MAPOZI: Mwanamuziki Evelyne Wanjiru
Na PAULINE ONGAJI
JINA lake katika ulingo wa muziki wa injili nchini sio geni; na sio kutokana na mwangaza mbaya wa habari au muziki tata, bali ni kwa nyimbo zake zenye ujumbe wa kina, kazi ambazo hazijachepuka mbali na ujumbe halisi wa injili.
Ni mojawapo ya sababu ambazo zimemuorodhesha Evelyn Wanjiru miongoni mwa wasanii wa injili wanaoheshimika sana Kenya huku akijiundia jina kwa kazi zake ambazo mbali na kutumbuiza, zimezidi kudumisha ujumbe halisi, tofauti na baadhi ya wasanii wa kisasa.
Huku akijivunia albamu tatu; Waweza, Mungu Mkuu na Matendo, zinazojumuisha nyimbo kama vile Waweza, Unatosha, Mungu Mkuu, Utukufu, Nikufahamu, Baba Inuka, Jehova Elohim na It’s Amazing, ni dhahiri kwamba Wanjiru ni Jina Kubwa katika ulingo wa muziki nchini.
Ni sifa hii ambayo imemfanya kutambuliwa katika tuzo mbalimbali huku akiteuliwa na kutuzwa katika baadhi ya tuzo zinazotambulika, ikiwa ni pamoja na tatu za Groove Awards na nne za Xtreem Awards.
Na katika harakati hizo amezuru mataifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini, Ghana, Zimbabwe, Tanzania, Sudan Kusini, Uganda na majimbo kadha ya Amerika, huku akitumbuiza kwenye jukwaa moja na baadhi ya majina makubwa kwenye ulingo wa muziki wa injili, kama vile Sinach na Mary Mary miongoni mwa wengine.
Kadhalika anajivunia kuhirikiana na wasanii wa haiba ya juu nchini na mbali.
Kwa mfano kwenye kibao Sawa ameshirikiana na mwanamuziki Tembalami kutoka Zimbabwe. Pia ana fahari ya kufanya kazi na mwanamuziki Mkhululi Bhebhe kutoka Afrika Kusini na Celestine Donkor kutoka Ghana.
Wanjiru alianza kuimba akiwa mchanga huku kipaji chake kikijitokeza akiwa na miaka tisa pekee, ambapo tayari alikuwa anaimba kanisani na katika tamasha za muziki shuleni. Akiwa shuleni alijihusisha sana katika drama na kwaya ya shuleni.
Kitovu cha ufanisi
Ufanisi wake kama msanii ulijiri baada ya kukutana na produsa Agundabweni Akweyu ambapo pamoja walianzisha studio ya Bwenieve Productions.
Alirekodi albamu yake ya kwanza kwa jina Mazingira ambayo baadaye ilibadilishwa na kuwa Waweza. Albamu hii ilimletea umaarufu hasa uliotokana na vibao Waweza na Hossana.
Wimbo Waweza uliteuliwa kama wimbo wa sifa wa mwaka huku Wanjiru akiteuliwa kama msanii chipukizi wa mwaka katika tuzo za Groove Awards mwaka 2012. Mwaka wa 2010 kibao Mazingira kilichaguliwa kama wimbo maalum katika kampeni za serikali ya Kenya za kurejesha hali ya awali ya Msitu Mau.
Katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu alifurahishwa na wimbo huo kiasi cha kumteua Wanjiru kama mjumbe rasmi wa muziki wa msitu Mau. Ni hapa ndipo alianzisha kampeni ya Mazingira Bora Afya Bora katika jitihada za kuimarisha mazingira na afya bora.
Kibao Mungu Mkuu amabacho pia kilikuwa kichwa cha albam yake ya pili kilishinda tuzo ya albamu ya mwaka kwenye tuzo za Groove Awards mwaka wa 2015, na hivyo kumuinua hata zaidi.
Kwa upande mwingine wimbo wake Tulia kutoka kwa albamu yake ya tatu Matendo alichoimba kwa ushirikiano na Vick Kitonga, kilishinda tuzo za ushirikiano wa mwaka kwenye tuzo za Groove Awards mwaka wa 2016, huku Nikufahamu pia kutoka kwa albamu hiyo kikiteuliwa kwenye tuzo za Afrimma. Kadhalika alitwaa tuzo ya msanii bora wa kike wa mwaka eneo la Afrika Mashariki kwenye tuzo za Xtreem.
Mwaka wa 2017 aliteuliwa mara mbili kwenye tuzo za Groove awards; msanii bora wa kike wa mwaka huku albamu yake Matendo ikiteuliwa kama bora mwaka huo. Hii ilikuwa kando na kuteuliwa kwenye tuzo za Sauti Awards nchini Amerika, katika vitengo vya msanii bora wa kike wa mwaka na video ya mwaka.
Haina shaka kwamba Evelyn Wanjiru amezidi kung’aa kimuziki pasipo kuchujua ujumbe wa injili kutoka kazi zake, na hivyo kuwa mfano wa kipekee kwa wasanii chipukizi wa injili.