Kinda anayeunganisha wachoraji wa Afrika kwa mianya ya sanaa ng’ambo
PICHA ina thamani sawa na idadi ya maneno 1, 000, na Yiyi Wang anakiri haya kupitia kipaji chake cha sanaa.
Kinda huyu mwenye umri wa miaka 17, ana mapenzi ya mazingira na yaliyomo kupitia uchoraji.
Kipenzi cha mimea na wanyama, Yiyi msichana mwenye asili ya China, huzungumza upendo wake kwa mazingira kupitia sanaa.
“Sanaa haielezei hadithi pekee, ila pia inaonyesha na kutoa hisia, na jumbe,” anasema msanii huyu anayetoka Beijing, China.
Kwake picha na michoro, inaelezea lugha ambayo maneno yasingeweza.
Akiwa mwanafunzi wa Shule ya Upili China, Yiyi huvutiwa na mazingira kiasi cha kutoa hamasisho kuhusu wanyamapori na mimea kwa kutumia michoro.
Kwa sasa, ni mwanafunzi wa madarasa ya juu (senior student), mwaka wa pili Beijing High School’s International Department.
Mapenzi yake katika sanaa, yalianza akiwa mchanga kiumri, babake Tan Wang, akifichua kwamba alikuwa akichora kwenye jukwaa lolote alilokutana nalo.
“Akiwa na miaka mitano, alionyesha ari ya sanaa na kwa siku angelala saa tano pekee kwa sababu ya kufanya uchoraji,” Wang akaambia Akilimali kwenye mahojiano ya kipekee Jijini Nairobi.
Wang na bintiye, walikuwa wamezuru Kenya majuzi ambapo walipata fursa ya kutembelea Mbuga ya Kitaifa ya Wanyamapori Nairobi.
Yiyi alivutiwa zaidi na twiga na nguruwe wa mwituni (warthog), viumbe anaohoji hajawahi kuwaona ana kwa ana.
Anaridhishwa na mila itikadi za Kiafrika, mapenzi anayosema yalichochewa na hadithi kuhusu Bara Afrika alizosimuliwa na babake aliporejea China, akiwa mchanga.
Wang alikuwa akifanya kazi Afrika.
“Kila aliporejea nyumbani, alikuwa akija na michoro kutoka kwa wasanii wa Kiafrika, ambayo ilifanya nivutiwe na mila za Afrika,” Yiyi akasema.
Mwongo mmoja baadaye, sasa amegeuza aliyoshuhudia babake na kuwasimulia kuwa sanaa yake mwenyewe.
Kinachomfurahisha zaidi, Yiyi anasema ni uwezo wake kuwasilisha lugha na hisia za wanyama kupitia michoro.
Aidha, anakumbuka utangamano na mbwa kipenzi chake anayesema hakuelewa alichotaka alipobweka.
“Huenda alitaka maji, huenda chakula.”
Yiyi anasema muhimu ni utangamano kati ya binadamu na wanyama, wawe wa nyumbani au pori.
“Husikitika sana kuona makao ya wanyamapori yakivamiwa kupitia uharibifu wa mazingira, hasa misitu,” anasema.
Huku akiendelea kunoa makali katika sanaa shuleni, ana imani atayapalilia zaidi katika chuo kikuu.
Kwenye safari ya uchoraji, kinachomridhisha zaidi ni kuunganisha wasanii wa Afrika na masoko ya China.
Julai 2024, licha ya umri wake mdogo, aliandaa hafla ya wasanii kutoka Afrika kuuza michoro yao China.
Ikiwa na kaulimbiu ‘Sillage African Folk Artists Charity Art Sale’, ilivutia wasanii 13 na kuegemea michoro yenye mada; itikadi na mila za Kiafrika.
“Ilishirikisha kina mama waliovalia mavazi ya Kiafrika, nyimbo na ala za muziki, ikiwa ni pamoja na wanyamapori tajika Barani Afrika,” Yiyi anafafanua.
Hata ingawa haikuwa rahisi kuandaa maonyesho hayo, anasema alisaidiwa na babake, marafiki na hata walimu wake.
Alitumia mitandao ya kijamii kama vile Instagram, Youtube, Facebook na Tiktok, kusaka wachoraji.
Hafla hiyo, Yiyi alikusanya zaidi ya Yuan 30, 000 sawa na kima cha Sh543, 000 thamani ya Kenya, hela alizotumia kupiga jeki wachoraji kutoka Afrika kwa kuwanunulia vifaa vya kuchora na hata kulipia wengine karo kunoa bongo katika sanaa.
Ana imani ataendelea kutumia weledi wake kuinua wasanii wa Kiafrika.
Akiwa raibu wa kahawa ya Kenya, kufikia sasa amezuru nchi za Kenya na Misri, Barani Afrika.