• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
KURUNZI YA PWANI: Uchunguzi kubaini gari lilivyozama Likoni waanza

KURUNZI YA PWANI: Uchunguzi kubaini gari lilivyozama Likoni waanza

Na MOHAMED AHMED

MAAFISA wa upelelezi wanajaribu kutegua kitendawili kuhusiana na ajali ya gari lililotumbukia katika Bahari Hindi lilipotoka kwenye feri Septemba 29, 2019, katika kivuko cha Likoni, likiwa na mwanamke na mwanawe.

Suala kuu ambalo maafisa hao wanataka kubainisha ni iwapo injini ya gari hilo ilikuwa inawaka ama imezimwa wakati gari hilo lilidondoka kwenye feri ya MV Harambee na kuingia majini siku ya mkasa.

Hii ni baada ya uchunguzi wa kwanza uliofanywa mara tu gari hilo lilipotolewa majini Ijumaa iliyopita na kuonekana kuwa gari lilikuwa limezimwa na gia ikionyesha limeegeshwa kwa njia salama.

Aidha, vifaa vya kusafisha kioo cha mbele cha gari wakati wa mvua vilipatikana vikiwa vimewashwa baada ya gari hilo kutolewa baharini.

Maafisa hao sasa wanajiuliza iwapo kweli gari hilo lilikuwa limezimwa kabla ya kutumbukia baharini, ama lilizimwa wakati lilikuwa linaelea juu ya maji kabla ya kuzama.

“Tunajaribu kuangalia iwapo marehemu alilizima gari baada ya kushtuka ama alifanya hilo muda tu baada ya kuingia kwenye feri. Hii ni kutokana na kuwa, uchunguzi wa kwanza unaonyesha gari lilikuwa limezimwa kama inavyostahili,” akasema afisa moja kutoka kitengo cha jinai anayehusika na uchunguzi huo.

Vilevile, ilibainika kuwa mlango wa gari hilo haukuweza kufunguka kwa sababu gari hilo lilikuwa limezimwa.

Maafisa walilazimika kuvunja upande mmoja wa gari hilo siku ambayo lilitolewa majini ili kutoa miili ya Bi Mariam Kighenda na mwanawe Amanda Mutheu.

Iwapo itabainika kuwa gari hilo lilikuwa limezimwa, basi kuna uwezekano mkubwa kwamba lawama zote zitaendea shirika la huduma za feri kwani mlango wa feri hiyo ya MV Harambee ulionekana kuwa mbovu.

Kuchukua taarifa

Tayari, maafisa hao wameanza kuchukua taarifa kutoka kwa maafisa wa KFS wanaohusishwa na ajali hiyo.

Miongoni mwao ni nahodha wa feri hiyo, maafisa wa kuelekeza magari na walinzi katika kivuko hicho.

Mkuu wa DCI Mombasa, Bw Anthony Muriithi, alithibitisha mipango hiyo ya kuandikisha taarifa kutoka kwa wahusika.

Gari hilo liliondolewa baharini Ijumaa baada ya juhudi zilizoendelezwa kwa siku 13 tangu lilipozama mnamo Oktoba 6 na kikosi kilichojumuisha makundi mbalimbali ya kiserikali na kibinafsi, yakiwemo ya kigeni.

Rais Uhuru Kenyatta alituma risala za rambirambi kwa familia ya Bw John Wambua ambaye alimpoteza mkewe na bintiye katika mkasa huo.

Taarifa kutoka Ikulu ilisema Rais amehuzunishwa na tukio hilo na anawahakikishia Wakenya wote kwamba hatua zinachukuliwa kuhakikisha kisa kama hicho hakitatokea tena katika siku za usoni.

Mbali na ukarabati wa huduma za feri unaoendelea, Rais alisema ujenzi uliopendekezwa wa Daraja la Likoni, ujenzi unaoendelea wa barabara ya Dongo Kundu na pia kukamilishwa kwa barabara ya Samburu-Kinango-Kwale, kutasaidia kupunguza msongamano katika kivukio hicho cha baharini kati ya Kisiwa cha Mombasa na Kusini mwa Pwani.

“Rais ambaye amekuwa akifuatilia kwa makini shughuli za kutafuta na kutoa gari na miili hiyo katika muda wa siku 13 zilizopita, anapongeza kundi la wataalam waliohusika kwa bidii yao kuhakikisha kufaulu kwa shughuli hiyo ambayo imechukua muda mrefu, ya kuchosha na ya hatari,” taarifa hiyo ikasema.

Pia aliahidi familia ya Bw Wambua kwamba serikali itaendelea kuwasaidia.

You can share this post!

Oparanya ashutumu wanaopinga juhudi za kufufua Mumias Sugar

VIKEMBE: Martinelli kivuli chipukizi cha Ronaldo

adminleo