KURUNZI YA PWANI: Kampuni inayowafaa wanafunzi werevu kutoka familia masikini
Na KAZUNGU SAMUEL
WAKATI Naima Hilal alipomaliza kidato cha nne na kupata alama ya C+, alijua fika kilichokuwa kikimsubiri.
Kutokana na ugumu wa maisha katika familia yake katika eneo la Wasini, Kwale, hakuwa na matumaini yoyote ya kuendelea na masomo ya chuo kikuu.
“Wazazi wangu hawakuwa na uwezo wowote na nilijua kuwa kuendelea na masomo ya chuo kikuu itakuwa vigumu,” akasema binti huyo mwenye umri wa miaka 23 na ambaye alimaliza masomo yake ya sekondari mwaka wa 2013 katika shule ya upili ya wasichana ya Matuga.
“Viwango vya umaskini katika eneo la Wasini viko juu sana na nilijua kwamba ndoto yangu itakuwa vigumu kutimia,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Naima ni miongoni mwa wanafunzi ambao wanasoma kupitia kwa ufadhili wa kampuni ya kuchimba madini ya Base Titanium yenye makao yake katika kijiji cha Maumba, kaunti hiyo ya Kwale.
“Baada ya kuhangaika bila kujua nitapata wapi karo, mwaka wa 2015, niliona tangazo kwamba kamuni ya Base ilikuwa inatoa ufadhili wa maosmo na mara moja nikajaribu bahati yangu na nikaitwa,” akasema.
Kwa sasa binti huyo ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu na anatarajia kuingia mwaka wake wa nne mwezi Septemba katika chuo kikuu cha Kenyatta jijini Nairobi. Tulikutana pia na Bw Ali Omar, 32, ambaye vile vile ni mkazi wa Bongwe/Gombato. Yeye kwa sasa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo kikuu cha Pwani kilichoko katika kaunti ya Kilifi, kwa usaidizi pia wa kampuni hiyo ya Base Titanium.
“Ningekuwa kwa sasa mimi ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu lakini nililazimika kurejelea masomo kutokana na ukosefu wa karo. Nilibakia nyumbani kwa mwaka mmoja mpaka pale niliposikia kwamba kampuni ya Base ilikuwa ikitoa ufadhili wa masomo na hapo ndipo nikaamua kujaribu bahati na nikaitwa kwa mahojiano. Nilifaulu na sasa ninaendelea vizuri,” akasema Bw Ali.
Ili kujipatia riziki na kusukuma maisha yake, Bw Ali anafundisha katika shule moja ya kijijini katika eneo hilo la Bongwe.
Naye Bakari Njemo,ambaye ni mmoja wa wale walionufaika na mpango huo wa masomo alisema kuwa anataka kutumia fursa hiyo kurudi kwao Kinondo na kuhamasisha wakazi juu ya umuhimu wa elimu pindi tu akimaliza masomo yake.
“Mimi kwa sasa ni mwanafunzi wa mwaka wa nne katika chuo kikuu cha Kenyatta kitivo cha Mombasa nikisomea hesabu na sayansi,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Alisema kuwa pindi tu atakapomaliza masomo yake, atarudi kwao kuendeleza gurudumu la elimu na kukomboa kijiji kutoka kwa minyororo ya kutosoma.
Na msaada huu wa masomo pia umempatia matumaini kijana Ibrahim Amiri kutoka Kinondo pia ambaye kwa sasa anasomea Hisabati na Fizikia katika chuo kikuu cha Kenyatta.
“Mpango huu wa masomo umenisaidia sana kwa sababu sikujua nifanye nini baada ya kumaliza masomo yangu. Familia yangu haijiwezi kamwe,” akasema.
Naye Nrika Rika mwenye umri wa miaka 26, na mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo kikuu cha Pwani, masomo kwake yangelikuwa ghali kama si mpango huo wa basari.
“Nilimaliza masomo yangu katika shule ya upili ya Matuga mwaka wa 2014 na kupata alama ya C+ na baada ya kukaa nje kwa mwaka mmoja, niliona tangazo kwamba kampuni ya Base Titanium ilikuwa ikitoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi. Nilijaribu bahati na kufaulu,” akasema.
“Lengo langu kuu ni kuhakikisha kwamba wasichana wengi wanapata fursa ya kusoma hasa katika kijiji cha kwetu Tsimba/Golini,” akasema.
Meneja wa uhusiano wa jamii wa kampuni hiyo ya Base Bw Pius Kassim alisema kuwa kampuni hiyo kufikia sasa imesaidia jumla ya wanafunzi 1,484 kupata msaada wa masomo.
Aidha alisema kuwa mara nyingi huwa wanalenga wale wanafunzi ambao wamepata kuanzia maksi 300 na kuendelea mbele.
“Wanafunzi wote ambao wanafaulu kupata ufadhili huo wanafundishwa kwa muda wote wa seondari na wale wa vyuo vikuu vile vile wanafadhiliwa hadi wamalize,” akasema.
Vile vile Bw Kassim alisema kuwa kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana kwa karibu na serikali ya kaunti ya Kwale pamoja na washika dau wengine kufanikisha zoezi hilo.
“Kuwekeza katika elimu kwa vijana wa Kwale ni mojawapo ya nguzo thabiti za kampuni hasa tukijua kwamba tunafanya hivi tukiwatayarisha kwa nafasi nzuri siku za usoni,” akasema.
Kila mwaka, kampuni hiyo hutumia Sh30 milioni kugharamia mpango wa masomo kwa wanafunzi werevu kutoka familia maskini na kufikia sasa, jumla ya Sh164 milioni zimetumika tangu mpango huo uanze.
“Hizi ni pesa ambazo kampuni imetumia tangu mwaka wa 2013 hadi sasa wakati mpango huo ulipoanza,” akasema Bw Kassim.