KURUNZI YA PWANI: Wakazi Mombasa wahofia kuishi na polisi mitaani
NA MOHAMED AHMED
MATUKIO ya mauaji ya vijana kiholela mikononi mwa polisi maeneo ya Mombasa, yamefanya viongozi wa kisiasa, mashirika ya kutetea haki za kibinadamu na wakazi kuhofia mpango mpya wa serikali utakaopelekea polisi kuishi mitaani.
Katika mageuzi hayo ambayo yanatarajiwa kuanza rasmi baada ya miezi mitatu, maafisa wa usalama wanatajariwa kutangamana na raia wa kawaida mitaani katika hatua ambayo Rais Uhuru Kenyatta alisema itafanikisha ushirikiano mwema kati ya polisi na jamii.
Mbali na mauaji ya vijana, wakazi pia wanahofia kuwa huenda magenge yakapata njia rahisi ya kulipiza kisasi kwa polisi watakaokuwa mitaani na hivyo basi kusababisha makabiliano ya mara kwa mara kati yao na polisi, na kuweka raia wasiokuwa na hatia hatarini.
Wakazi wa Kisauni, miongoni mwa maeneo ambayo yamekumbwa na visa vya ukosefu wa usalama walisema kuwa kutangamanisha polisi na jamii kutaongeza visa vya mauaji.
“Ni eneo hili ambapo miezi michache tu polisi aliuliwa na vijana wa magenge ya uhalifu. Ukileta polisi karibu na wakazi ni kama kujenga ugomvi,” akasema Bw Said Mbarak.
Seneta wa Mombasa Mohammed Faki, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir na maafisa wa mashirika ya kijamii ya Haki Africa na Muhuri walitaka serikali kutekeleza mageuzi hayo kwa uangalifu mkubwa wakisema kutangamana kwa maafisa wa usalama na raia kwa ukaribu huenda kukaleta shida za kiusalama. Bw Faki alisema kuwa ni lazima mpango huo utekelezwe pole pole na si kwa mpigo ili kuruhusu raia kuzoea hali hiyo mpya.
“Tukiamka tu tuseme kuwa maafisa wa usalama waanze kuishi na raia wa kawaida mitaani ni lazima tujue ni mambo yapi tutafanya ili tusilete madhara yoyote hususan ya kiusalama,” akasema Bw Faki.
Bw Nassir kwa upande wake alisema kuwa hali ya utovu wa usalama ilichangiwa na vifo vinavyosababishwa na polisi na magenge ya wahalifu, na hivyo kutangamana huko na raia kutaongeza shida zaidi.
“Iwapo polisi watabeba silaha hizo hadi majumbani mwao basi kunaweza kukatokea mauaji zaidi ya kiholela,” akasema Bw Nassir.
Mkurugenzi mkuu wa Haki Africa, Hussein Khalid alisisitiza kuwa kuna haja ya mageuzi hayo kufanywa pole pole la sivyo usalama utazidi kudorora hususan Mombasa.
Alisema kuwa tayari visa vya polisi kuua vijana vimekithiri na utangamano huo huenda utachangia mauji zaidi.
“Tayari tuna kesi nyingi za mauaji, mageuzi haya ni sawa ila yafanywe taratibu,” akasema Bw Khalid.
Mkurugenzi wa shirika la Muhuri kwa upande wake alisema kuwa mageuzi hayo yasiwe ya sare za polisi pekee bali na mienendo yao ya kikazi.
Hata hivyo, Bi Shamsa Hemed ambaye ni mkazi wa Mwandoni alikuwa na maoni tofauti. Asema utangamano wa polisi na raia utaleta usalama karibu na jamii.
Alisema kuwa iwapo polisi hao watakuwa karibu na wakazi basi visa vya vijana kuvamia watu kwa visu na mapanga vitapungua.
“Kutakuwa na hofu miongoni mwa wahalifu na hiyo itaruhusu tupate usalama wa kutosha cha muhimu ni kuhakikisha kuwa maafisa hao pia wanapata usalama wao wa kutosha,” akasema Bi Hemed.