Makala

Mama aliyepuuza ushauri wa bosi kuavya mimba ataabika bila ajira

Na FRIDAH OKACHI September 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

MILKAH, 35, (si jina lake halisi) kutoka Nairobi, amesalia nyumbani zaidi ya mwaka mmoja baada ya kuacha kazi kutokana na ubaguzi dhidi ya ujauzito wakati bosi wake alipomhimiza kuavya mimba.

Nchini, kwenye Katiba, Sheria ya Wafanyakazi sehemu (ii) Kifungu cha 5 (3), mwajiri hana ruhusa ya kumbagua mfanyakazi wake kwa njia yoyote au kumnyanyasa kwa misingi ya rangi, jinsia, dini, siasa, kabila au jamii, ulemavu, hali ya kiakili, virusi vya ukimwi na ujauzito.

Pia, sehemu ya (iv) Kifungu cha 46 (a) Mwajiri haruhusiwi kumfukuza mwanamke mjamzito au kumpa adhabu yoyote inayohusiana na ujauzito wake.

Hata hivyo, Milkah alipokea adhabu ya kutengwa kwenye mikutano muhimu pamoja na kushushwa cheo baada ya kumfahamisha mwajiri wake anaujauzito.

“Mimi na bosi wangu tulikuwa marafiki sana. Ndipo aje kuanzisha kampuni yake nchini Kenya, alinihusisha kumtafutia wafanyakazi. Pia, nilihusika kununua hisa. Kutokana na urafiki wetu nilinunua hisa,” alieleza Milkah.

Alimweleza bosi wake kuhusiana na ujauzito, akiwa na matarajio ya kupongezwa.

“Alinishauri kuavya mimba. Alinieleza kazi hiyo ambayo wakati mwingi nilifanya nikiwa afisini kwa wakati huo itahitaji mwanamume kwa kuwa hana muda ya kubeba ujauzito,” alishangaa Milkah.

Kwa wakati huo, mama huyo wa mtoto mmoja, alichukulia usemi huo kuwa mzaha. Siku zilivyosonga, urafiki wao ulizidi kuingia doa, kila mara akipokea simu ya mwajiri wake akitaka kufahamu iwapo alifuata ‘ushauri’ aliompa.

Taifa Dijitali, iliweza kusikiza sauti zilizonakiliwa na Milkah wakati wa mazungumzo ya simu na bosi huyo.

“Natumai uliwazia ushauri ambao nilikupa. Kazi nyingi ikiwemo hii unayofanya haifanywi na wanawake wajawazito. Mwanamke anapopata mtoto mambo mengi hubadilika kama vile kuomba ruhusa kila wakati,” ilisema sauti ya bosi iliyonakiliwa.

“Siwezi kufanya hivyo, nikizingatia kuwa huyu atakuwa mwangu wa kwanza. Umri hauniruhusu kusubiri zaidi,” alimjibu Bi Milkah.

Maji yalizidi unga baada ya daktari wa Milkah kumshauri kupunguza safari za kila mara kutokana na matatizo ya kiafya. Huu ukiwa ni mwanzo wa kumbagua wakati wa mikutano na wafanyakazi wengine.

Milkah alifahamu kuwa anatengwa baada ya wenzake kumuuliza sababu za kutohudhuria mikutano. Hali hiyo ilipelekea mawazo mbalimbali ya kufanikisha kampuni hiyo yakitupiliwa mbali.

 “Matendo yake yalibadilika, baadhi ya wafanyakazi walishangaa mbona sihusishwi na mikutano inayoandaliwa naye. Mapendekezo niliyotoa kupitia kwa barua pepe yalitupiliwa tu,” alikerwa.

Desemba 2022, Milkah alipata uvumi uliosambaa kuwa kampuni ilikuwa ikitafuta mtu wa kuchukua nafasi yake kabla ya kuelekea kwenye likizo ya kujifungua.

Kwa ujasiri alifika katika afisi ya meneja wa wafanyakazi ili kufahamu sababu ya nafasi yake kutangaza wazi bila majadiliano naye. Meneja huyo alimtaka kupuuza akihoji kuwa ni uvumi tu.

Miezi mitatu baada ya kurejea kazini, alipata nafasi yake haipo. Mwajiri wake aliomba kufanya mazungumzo naye. Kwenye kikao hicho bosi wake alimpendekezea kufanya kazi tofauti.

“Nilimkumbusha nafasi anayosisitiza ni njia moja ya kunieleza niondoke. Maana alijua tulijaribu kuajiri wafanyakazi kadhaa na haikufua dafu,” alisema.

Milkah alishikilia msimamo wake kuwa angependa kurejea katika nafasi yake kwa kuwa pendekezo alilipowea halikuwa linaendana na viwango vya masomo yake.

Hatimaye alijiuzulu akiomba kupewa cheti cha kuonyesha alifanya kazi pale. Kampuni hiyo ilimpa masharti magumu yaliyokusudiwa kumzuia asizungumze kuhusu jinsi alivyotendewa kinyama.

“Nilishangaa kuelezwa nisitoe sababu zozote za kujiuzulu. Pia, walitaka cheti hicho kuandikwa nilijiuzuru kazi mnano Novemba 2023, ilhali ilikuwa Juni, 2023.”

Katika ombi lake kwa Mahakama ya Wafanyakazi nchini, Milkah alitafuta haki ya ubaguzi dhidi ya ujauzito pamoja na kurejeshewa hisa zake.

Miongoni mwa malalamishi mengine ni kulipwa bonasi kulingana na mkataba wa kampuni hiyo.

Kwenye kesi hiyo, mshtakiwa alipinga madai yaliyotolewa na mlalamishi. Alijitetea kuwa rekodi zilizowasilishwa na Milkah ilikuwa kinyume na miongozo ya mahakama. Malipo aliyodai alisema yatalipwa mwisho wa mwaka.

Mahakama ilimwelekeza mwajiri wa Milkah, kumpa cheti hicho kabla ya siku saba pamoja na hisa bila fidia.

Meneja anayehusika kuajiri wafanyakazi Bi Vanice Olal, aliambia Taifa Dijitali, matukio hutokea kwenye kampuni mbalimbali nchini. Alitaja baadhi ya kampuni hutumia mbinu ya kuwashusha madaraka ikiwa ni mbinu ya kuwafuta.

“Wakati mama mjamzito anapoeleka kwenye likizo ya miezi mitatu, unapata kampuni nyingi hazina mbinu ya kutafuta mtu wa muda wa kushikilia kazi ile. Yule mama anaporejea, utapata anafuta kazi au kupewa nafazi ambayo ni tofauti na ile ya awali na si haki.”