KUZIMA UFISADI: Wito elimu ya Blockchain ienezwe kote nchini
NA FAUSTINE NGILA
NI SIKU ya Ijumaa ambapo Taifa Leo imehudhuria Warsha ya Teknolojia katika Chuo Kikuu cha Strathmore. Kumejaa wanafunzi, wataalamu na wadau katika vyumba tofauti chuoni humu, wengi wakiwa wamefika kukata kiu ya teknolojia za kisasa na hatimaye kupata ajira.
Yamkini kampuni zote za teknolojia humu nchini zimefika hapa, huku wawakilishi wake wakitengewa muda kuwasilisha mada mbalimbali kuhusu matumizi na umuhimu wa teknolojia katika makuzi ya uchumi wa nchi. Ni mara ya nne kwa warsha hii kuandaliwa tangu iasisiwe hapo 2016.
Baadhi ya mashirika haya ni Moringa School, Muungano wa Teknolojia ya Blockchain, Microsoft, Google, Facebook, Jumo, Andela, Tala, iHub, Liquid Telekom, Twiga, Nailab, Little, Belva Digital, Pangea na Shelter Tech. Zote hizi zimefika kutangamana katika warsha kubwa zaidi Afrika kusini mwa Sahara inayoandaliwa kila mwaka jijini Nairobi.
Wasilisho linalotuvutia zaidi ni teknolojia ya Blockchain ambayo serikali imekuwa ikiwazia kuanza kuitumia katika miaka ya usoni.
Katika maelezo kuhusu uvumbuzi huo, watalaamu walionya kuwa utumizi wake bila kutoa mafunzo kwa wananchi huenda ukalemaza ufanisi wake.
Walitoa wito kwa serikali kushirikiana na sekta ya kibinafsi kuelimisha umma kote nchini kuhusu matumizi ya Blockchain katika ukuzaji wa uwazi na uwajibikaji serikalini na kampuni za kibinafsi.
Benjamin Arunda, mwandishi wa kitabu cha kwanza nchini Kenya kuhusu teknolojia hiyo, Understanding The Blockchain na aliye pia mkuu wa mafunzo katika Muungano wa Wataalamu wa Blockchain nchini (BAK), alielezea haja ya kuandaa mafunzo na warsha kuhusu teknolojia hiyo akisema ndio ufunguo wa kukubalika na kutumika kwake.
Naye mtaalamu wa Blockchain katika kampuni ya Kesho Labs, Bi Roselyne Wanjiru aliirai serikali kuanzisha mafunzo hadi kwenye kaunti kuelezea wananchi kuhusu manufaa ya teknolojia hiyo.
“Hakutakuwa na ufanisi wowote ikiwa matumizi ya Blockchain yataanza bila kutoa maana yake kwa wananchi na watumizi. Wakenya wanafaa kuelezwa kuhusu uwezo wa teknolojia hii kuzima ufisadi,”; akasema.
Afisa mkuu mtendaji katika kampuni ya Aeternity Hub Africa Bw Frank Deya alisema kuwa ingawa serikali iko tayari kutumia teknolojia hiyo kukomesha wizi na ulaghai katika sekta za fedha, afya na umiliki wa ardhi, watumizi wake wanafaa kuelezwa kwa kina kuhusu uwezo wake.
“Tunahijati kutatua ukosefu wa ujuzi wa Blockchain mwanzo kabla ya kuanza kuitumia. Tunapaswa kujenga imani kuhusu teknolojia hii kwa Wakenya. Kila mtu anaweza kufunzwa kwa umri wowote, wakati wowote,” alisema.
Haya yanajiri huku Jopokazi kuhusu Blockchain na Teknolojia ya Kiotomatiki likisubiri kuwasilisha ripoti yake ya utafiti kwa waziri wa Teknohama Joe Mucheru ambapo itakabidhiwa Rais kutathmini uwezo wa taifa hili kutumia Blockchain katika asasi kuu za serikali.
Teknolojia hii iliripotiwa kuwa dhabiti wakati taifa la Sierra Leone iliitumia kwa majaribio kuhesabu kura wakati wa uchaguzi wa urais 2018. Hata hivyo, taarifa hiyo ilipokelewa kwa tahadhari kuu nchini humo.
Blockchain ndio teknolojia ya kipekee inayowezesha usimamizi wa data kubwa kidijitali bila kubatilishwa na wanadamu. Hata hivyo, kukuza imani kuihusu kunafaa kuanza na elimu kwa umma kuhusu jinsi inaweza kutumiwa kunasa wafisadi wa fedha za serikali na kampuni.
“Teknolojia hii inawafungia nje wadukuzi kupata data ya siri kufanikisha wizi wa pesa au taarifa. Kwa mdukuzi kufanikiwa, anahitajika kudukua kila kila kijisehemu cha nyororo ya mfumo huo, na kuna mabilioni ya vijisehemu hivi,” akasema Bw Deya.
Huu ni mwako mpya katika juhudi za kuwatambua wezi wa fedha za serikali za kaunti kwa kuwa inawezesha kunaswa kwa mwizi moja kwa moja.
“Tatizo tunaloshuhudia kaunti zinapopoteza mamilioni kwa wanasiasa ni kuwa pesa hizo hutoka eneo moja, kwa Hazina Kuu. Blockchain inawezesha fedha kutumwa kwa kila eneo, huku kila serikali ya kaunti ikifuatiliwa kwa ukaribu kuhusu jinsi inatumia fedha ilizotumiwa. Usahihi wa teknolojia hii utaipa Hazina Kuu habari kuhusu kiasi cha pesa zilizotumika kabla ya kutuma zingine,” akasema Bi Wanjiru.
Wataalamu hao walisema kuna matumaini kuhusu mustakabali wa taaluma ya uanasheria na usimamizi wa ushuru.
“Tukipigwa jeki na serikali, ushahidi kutokana na Blockchain utatumika mahakamani kuwahukumu wafisadi. Hili litawaletea haki walalamishi,” akasema Bw Arunda.
Mtaalamu huyo aliirai serikali pamoja na sekta ya kibinafsi kuwekeza kwa ujuzi wa kompyuta hasa mbinu za msimbo (coding) kuanzia miaka saba maanake teknolojia inakua kwa kasi mno.
Warsha hiyo ya teknolojia imepata umaarufu katika miaka ya hivi karibuni tangu lianze hapo 2016 ambapo watu 700 walishiriki. Mwaka huu ilivutia watu zaidi ya 1,500 kulingana na meneja mkuu wa Nairobi Tech Week Bi Anne Salim.
Adrian Muthomi, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa mwisho wa Teknolojia ya Habari kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jomo Kenyatta aliambia Taifa Leo kuwa warsha hiyo imemletea manufaa sana kiasi kwamba imemlazimu kubadilisha mwonekano wa kifa uroro (software) anayounda kuuzia maduka ya jumla.
“Ina taarifa nyingi mpya kuhusu teknolojia. Siwezi kukosa kuhudhuria tena kwani nitakosa mambo muhimu kuhusu uvumbuzi wa kompyuta,” akasema Tabitha Kavyu, mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Nairobi anayesomea Sayansi ya Kompyuta.
Pauline Onyango, ambaye ni mtaalamu wa ukusanyaji ushuru aliduwazwa na jinsi teknolojia za kidijitali zimeweza kubalisha ofisi za kisasa na jinsi teknolojia inaweza kutumiwa kuzima wakwepaji wa ushuru.