Jamvi La SiasaMakala

Mapambano yanukia vyama vya Ruto na Raila vikifanya uchaguzi

Na MOSES NYAMORI April 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA tawala cha United Democratic Alliance (UDA) na Orange Democratic Movement (ODM) vinafanya maandalizi ya mwisho ya uchaguzi wa mashinani uliopangwa kufanyika wiki ijayo.

Uchaguzi wa vyama hivi viwili vikubwa vya kisiasa unaashiria kuwepo mapambano makali katika harakati za kudhibiti vyama hivyo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027, huku nchi ikitarajia mabadiliko makubwa ya kisiasa.

ODM, chama kinachoongozwa na mwanasiasa wa miaka mingi Raila Odinga, tayari kimetuma maafisa wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo bunge yote 290 na maafisa wa kusimamia uchaguzi katika wadi zote kabla ya zoezi hilo lililopangwa kufanyika Jumatatu na Jumatano.

Chama cha UDA, kinachoongozwa na Rais William Ruto, pia kimepanga mafunzo kwa maafisa wake wa uchaguzi kuanzia Jumatatu, kabla ya uchaguzi kufanyika Ijumaa na Jumamosi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi ya UDA, Antony Mwaura, alisema Jumatano kuwa watatumia vifaa 15,000 vya kidijitali katika zoezi hilo ili kufanikisha mchakato huo katika kaunti 17.

Bw Mwaura alisema mafunzo kwa maafisa wa uchaguzi yataanza Jumatatu hadi Alhamisi na akawahakikishia wagombeaji kuwa mchakato huo utakuwa huru na wa haki.

Mnamo Aprili 11, zoezi hilo litafanyika katika kaunti za Kitui, Machakos, Makueni, Kajiado, Turkana, Kisii, Nyamira na Bungoma. Kaunti nyingine ni Migori, Siaya na Kisumu.

Mnamo Aprili 12, uchaguzi utafanyika katika kaunti za Garissa, Wajir, Mandera, Marsabit, Isiolo na Taita Taveta.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uratibu wa Uchaguzi wa ODM, Emily Awita, alisema chama kimeweka mipango yote kuhakikisha mchakato huo unakuwa wa kuaminika.

“Uchaguzi wa Jumatatu utafanyika katika ngazi ya tawi dogo, ambayo ni wadi. Katika ngazi ya wadi, ni wajumbe pekee walioteuliwa katika vituo vya kupigia kura ndio watakaoshiriki katika zoezi hilo. Wale watakaochaguliwa kama wajumbe wa wadi wataendelea hadi ngazi ya tawi, ambapo uchaguzi utafanyika Jumatano, Aprili 9, 2025,” alisema Bi Awita.

“Tuko tayari kabisa kwa zoezi hili. Mipango yote imekamilika, na tunatarajia mchakato huo uende vizuri. Tumewaajiri na kuwapanga wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo bunge yote 290 na wasimamizi wa uchaguzi katika wadi zote kuhakikisha zoezi linaendelea bila matatizo.”

Uchaguzi wa maeneobunge unaonekana kuwa moja ya mapambano makubwa katika harakati za kudhibiti chama.

Viongozi walioko madarakani na wale wanaotazamia kugombea mwaka 2027 ni miongoni mwa wale wanaojiandaa kwa uchaguzi wa maeneobunge, ambapo matokeo yake yatakuwa na athari kubwa kwa uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa chama.

Wenyeviti wote wa maeneobunge ni wanachama wa Baraza la Kitaifa la Wajumbe wa chama (NDC), chombo cha juu chenye mamlaka ya kuamua sera za chama na kuchagua maafisa wa kitaifa.

Baadhi ya wabunge wa sasa wanahudumu kama wenyeviti wa maeneobunge na huenda wakatetea nyadhifa zao au kuteua washirika wao ili kudumisha udhibiti wa chama katika maeneo yao.

Baadhi ya wabunge pia ni wenyeviti wa matawi ya kaunti – kama vile Mbunge wa Makadara, George Aladwa (Nairobi) – na wangependa watakaochaguliwa waweze kusaidia kuhifadhi viti vyao katika ngazi ya kaunti.

Kuwa afisa wa chama, hasa kwa wale wanaotaka kugombea mwaka 2027, kunachukuliwa kuwa ni faida katika kupata tiketi ya chama.

Uchaguzi huu umepangwa kama sehemu ya mpango wa Bw Odinga wa kuimarisha chama kabla ya uchaguzi wa 2027.