KIPWANI: Azma kuu ni kufanya kolabo na Akothee
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
NI mmojawapo wa wasanii chipukizi Pwani wanaokuja kwa kasi ya ajabu.
Kutana na Ian Ngesa al-maarufu Mnigianrass Forty-Five rapa anayesema ana hamu kubwa ya kufanya kolabo na Akothee Madam Boss ila juhudi zake za kumfikia zimekuwa zikigonga ukuta.
“Nimejaribu juu chini kuwasiliana na Akothee kwa njia kadhaa ikiwemo kwa Instagram, Facebook na Twitter lakini hadi sasa bado sijafanikiwa,” asema.
Lengo lako hasa la kujaribu kumfikia msanii Akothee ni lipi?
Mnigianrass: Nataka tu akubali ombi kushirikiana nami kimuziki kwani najua atanisaidia kupaa kwa kasi na kuwa msanii mtajika sio hapa nchini pekee bali kote barani Afrika.
Mbali na juhudi za kuwasiliana naye mtandaoni, umejaribu mbinu nyingine kumvutia?
Mnigianrass: Naam! Nilitunga na kuimba kibao Akothee Madam Boss nikiangazia sifa zake nikiwa na imani kuwa akikisika atajua namhitaji katika safari yangu kimuziki. Lakini wapi! Natumai akisoma makala haya atanifuata tufanye kolabo naye.
Lipi lilokufanya ujiingize katika fani hii ya muziki?
Mnigianrass: Tangu utotoni nilipenda muziki kiasi kwamba nilikuwa nikitengeneza ngoma nikitumia sufuria na vijiti na baadaye niliunda gita la mabati na kuanza kuimba nyimbo za wasanii niliyowaenzi. Lakini nilianza kutunga nyimbo zangu nilipoingia shule ya upili.
Uliiachia kibao au vibao ukiwa shuleni?
Mnigianrass: Nilitoa wimbo wangu wa kwanza Tumekataa mwaka 2016 nilipokuwa kidato cha tatu nikiwalaumu wanasiasa kwa kutudanganya kila wakati wa kampeni na wakishachaguliwa hawatekelezi ahadi walizotoa. Nina nia ya kufanya video ya nyimbo hiyo ili kuwatahadharisha wananchi wasidanganyike na ahadi za uwongo za wanasiasa.
Umeachia kazi zingine tangu wakati huo?
Mnigianrass: Ndio! Tayari nina ngoma tano zaidi ambazo ni Madem, Mziki Iwe Riziki, Akothee Madam Boss, Staki Niwe Solo na Kanchunguze kibao ambacho kinazidi kupata umaarufu.
Nini matarajio yako katika tasnia hii?
Mnigianrass: Ninataka kuwa mwimbaji maarufu sawa ama zaidi ya Kaligraph Jones ili nitambulike kimataifa.
Ungetaka hatua zipi zichukuliwe Pwani kuimarisha tasnia hii?
Mnigianrass: Kwa hakika kuna wanamuziki wazuri wengi hapa Pwani lakini tatizo kubwa ni ukosefu wa wadhamini. Kama serikali za kaunti zitawasaidia wanamuziki chipukizi kwa kuwaanzishia studio za kurekodi nyimbo zao na pia vituo vya redio na televisheni, basi muziki wa Pwani utaimarika.
Mashabiki wako wasubiri nini wakati huu?
Mnigianrass: Niko mbioni kutoa albamu mpya yenye nyimbo tano lakini tatu zitakuwa tayari kufikia sikukuu ya Krismasi ihali nyingine mbili nitazikamilisha mwezi Januari mwakani.