Makala

KIPWANI: Msanii Best Boomer

May 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

KWA msanii kuendeleza kipaji chake, anahitajika kuzunguka sehemu ambazo zinaweza kumuongezea soko lake hasa kwenye miji mikubwa.

Kwa msanii Mishi Mohammed almaarufu Best Boomer, alichukua uamuzi kuhama kimuziki kutoka kwao Mariakani hadi jijini Nairobi ambapo alikuwa na uhakika ataweza kupanua soko lake.

“Ninashukuru uamuzi wangu umeanza kutoa matunda kwani tangu nije Nairobi, nimeweza kuzidi kung’ara na nina imani nitaweza kufanikiwa kwa lengo langu la kuwa mwimbaji wa kutajika sio kwetu Pwani pekee bali kote nchini na Afrika Mashariki,” akasema Best Boomer.

Tangu afike Nairobi, amefanikiwa kuimba nyimbo alizowashirikisha waimbaji wengine; nyimbo ambazo zimemuinua na kupendwa na mashabiki wa muziki wakiwemo wa nyumbani kwao Mariakani mwambao wa Pwani.

Wimbo wa kwanza alioutoa akiwa jijini Nairobi ni ‘Wana nini’ aliomshirikisha Msupa S kabla ya kutoa kibao cha ‘Hela’ akimshirikisha kijana Becho.

“Nimerekodi nyimbo hizi ambazo zimeitikiwa vizuri katika studio ya Rico Beats produsa akiwa Rico,” akasema msanii huyo.

Kwa wakti huu anasema anatayarisha kibao atakachoimba peke yake cha ‘Tamu sukari’ ambacho anatarajia kukizindua baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhan na ana imani kubwa kitashabikiwa na wapenda muziki wengi nchini Kenya.

“Nyimbo zangu hizo tatu nimetumia mitindo ya kisasa ya Afro Beat na Hip Hop na nina imani kubwa ‘Tamu sukari’ ni kibao kitakachopendwa hata nje ya mipaka ya Kenya huko Tanzania na Uganda,” akasema mwimbaji huyo ambaye anajitungia mashairi yake mwenyewe.

Anashukuru kwamba tegemeo lake alipoondoka Mariakani la soko kuongezeka limefanikiwa kwani ameongeza mashabiki wengi na kuwa maarufu zaidi.

Best Boomer anasema ana nia kubwa ya kuinua kipaji chake kwa sababu ya kuwa maarufu na kufanikiwa ili awasaidie wanamuziki wenzake wa huko nyumbani Pwani.

“Nitakuwa bnikihamasisha wanamuziki wenzangu wa nyumbani nitakapofanikiwa,” akasema.

Kuimba mbele ya halaiki ya watu kwenye mikutano ya kisiasa kunawasaidia wasanii wengi kupata umaarufu. Naye Best Boomer kupewa fursa kwake kuimba katika mkutano mkubwa wa kampeni za mgombea kiti cha Urais, Uhuru Kenyatta ulimaanisha mengi kwa mwimbaji huyo.

Alipopewa fursa ya kuimba katika mkutano wa kampeni ya mgombea Urais wa mgombea Kenyatta – ambaye alitangazwa mshindi baadaye – uliofanyika mjini Mariakani mwaka 2017, alizidi kupata umaarufu hata kwa wale ambao si mashabiki wa muziki.

“Wimbo niliouimba wa ‘Sadakta’ ulikuwa tayari ni maarufu kwa wapenda muziki na kwa hivyo, walikuwa wakiuitikia nilipouimba. Mikutano hii ya kisiasa inatujenga sana sisi wasanii kupata umaarufu mkubwa,” akasema Mishi.

Wimbo huo wa ‘Sadakta’ ni wake wa tatu kuimba tangu alipoanza kuimba mwaka 2015. Wimbo huo ameuimba kwa mtindo wa Hip Hop na kuurekodi Studio ya Cracksound hapo Mariakani, produsa akiwa Lai.

“Umaarufu wangu uliongezeka kutokana na wimbo wangu huo na ndiyo maana niliamua kuuimba kwenye mkutano wa kisiasa. Ulinipa hadhi ya kipekee ya kujihisi nimekuwa mwimbaji wa kutambulika,” akasema.

Best Boomer anasema yuko safarini kuhakikisha anakuwa miongoni mwa wasanii mashuhuri nchini.

Msanii Best Boomer. Picha/ Abdulrahman Sheriff

“Hakuna fundi wa muziki ni kuamua na kufanya bidii. Nitafaulu kwani namuweka Mungu mbele kwa kila nitakalo,” akasema.

Alianza kwa kutoa kibao cha ‘Ndoto zangu’ mnamo mwaka 2015 kikiwa katika mtindo anaoupenda zaidi wa Hip Hop na kukirikodi katika studio ya Bullets Records iliyoko Jomvu, produsa akiwa Underwater.

Manny Manny Music ya prodyusa Manny, ni studio ambayo alirikodi wimbo wake wa pili wa ‘Mtoto wa kike’. Nyimbo zake hutumika zaidi stesheni za FM na hasa zile za Pilipili, Kaya, Pwani FM na Boss Radio.