MakalaSiasa

KINAYA: Raila, Ruto kutongozana kuna ukweli fulani haijalishi aliyeanza mwingine

April 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA DOUGLAS MUTUA

VUNJA mtu shingo! Nani? RAO… subiri kidogo. Daktari wa Sugoi! Naam, wote wawili. Wana nini? Nawahimiza wavunjane shingo, walane hata maini! Si ndugu zangu hao!

Nimekaa nikajiambia siwezi kutetea wajanja wawili wa kisiasa, hivyo nikaamua kuwahimiza wacharurane vilivyo, mwanamume kamili asalie hai tuendelee na safari.

Mbona tena? Ala! Hujasikia wakilaumiana eti kila mmoja alimwendea mwenzake usiku wa kiza kama Nikodema wa Biblia alivyowendea Yesu Kristo kutangaza anamtambua?

Daktari wa Sugoi – maarufu kwa kuwa kiguu na njia kote nchini mpaka mkuu wake akampagaza msimbo wa jina ‘Kijana wa Kutangatanga’ – amepasua mbarika!

Amedai RAO alijaribu kumshawishi kisiri mwaka jana, eti waanzishe ushirikiano wa kisiasa ili wamhini ‘Kamau wa Pili’ na watu wake.

Lo! RAO naye kusikia hayo ameruka juu kama aliyeng’atwa na mbung’o, akasema ‘kijana mtundu wa Sugoi uliyaanza wewe mwenyewe!’

Hiki sasa kimekuwa kama kile kisa anachopenda kuhadithia sana RAO: Mwizi kuparura simu ya mtu na kutimka huku akisema ‘mwizi! mwizi’ kana kwamba anamkimbiza.

Ukweli usemwe – RAO na Daktari ni wanasiasa wajanja sana wanaopenda kujipanga mapema kabla ya kupangwa.

Usinikumbushe kwamba RAO amepangwa mara kadhaa akapangika sawasawa, labda si kweli. Wapo wafuasi wake wanaoamini kwamba yeye hushinda ila kura zake huibwa.

Huo ni mjadala tofauti unaohitaji siku nzima kukamilisha, lakini nakuachia tafakuri: I wapi mantiki ya mtu kutafuta punje za mahindi mwaka mzima na kuwaachia kuku kuzidonoa kwa dakika? Kuna tatizo hapo.

Haya basi, sasa turejee kwenye majaribio, au madai ya majaribio, ya wajanja wawili wakuu nchini kujaribu kuwaigiza Nikodema na Kristo.

Wewe utamwamini nani? Sijali maoni yako kwa maana nami nina akili zangu pia, lakini haidhuru kuulizana. Ni vyema ukajiuliza maswali kadhaa kabla ya kujibu swali langu hilo.

Hata hivyo, hata kabla hujajiuliza swali lolote, naomba nikusadikishe kwamba wawili hao wana uwezo mkubwa wa kufanya mambo wanayolaumiana kutenda.

Kwanza, nilikwambia tangu mwanzo kwamba Daktari angetaka kujipanga mapema ili akisalitiwa na kina mwana wa Mlima Kenya, wakatae na deni lake, awaonyeshe kivumbi.

Kuna uwezekano kwamba alijua RAO, hoi na mwingi wa hasira baada ya kutiwa pilipili machoni katika kinyang’anyiro cha urais mnamo 2017, angetaka kulipiza kisasi dhidi ya ‘Kamau wa Pili’.

Pengine alijua RAO, dhaifu kupindukia wakati huo, angekubali hata mfupa wa mwaka jana mkavu na usio na nyama badala ya kutoka bure-bure. Kumbuka RAO anapenda sana mkate-nusu na mkeka.

Vilevile, namini kuna uwezekano kwamba RAO hakumsahau aliyemnyima urais mnamo 2013, ambaye bila shaka ni Daktari, na alitamani kumtia kitanzi ghafla!

RAO anajua fika kuwa Daktari angedumu naye, mwana huyo wa Jaramogi angelala Ikulu kuanzia 2013 mpaka 2022.

Swali la msingi kujiuliza ni kwa nini sasa wawili hao wakaitunza siri hiyo ya kujaribu kupatana gizani huku mwenyeji wa Ikulu akinywa ‘Muratina’ na kula bata.

Labda ni kweli Daktari alijaribu kumfikia RAO, ila sasa akaona mkono wa mapatano waliopokezana RAO na ‘Kamau wa Pili’ umenata sana na kwa muda mrefu? Tafakari.

[email protected]