Kinaya Raila kushikilia hana handisheki na Ruto
KINARA wa upinzani Raila Odinga amekanusha ripoti kwamba ana handisheki yoyote na Rais William Ruto, akisema alichofanya ni kuzuia nchi kutumbukia katika machafuko kufuatia maandamano ya Gen Z yaliyosababisha umwagaji wa damu.
Bw Odinga amelaumiwa kwa kunufaika na damu ya vijana wa Kenya walioandaa maandamano ya kupinga mswada wa fedha 2024 mwezi Juni na kuwa sehemu ya utawala wa Rais Ruto wa Kenya Kwanza.
Lakini akizungumza katika mahojiano kwenye runinga ya Citizen Ijumaa usiku, kiongozi huyo wa ODM alitaja kama ‘tuhuma isiyo na msingi,’ madai kuwa alinufaika na maandamano ya Gen Z.“Hayo yamekuwa madai yasiyo na msingi yanayotolewa na vyombo vya habari. Sijafaidika. Kilichotokea ni hitaji la kuhusisha jamii pana katika utawala na kumpa Rais Ruto baadhi ya watu kutoka chama chetu.
“Nilishauriana na wenzangu wengine katika muungano wa Azimio na wengine walikuwa tayari na wengine hawakuwa tayari. Kisha nikatuma baadhi ya watu wetu kwa serikali kufanya kazi. Lakini haikuwa kama kuunda mapatano au muungano kwa sababu hatukujadiliana kwa msingi wa muungano,” Bw Odinga akaeleza
.Aliendelea: “Kwa hivyo, watu hawa kimsingi waliajiriwa tu na ilibidi wavue nyadhifa zao kwenye chama lakini si uanachama. Wanasalia kuwa wanachama wa chama cha ODM.”
Bw Odinga alikuwa akizungumzia kujumuishwa kwa baadhi ya viongozi wakuu wa ODM katika ‘baraza la mawaziri la Rais Ruto mnamo Julai.Wao ni waliokuwa naibu viongozi wa chama cha ODM Hassan Joho na Wycliffe Oparanya, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitaifa wa ODM John Mbadi na aliyekuwa Katibu wa Masuala ya Kisiasa Opiyo Wandayi pamoja na aliyekuwa mwanachama wa bodi ya uchaguzi ya chama hicho Bi Beatrice Askul.
Bw Joho aliteuliwa kuwa Waziri wa Madini, Uchumi wa Majini na Masuala ya Bahari, Bw Oparanya kuwa Waziri wa Ushirika, Bw Mbadi aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango ya Uchumi, Bw Wandayi ni Waziri wa Kawi na Petroli huku Bi Askul akisimamia wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Maendeleo ya Kikanda.
Zaidi ya hayo, Rais Ruto hivi majuzi aliteua washirika zaidi wa Bw Odinga kuchukua nyadhifa za serikali.Prof Adams Oloo, Bw Joe Ager na Dkt Sylvester Kasuku – washirika wote wa Bw Odinga – sasa ni sehemu ya Baraza la Washauri wa Kiuchumi la Rais Ruto.
Mshauri wa mikakati
Prof Oloo atakuwa Mshauri wa Mikakati na Mawasiliano huku Dkt Kasuku akishughulikia Utawala. Bw Ager atakuwa Katibu wa Utawala.Bw Ager na Prof Oloo walikuwa katika timu iliyoanzisha mapatano kati ya Rais Ruto na kiongozi huyo wa ODM, na kusababisha wanasiasa wa upinzani kujiunga na Baraza la Mawaziri.
Prof Oloo amekuwa mshauri wa Bw Odinga kwa miaka mingi na alitekeleza majukumu muhimu katika kampeni zake za urais na pia alihudumu katika timu ya kiufundi ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo.
Dkt Kasuku aliwahi kuwa Katibu wa Mradi wa Miundombinu na Lapsset katika Ofisi ya Waziri Mkuu wakati huo.Wakati wa mahojiano yake Ijumaa, Bw Odinga hata hivyo, alikanusha kuwa na mapatano yoyote na Rais Ruto, akirejelea maandamano ya Juni ambayo alisema kuwa yalikuwa na uwezo wa kusababisha nchi kuingia katika machafuko.
“Hatukusaidia kuokoa meli inayozama(serikali). Usilofahamu ni kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa sana wa nchi kutumbukia katika machafuko ambayo yangeweza kuwa hatari sana.’Unaweza kuona kile kilichotokea Misri na Libya wakati wa msukosuko wa Kiarabu. Ikiwa hatungekuwa waangalifu mpango huo ungeweza kutokea hapa kwa urahisi,” Bw Odinga alisema.
Hatuna makubaliano
Vile vile, alimwondolea Bw Kenyatta madai hayo baada ya washirika wake pia kujumuishwa katika baraza la mawaziri hivi majuzi.“Sijisalimiana na Ruto kwa sababu hatujaafikiana katika maandishi. Handisheki niliofanya na (rais wa zamani) Mwai Kibaki kisha baadaye na Uhuru Kenyatta – tulitia saini makubaliano ambayo yaliishia kutolewa kwa ripoti. Tulijitokeza hadharani mbele ya afisi ya rais na tukasalimiana rasmi na Uhuru, kama tulivyofanya na Kibaki,” kiongozi huyo wa ODM alisema.
Alisema Bw Kenyatta ‘alimsalimia Ruto,’ lakini hakuwahi kwamba watafanya kazi pamoja.’Wakati wa kuwaleta washirika wa Uhuru, rais Ruto alisema anataka kuunda serikali ambayo itawakilisha nchi nzima.“Alianza alipopata baadhi ya watu kutoka ODM, na sasa wengine kutoka Jubilee. Hii sio handisheki, ni kupanua tu serikali yake,” aliongeza Waziri Mkuu huyo wa zamani.
IMETAFSIRIWA Na BENSON MATHEKA