi elfu sita kwa lori huku bomba la maji likipita katika vijiji hivyo hadi Modika.
“Inakuwaje bomba la maji linapita hapa kufikisha maji kwenye kambi ya jeshi ilihali sisi ambao ni wengi hatuna maji?” Bw Amey aliuliza.
Mwakilishi wa Wadi ya Galbet, Abubakar Khalif akiunga mkono maandamo hayo alisema serikali ya Kaunti ina mipango ya kusambaza maji katika eneo hilo kame.
“Kuandamana ni lugha ya kisiasa na ujumbe hufikia mlengwa kwa haraka. Ninafahamu kuwa mipango ipo katika bajeti ya mwaka ujao kuhakikisha maji yatafikishwa katika eneo hilo,” Bw Khalif alisema.
Kulingana na Mwakilishi Wadi huyo, mradi wa kusambaza maji katika mji wa Garissa umecheleweshwa na ukosefu wa fedha.
Bi Salima Ali alisema ukosefu wa maji umewasumbua kwa muda mrefu.
“Nimeishi katika eneo hili kwa muda wa miaka tisa bila maji na kila siku lazima ninunue maji kwa lori. Watoto wangu huhangaika kila asubuhi kujitayarisha kwenda shuleni kwa kukosa maji,” alisema.
Mama huyo aliitaka serikali ya kaunti kusambazia akina mama maji nyumbani ndipo waweze kulea watoto wao vyema.
“Sisi kama akina mama tunahitaji maji kila sekunde ya maisha yetu. Tunahitaji kupika na kufanikisha usafi wa nyumbani kwa jumla. Ukosefu wa maji ni aibu kubwa kwa sisi akina mama,” alisema.
Bw Mohamed Sahal, aliyekuwa mwakilishi Wadi ya Galbet alisema ni ajabu kuwa zaidi ya miaka kumi ya serikali za kaunti bado eneo hilo halina maji.
“Maendeleo katika eneo hili yanategemea jamii na uhusiano na gavana. Sisi kama wakazi wa eneo hili tumekosa maendeleo kwa sababu ya ubaguzi,” alisema.
Bw Sahal aliwataka viongozi wote waliochaguliwa katika eneo la Garissa kuhakikisha kuwa wanafanyia maendeleo watu wote bila mapendeleo.