Akili MaliMakala

Kupanda kwa maji Ziwa Baringo kunavyotishia wakulima

Na SAMMY WAWERU October 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KWA zaidi ya miaka 30, Moses Keben, mkazi wa Kaunti ya Baringo, amekuwa akitegemea kilimo kukithi familia yake mahitaji muhimu ya kimsingi.

Hata hivyo, ongezeko la maji Ziwa Baringo sasa linatishia riziki yake.

Baba huyu wa watoto tisa, hukuza mimea inayochukua muda mfupi kukomaa kama vile nyanya na mboga, na pia nafaka ikiwemo mahindi na maharagwe eneo la Kampi ya Samaki, lililo karibu na ziwa.

Kulingana na Keben, anategemea shughuli za kilimo kulisha familia yake.

Moses Keben akionyesha baadhi ya mahindi yaliyooza kufuatia kupanda kwa maji Ziwa Baringo. Picha|Sammy Waweru

Lakini tangu 2021, shamba lake, pamoja na mashamba ya wakazi wengine eneo hilo ‘yamevamiwa’ na maji ya Ziwa Baringo yanayoendelea kuongezeka kila uchao.

“Kisa cha hivi karibuni ni cha Julai (mwaka huu – 2025), na sasa mashamba yetu yote yamejaa maji,” Keben alieleza wakati wa mahojiano na Akilimali.

Awali, ziwa hilo lilikuwa umbali wa karibu kilomita nne kutoka mashamba yao.

Sasa ardhi waliyoitumia kwa miongo kadhaa kulima chakula imefunikwa na maji.

Maji kutoka Ziwa Baringo yamefurika mashamba ya wakulima. Pichani, kipande cha mahindi yanayooza. Picha|Sammy Waweru

Kilio cha Keben si tofauti na cha wakulima wengine wanaotegemea kilimo na ufugaji.

“Nina hofu kwamba hali ikiendelea hivi, familia yangu itateseka,” analalamika Benson Parsalach, mkulima mwingine.

Wakati wa ziara na mahojiano, tulipata mashamba ya Keben na Parsalach yakiwa yamefunikwa na maji.

Mashamba ya nyanya ya wakulima, tulipata minyanya ikiwa imelemewa na maji. Mimea iliyostawi vizuri, sasa imegeuka sehemu ya ziwa.

Benson Parsalach, mkulima wa nyanya akiwa kwenye shamba lake lililofunikwa na maji kutoka Ziwa Baringo. Picha|Sammy Waweru

Tulipozuru shamba la Keben, fensi ya miti na nyaya iliyoundwa kuzuia viboko iliyotukaribisha ilikuwa bado inasimama, lakini hatua chache tu kutoka langoni maji ya ziwa yanaitishia.

Mmoja wa wafanyakazi wake shambani alikuwa akichimba mitaro.

“Tunajaribu tu kuona kama itazuia maji yasiingie kwa nyanya,” Keben alisema.

Hata hivyo, juhudi hizo hazitoshi kupinga mawimbi ya maji.

Sehemu kubwa ya shamba lake imejaa maji, huku minyanya mingi ikiwa katika kipindi cha kuchana maua na mingine kuanza kutunda. Maji ya ziwa yanatishia mazao yake.

Minyanya karibu na Ziwa Baringo inayoonekana kulemewa na maji. Picha|Sammy Waweru

Kwenye shamba la mahindi, baadhi tayari yameharibika kwa kuoza.

Kwa kawaida, Keben anadokeza kwamba huvuna zaidi ya magunia 30 ya kilo 90 kila msimu. Lakini sasa, ni kiasi kidogo tu alichookoa.

Mbali na kutishia uzalishaji wa chakula, maji hayo pia yana hatari nyingine.

“Ziwa Baringo lina mamba, maji haya yanakuja na wanyama hao ambao huhatarisha maisha yetu tunapokuwa shambani,” akasema Parsalach wakati wa mahojiano.

Wataalamu wanasema kuongezeka kwa maji Ziwa Baringo kunachangiwa na mvua nyingi inayohusishwa na mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa ardhi, ukataji miti kiholela maeneo ya juu yanayosababisha mmomonyoko wa udongo unaoishia kupata makao ziwani, pamoja na mikondo ya maji inayotoka chini kuelekea juu kwenye ziwa kuzibwa.

Shamba hili la mahindi sasa haliwezi kuendeshwa shughuli za kilimo kwa sababu ya kufunikwa na maji kutoka Ziwa Baringo. Picha|Sammy Waweru

Athari hizo zimesababisha ziwa kupanuka na kufunika shule hususan zilizoko visiwani, mashamba, nyumba na hata vituo vinavyovutia watalii kama vile hoteli na mikahawa iliyojengwa kwenye kingo na pia visiwani. Maelfu ya wakazi wamehamishwa.

Serikali ya Kaunti ya Baringo kwa kushirikiana na serikali kuu na mashirika ya kutoa misaada kama vile Red Cross, inajitahidi kusaidia walioathirika.

Kulingana na Felix Maiyo, Mkuu wa Red Cross kanda ya South Rift, mmomonyoko wa udongo unachangia Ziwa Baringo kiwango cha maji kupanda kwa sababu unapandisha kina na pia kuziba njia za maji kutoka – hasa msimu wa mvua, na hivyo kusababisha maji ya ziwa kuongezeka.

Mbali na Ziwa Baringo, maziwa mengine kama Naivasha, Nakuru, Bogoria, Elementaita, Bogoria na Turkana pia yameandikisha visa vya kiwango cha maji kupanda.

Maji kutoka Ziwa Baringo yameenea hadi kwa mashamba ya mimea, umbali wa kilomita tano. Wakazi pia wanahofia kushambuliwa na mamba. Picha|Sammy Waweru

Kwa Keben, ambaye pia ni mfugaji, alikuwa akiskia zamani maji Ziwa Baringo yalikuwa yakipanda ila sasa ameshuhudia mwenyewe.

Moja ya nyumba alizojenga shambani mwake ili wafanyakazi walinde mimea dhidi ya viboko tayari imefunikwa na maji.

Alitegemea kilimo kukithi familia yake mahitaji muhimu ya kimsingi, na sasa matumaini yake anasema ameyaelekeza kwa Mungu.

Mkulima Benson Parsalach, ambaye hulima karibu na Ziwa Baringo akikagua mazao yake ya nyanya. Kwa sababu shamba lake kufurikwa na maji, imani yake sasa ni kwa Mungu tu. Picha|Sammy Waweru