• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
KIPWANI: Princess Cathy aamini kufanya shoo mataifa ya kigeni humzolea msanii sifa

KIPWANI: Princess Cathy aamini kufanya shoo mataifa ya kigeni humzolea msanii sifa

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

KUNA umuhimu kwa wanamuziki kufanya ziara ya kutembelea sehemu mbalimbali nje ya nchi wanayoishi ili waweze kupata fursa ya kuimba na kuonyesha ubora wao.

Kwa kufanya hivyo, wanaweza kuinua vipaji vya uimbaji wao.

Hayo ni matamshi ya msanii wa Pwani, Catherine Mbithe almaarufu Princess Cathy ambaye kwa wakati huu yuko kwenye mipango kabambe ya kufanya ziara ya kwenda Uganda na Amerika kwa ajili ya kushiriki kwenye shoo mbalimbali ambazo ana uhakika zitaweza kumfanya apate umaarufu.

“Ninakubaliana na wasanii ambao wana mawazo kuwa ni muhimu kwenda nje ya nchi yako, kuimba huko na kufanya shoo ambazo zitatambulika. Nina imani kubwa nikikamilisha ziara ninazokusudia kuzifanya za Uganda na Amerika, jina langu litapaa kote Afrika Mashariki,” akasema Princess Cathy.

Princess Cathy anasema amechagua nchi hizo mbili kwa sababu ndizo anazowasiliana na marafiki zake. Lakini anaongeza kuwa atakapokamilisha ziara ya nchi hizo, atapanga kutembelea mojawapo ya mataifa ya barani Ulaya.

Princess Cathy anasema ana uhakika huko atakapokwenda, atakutanishwa na waimbaji maarufu wa Injili na hivyo, ana imani atapata vitu muhimu kutoka kwao ambavyo vitainua kipaji cha uimbaji wake.

Msanii huyo amezindua audio ya nyimbo ‘Utanu’ ambayo ameirekodi Nairobi na produsa Sammy Gitonga wa Dede Records anayefanya kazi naye kuizindua rekodi nyingine ya ‘Musinde’ pale tutakapokuwa makini baada ya janga la corona.

Akieleza ni kwa nini anazindua audio na si video za rekodi hizo mbili, mwimbaji huyo alijibu: “Kwa upande wa video, naendelea kufanya kazi ya kuzirikodi nyimbo hizo mbili nikiwa na produsa mashuhuri Muigai Ndungu wa Mchoro Pictures pia wa jijini Nairobi.”

Princess Cathy anasema nyimbo zakeu zote anatumia mitindo ya Kuabudu na Kusifu na akawashukuru mashabikji wake ambao wamekuwa wakipendelea aimbe kwa mitindo hiyo.

Anasema hakuanza kuimba nyimbo za karne mpya kwa sababu alikuwa hana nia ya kuwa mwimbaji lakini aliamua kuingia moja kwa moja kwa nyimbo za sifa ya Bwana kwa sababu ni yeye Mungu ndiye aliyemwekea kipaji cha kuimba nyimbo zake.

“Wasanii wanaonipa moyo wa kuendelea kuinua kipaji changu ni kina Christine Shusho wa Tanzania, Mercy Masika wa hapa nchini Kenya na Mkenya mwingine, Emmy Kosgei aliyeko Nigeria ambako ameolewa,” akasema.

Kwa wakti huu ni jambo gani ambalo ni changamoto katika kuinua uimbaji wako?

Princess Cathy: Kwa wakati huu kiuhakika jambo linaloniumisha kichwa ni jinsi nitakavyoinua kipaji cha uimbaji wangu na hasa kutafuta stesheni za redio na televisheni kuzipiga nyimbo zangu zipate umaarufu.

Una maoni gani juu ya waimbaji wa Pwani?

Princess Cathy: Ninahimiza wasanii wetu wajitokeze kwenye vyombo vya habari, mitandaoni na kwenye shoo ili watambulike. Nashukuru Taifa Leo kutupa fursa ya kujitambulisha na kutokuwa na ubaguzi wowote.

You can share this post!

Magufuli azungumza na Uhuru kumaliza uhasama maeneo ya...

Mama ajifungua katika kambi alikotafuta hifadhi mafuriko...

adminleo