Makala

Polisi wataka kujua jinsi mwanamke mfanyabiashara ya mapenzi Eldoret alifia chumbani

Na TITUS OMINDE December 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

POLISI mjini Eldoret wanamsaka mwanamume anayeshukiwa kumuua mwanamke katika danguro moja eneo la Tairi mbili kando ya barabara kuu ya Eldoret-Webuye.

Mwili wa mwanamke huyo ulipatikana katika chumba ambacho alikuwa amekodisha kwa muda ili kuwahudumia wateja wake.

Kwa mujibu wa jirani wa marehemu aliingia chumbani na mtu ambaye anashukiwa kumuua.

“Rafiki yangu aliingia chumbani akiwa na mteja wake majira ya saa tisa asubuhi na mwanamume huyo akaondoka mwendo wa saa tano asubuhi siku ya Jumanne. Nilishuku kulikuwa na kuna kitu kisichokuwa cha kawaida nilipogundua kuwa mlango ulikuwa wazi, nilipoingia ndani nilikuta mwili wake ukiwa umefungwa kitambaa huku ukitokwa na damu,” alisema mwanamke huyo aliyejitambulisha kwa jina la Nancy Maria. Tukio hilo liliripotiwa katika kituo cha polisi cha Baharini.

Maafisa wa polisi kutoka kituo hicho walizuru eneo la tukio na kuupeleka mwili huo katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya mafunzo na rufaa ya Moi (MTRH) huku uchunguzi ukianza.

Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi Uasin Gishu Stephen Okal alisema kuwa polisi hawajabaini chanzo cha mauaji hayo.

Bw Okal alisema wanamtafuta mshukiwa huyo kwa matumaini ya kumkamata haraka iwezekanavyo.

Mauaji hayo yamezua hisia kali kutoka kwa makundi ya kiraia yanayopigania haki za wafanyabiashara wa ngono wakidai kuwa mauaji kama hayo yanaongezeka jijini Eldoret.

“Hili si tukio la kwanza la aina hii, katika kipindi cha chini ya miezi minne takriban wanawake watatu wameuawa kwa namna hiyo hiyo, kwa sasa miili ya wenzetu wawili iko katika chumba cha kuhifadhia maiti baada ya kuuawa kwa namna kama hiyo,” alisema Ruth Kakenya mwanaharakati wa masuala ya jinsia anayetetea haki za wafanyabiashara wa ngono jijini Eldoret.

Bi Kakenya alisema kesi za unyanyasaji wa kijinsia miongoni mwa wafanyakazi wa kike ikiwemo kesi za ubakaji zinazidi kuongezeka.

Amewataka polisi kuharakisha uchunguzi wa matukio hayo.