Makala

Magavana wasema wamelazimishiwa vifaa vya matibabu vinavyomeza mabilioni ya SHIF

Na COLLINS OMULO December 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SAKATA nyingine inaelekea kutokota katika sekta ya afya nchini kuhusiana na mpango wa ukodishaji wa vifaa vya kisasa vya matibabu kwa matumizi katika hospitali zinazosimamiwa na serikali za kaunti.

Hii ni baada ya magavana kufichua kuwa walilazimishwa kutia saini mkataba, na Wizara ya Afya, kuhusu ukodishaji wa vifaa hivyo bila ufahamu wa kina kuhusu mpango huo.

Maseneta wameelezea mpango huo kama “usioendeshwa kwa uwazi” na huenda ukafanana na mpango mwingine sawa na huo uliofyonza Sh63 bilioni, pesa za umma.

Naibu mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Mutahi Kahiga mnamo Jumanne aliambia maseneta kwamba magavana hawana ufahamu mpana kuhusu mpango huo kwa jina National Equipment Service Project (NESP) unaoendeshwa na Serikali Kuu.

Akiongea Jumanne alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu (CPAC) Bw Kahiga, ambaye ni Gavana wa Nyeri, alisema kuwa magavana hawakuhusishwa katika utoaji zabuni kwa kampuni itakayowasilisha vifaa hivyo, japo walilazimishwa kuutia saini mkataba.

“Ni Wizara ya Afya iliyoweka tangazo katika vyombo vya habari na hata kuagiza vifaa hivyo. Wajibu wa serikali za kaunti ulisalia kuhifadhi vifaa hivyo kwa matumizi,” Bw Kahiga.

Hata hivyo, alisema majadiliano yalifanywa kati ya kikosi cha CoG na kile cha Wizara ya Afya.

Akimwaga mtama zaidi kuhusu mpango huo, Gavana Kahiga aliungama mbele ya kamati hiyo, inayoongozwa na Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang’, kwamba hawakuwa na lingine ila kutia saini mkataba huo wa ukodishaji vifaa hivyo vya kimatibabu.

Kufikia sasa, akaeleza, magavana 34 wametia saini mkataba huo.

“Ninasema haya kama naibu mwenyekiti wa Baraza la Magavana. Kwa kuzingatia hali ilivyo na mahala tulipo, sitasema kuwa mpango huu ndio bora zaidi. Hata sina hakika ikiwa vifaa hivyo vitafanya kazi. Lakini hatukuwa na jingine ila kukubali kuutia saini mkataba huo,” akasema.

Naibu huyo wa mwenyekiti wa CoG alisema ni Wizara ya Afya iliyoteua kampuni za kuwasilisha vifaa hivyo na kazi ya serikali za kaunti ilikuwa kuruhusu vifaa hivyo kuwekwa katika hospitali zao.

“Tulijipata katika hali ambapo tunafahamu kuwa chakula ni kibaya kinachoweza kukudhuru lakini unasema ni heri uendelee kula chakula hicho,” akasema Gavana Kahiga.

“Kwa maneno mengine unajipata na kundi la watu wanaohisi njaa lakini unawaambia kuwa japo chakula hiki kinaweza kuwadhuru, ni heri mwendelee kukila,” akaeleza.

Ajabu ni kwamba kamati hiyo ya CPAC iliambiwa kuwa wanasheria wakuu katika kaunti waliwashauri magavana kutotia saini mpango huo kwa sababu walitilia shaka uhalali wake na kwamba haukuendeshwa “kwa njia ya uwazi”.

Mwanasheria Mkuu wa Kaunti ya Nyeri Kimani Rucuiya, ambaye ni mwenyekiti wa Muungano wa Wanasheria Wakuu wa Kaunti, aliwaambia maseneta kuwa walichelea kuhusu mpango huo kwani unaenda kinyume na Katiba na sheria za uagizaji bidhaa na huduma.

Aidha, alisema kuwa Makubaliano Kati ya Ngazi Mbili za Serikali (IPA) yanayotiwa saini baada ya shughuli ya uagizaji kufanywa yanaibua maswali mengi kuliko majibu.

“Serikali ya Kitaifa ilikiuka wajibu wake wa kikatiba kwa kuagiza vifaa vya kimatibabu ilhali wajibu huo umegatuliwa. Mkataba wa IPA ungetiwa saini kabla ya uagizaji vifaa hivyo kufanywa.

“Hata hivyo, haiaminiki kuwa mpango huo utasaidia serikali za kaunti kupunguza gharama ya ununuzi wa vifaa hivyo,” akasema Rucuiya.