Makala

Magavana wanawake wanavyokumbwa na changamoto tele

Na JUSTUS OCHIENG, KAMAU MAICHUHIE March 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MAGAVANA wa kike nchini Kenya wanakabiliwa na changamoto kubwa za kisiasa na kiutawala, huku kukiwa na ongezeko la mashambulizi ya kimakusudi, vitisho vya kuondolewa madarakani, na hila za kisiasa.

Licha ya kuweka historia katika uongozi baada ya uchaguzi wa Agosti 2022, ambao  angalau saba wao walichaguliwa, wengi wao wanakumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa mifumo ya kisiasa inayoongozwa na wanaume.

Mashtaka ya usimamizi mbaya, kutokuwepo kazini, na kampeni za kuchafuliwa majina zimekuwa za kawaida, jambo linaloashiria mapambano makubwa ya wanawake katika nafasi za juu za uongozi.

Baadhi ya magavana wanawake wameripoti visa vya kutatizwa na wanasiasa wenye nguvu, wakiwemo wabunge wa maeneo yao, maseneta, na hata maafisa wa serikali kuu, ambao wanataka kudhibiti masuala ya kaunti.

Gavana wa Meru aliyeng’olewa mamlakani, Kawira Mwangaza, kwa mfano, alivunja kimya chake hivi majuzi na kuishutumu serikali kwa kupanga kuondolewa kwake madarakani.

Bi Mwangaza alidai kuwa wapinzani wake, hasa viongozi wa kiume, walikuwa na uchungu kwa sababu ya kushindwa kwao katika uchaguzi wa 2022, ambapo aliwashinda wanasiasa wenye majina makubwa kama aliyekuwa  Waziri wa Kilimo Mithika Linturi na Kiraitu Murungi.

“Kuondolewa kwangu hakukuakisi matakwa ya wananchi bali ilikuwa mpango wa wapinzani wa kisiasa na Serikali Kuu waliotaka kuniadhibu kwa kukataa kutumiwa kisiasa,” alidai Bi Mwangaza.

Gavana wa Nakuru Susan Kihika. Picha|Maktaba

Hali hii inajitokeza pia kwa Gavana wa Nakuru, Susan Kihika, ambaye anakumbwa na ukosoaji na vitisho vya kuondolewa madarakani kwa madai ya kutoonekana kazini licha ya kuwa kwenye likizo ya uzazi.

Kundi la viongozi wa kike lilijitokeza mapema wiki hii kumtetea Kihika huku kukiwa na malalamishi kutoka kwa wananchi kuhusu kutokuwepo kwake katika masuala ya kaunti.

Licha ya Kihika kufafanua kuwa alikuwa kwenye likizo ya uzazi na atarejea kazini hivi karibuni, wakazi wa kaunti walifikisha ombi kwa Bunge la Kaunti wakitaka uwajibikaji kutoka kwake.

Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga. Picha|Hisani

Katika mkutano na waandishi wa habari Jumanne, Maseneta Walioteuliwa Tabitha Mutinda, Hamida Kibwana, na Veronica Maina; Wawakilishi wa Wanawake Cynthia Muge na Betty Maina, pamoja na aliyekuwa Seneta Millicent Omanga, waliwataka wananchi kuwa na subira na kuelewa kuwa wanawake wanapitia changamoto kubwa za kusawazisha kazi na familia.

Gavana wa Homa Bay, Gladys Wanga, naye amekuwa akikumbwa na mashambulizi, hasa kutoka kwa wapinzani wake mitandaoni.

Bi Wanga, ambaye ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha ODM cha Raila Odinga, amesema kuwa anaendelea na majukumu yake na hatayumbishwa na wapinzani wake.

“Tuache propaganda. Kwa bahati nzuri, mimi najua kupambana, ninajua ninachofanya, na sitatetereka,” alijibu Bi Wanga baada ya mashambulizi ya mitandaoni dhidi yake.

 

Anne Waiguru ambaye mara kwa mara ameongoza magavana wenzake kulilia serikali kuu iachilie pesa. Picha|Maktaba

Ijumaa, Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru na mwenzake wa Kwale Fatuma Achani walisema kuwa changamoto wanazokumbana nazo zinawafanya kuwa viongozi imara zaidi.

“Vitendo hivi ni kielelezo cha changamoto zinazowakumba wanawake katika uongozi mara kwa mara. Jamii yetu inaweka viwango vya juu visivyo vya haki kwa viongozi wanawake,” alisema Bi Waiguru.

Gavana wa Kwale, Fatuma Achani, alisema kuwa wanawake wanaoingia kwenye siasa huwa wanajitayarisha kwa vita na watabaki imara katika kuhudumia wananchi.

“Unapokuwa mwanamke mwanasiasa, unatarajia kupingwa, hasa kutokana na mawazo ya kikale ya mfumo dume. Hii haiwezi kutuvunja bali inatufanya kuwa na nguvu zaidi,” alisema Bi Achani.

Gavana wa Machakos, Bi Wavinya Ndeti. PICHA|HISANI

Kama ilivyo kwa Bi  Mwangaza, Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti naye anakumbwa na vitisho vya kuondolewa madarakani, baada ya MCA wa Muthwani, Dominic Maitha, kutangaza kuwa atawasilisha hoja ya kumng’atua.

Akizungumza na Taifa Leo Bi Ndeti alikiri kuwa magavana wanawake wako kwenye shinikizo kubwa kutoka kwa viongozi wa kiume.

“Ndio, uongozi wa wanawake unakabiliwa na changamoto kubwa kutoka kwa wanaume wanaotaka kututawala. Nafasi za wanawake zinapaswa kulindwa vilivyo,” alisema Bi Ndeti.

Crispin Afifu, mtaalamu wa masuala ya jinsia katika Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Wanawake (ICRW), alieleza kuwa hali ya magavana wanawake kukabiliwa na vitisho vya kuondolewa madarakani si jambo la bahati mbaya.

Alisema kuwa kisa cha Bi Mwangaza na vitisho dhidi ya Wavinya Ndeti na Susan Kihika zinaonyesha mazingira ya kisiasa yanayopinga uongozi wa wanawake.

 

Gavana wa Kwale Fatuma Achani. PICHA | KNA

“Hali hii inaashiria kutoridhika kwa jamii na mabadiliko ya kijinsia katika uongozi. Wakati viongozi wa kiume wanapotenda mambo kama haya, wanaonekana kama jasiri, lakini wanawake wanapofanya hivyo huonekana kama wakaidi,” alisema Bw Afifu.

Aliongeza kuwa ingawa uwajibikaji ni muhimu, uchunguzi wa kupita kiasi dhidi ya magavana wanawake unaonyesha upendeleo wa kijinsia.