• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 10:55 AM
KURUNZI YA PWANI: Miraa inavyovunja ndoa baada vijana kukosa nguvu chumbani

KURUNZI YA PWANI: Miraa inavyovunja ndoa baada vijana kukosa nguvu chumbani

Na WINNIE ATIENO

Ndoa nyingi zimeathirika katika kaunti ya Mombasa huku vijana waliofikisha umri wa kuoa wakishindwa kufanya hivyo kutokana na uraibu wa kutafuna muguka.

Wawakilishi wa Bunge la kaunti ya Mombasa sasa wameanzisha mikakati ya kupiga marufuku uuzaji na matumizi ya miraa kufuatia athari za kiafya zinazotokana na uraibu wa utafunaji wa mmea huo.

Aidha wawakilishi wa wodi za Mombasa walisema ndoa nyingi zimevunjika huku vijana wengi na watoto wa shuke wakiwa waraibu sugu wa muguka.

Kadhalika, wanawake huko Kilifi waliandamana wakipinga matumizi ya muguka miongoni mwa waume zao na wanafunzi.

Naibu mwenyekiti wa kamati ya afya katika Bunge la Mombasa, Bi Fatma Kushe alisema mmea huo unawafanya wanaume wanazubaa na kushindwa kutekeleza wajibu wao kwenye ndoa.

“Muguka iko na stimu mbaya sana na kumfanya mtu kuwa zoba yaani hata anashindwa kufanya lolote hususan kwa wenye ndoa. Familia zinavunjika na ni jukumu letu kuhakikisha tunalinda maslahi ya umma kama kamati ya bunge ya afya,” akasema Bi Kushe.

Alisema watoto wa shule wa umri wa miaka 12 wameanza kuacha shule wakigubia muguka inayouzwa waziwazi bila taratibu zozote.

“Wafanyibiashara wanaangalia biashara zao badala ya afya ya umma, kwanini wanawauzia watoto ambao baadaye wanaanza kujihusisha na wizi wa mabavu,” akaongeza.

Mei mwaka huu bunge la kaunti ya Kwale lilipiga marufuku uuzaji na utumizi wa muguka huku wawakilishi wa wodi za eneo hilo wakiapa kuwashurutisha wenzao katika eneo la pwani kufuata mkondo huo.

Akiongea na Taifa Leo, Bi Kushe alisema wawakilishi wa wodi za Mombasa wamefanya mikutano kadhaa na wawekezaji wa muguka, wataalam wa afya na tume ya kupambana na dawa za kulevya ili kutafuta suluhu la kudumu.

Mmea huo ukuzwa eneo la Embu lakini soko lake kubwa linapatikana katika jiji la kitalii la Mombasa ambapo linapendwa na wengi, wakubwa kwa wadogo hususan wanaume.

Linauzwa katika soko la pwani linalofahamika kama Kongowea soko lengine linapatikana katika uwanja wa Tononoka.

Zaidi ya magari manne husafirisha zao hilo kutoka Embu hadi katika soko la Kongowea kila siku ambapo wafanyibiashara huenda kununua na kusambaza kwa masoko madogo.

Bi Kushe alisema amefanya kikao na wawekezaji na kuwalelezea kutafuta biashara mbadala kufuatia marufuku hayo yanyonuiwa.

Lakini katibu mkuu wa soko la Kongowea Daniel Matumo aliitaka bunge la kaunti hiyo kutopiga marufuku muguka na badala yake kufanya utafuti wa afya kufuatia madhara yake.

Bw Matumo alisema alitumia muguka kwa muda kabla ya kuacha baada ya kuokoka na hajawai ona madhara yake.

“Tatizo kubwa ni namna mtumiaji anavyotumia ili asiwe mraibu lakini muguka haina madhara ya kupunguza nguvu za kiume kama wanavyodai wawakilishi wa wodi ya Mombasa. Kuna watu wametumia tanguutotoni huko Embu na wanatimiza majukumu yao ya ndoa,” akasema.

Alisema biashara ya uuzaji na ukulima wa muguka inategemewa na familia nyingi sana huko Mombasa na ikipingwa marufuku mamia wataathirika.

Boxi ya muguka huuzwa kwa Sh3000 huko Mombasa.

Aliwatahadharisha wazazi dhidi ya kuwatuma watoto wa shule kuwanunulia muguka sokoni.

“Pia wao wanachangia katika kuwaingiza watoto kwenye uraibu wa muguka. Kuna zaidi ya wauzaji 200 wa muguka,” akasema Bw Matumo.

Lakini mwakilishi wa wodi ya Miritini Kibwana Swaleh alisema vijan ambao wamefika umri wa kuoa wameshindwa kuoa kutokana na uraibu wa muguka.

You can share this post!

Wakalenjin waitaka Mlima Kenya kuheshimu mkataba na kuunga...

Spika aitisha ripoti ya wabunge waliozuru Urusi kutazama...

adminleo