Lugha, Fasihi na Elimu

Lugha za kimaeneo zinakubalika, hivyo ni sawa kuwa na Kiswahili cha Kenya na kile cha Tanzania

Na NA PROF IRIBE June 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WIKENDI iliyopita nilikuwa nyumbani Salama katika Kaunti ya Laikipia. Nilipatana na binamu wangu na kukawa na mazungumzo kuhusu Kiswahili. Baada ya mazungumzo ya muda, binamu wangu walihitimisha kuwa Kiswahili cha Tanzania ni “kizuri” kuliko cha Kenya.

Nilisaili kujua sababu ya uamuzi huo na nikafahamishwa kuwa “wana maneno mengi tofauti na ya Kenya na yao hukubalika zaidi kwa namna wanavyoongea.”

Sikuelewa lakini sikutaka kuharibu dhifa na mjadala mzuri kwa kuingiza mkabala wa kiusomi na kitaaluma.

Jambo lililokuwa sahihi katika mjadala huo ni kwamba baadhi ya maneno yatumikayo Kenya na Tanzania kutajia kitu kilekile huwa tofauti.

Kwa mfano, nchini Kenya kuna uwezekano wa kumsikia mtu akitamka maneno kama ‘mshipi’, ‘matatu’, ‘tuktuk’ na ‘pesa’ ilhali maneno hayo yatakuwa ‘mkanda’, ‘daladala’, ‘bajaji’ na ‘hela’ mtawalia nchini Tanzania.

Kwa hakika, matumizi ya lugha kimaeneo ni jambo la kawaida. Matumizi ya aina hii ndiyo yanayochangia kuwa na Kiingereza cha Uingereza na kile cha Marekani. Hata hivyo, itakuwa makosa kusema kuwa kimoja ni bora kuliko kingine.

Ilivyo ni kwamba matumizi hayo tofauti hukubalika katika matumizi ya muktadha wake. Ilivyo ni kwamba huwa kuna yale matumizi rasmi na ndio sababu tuna Kiswahili Sanifu ambacho hukubalika kote ulimwenguni mnapotumiwa Kiswahili.

Kwamba Watanzania watatumia “mkanda” ilhali Wakenya watatumia “mshipi” haimaanishi kuwa kuna matumizi “mazuri” au “mabaya,” hizi ni tofauti za kimaeneo tu!

Ukweli ni kwamba tofauti hizi huweza kujitokeza hata katika nchi moja. Tanzania visiwani (hasa Unguja) watatumia “kamusi la …” ilhali bara watatumia “Kamusi ya …” Matumizi yote haya yanakubalika.