Makala

Mara hii atabahatika? Azma ya Raila AUC yapigwa jeki, ushidani ukibaki Djibouti na Madagascar pekee

Na CHARLES WASONGA November 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

AZMA ya Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kutwaa wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) imepigwa jeki baada ya taifa la Mauritius kumuunga mkono.

Hatua hiyo inaashiria kuwa Waziri wa zamani wa Masuala ya Kigeni wa nchi humo Anil Kumarsingh Gayan, anayewania kiti hicho, sasa ameondoka kinyang’anyironi.

Hii ni kwa sababu kulingana na kanuni ya uchaguzi wa uenyekiti wa AUC, wagombeaji sharti waungwe mkono na serikali za nchi zao.

Lakini Jumanne, Novemba 26, 2024, Waziri Mkuu wa Mauritius Navinchandra Ramgoolam alitangaza kuwa anamuunga mkono Bw Odinga kwa cheo hicho.

Mawasiliano kwa njia ya simu

Hii ni kufuatia mawasiliano kwa njia ya simu kati ya Rais William Ruto na Ramgoolam, ambaye ndiye kiongozi wa Mauritius na  atakayeshiriki katika upigaji kura kuamua mwenyekiti mpya wa AUC, 2025.

Wakati wa mazungumzo hayo, Rais Ruto alimshukuru Waziri Mkuu huyo kwa uamuzi huo huku akikariri uwepo wa ushikiano mzuri kati ya Mauritius na Kenya.

“Nimefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu mpya wa Mauritius Mheshimiwa Navinchandra Ramgoolam. Nampongeza kwa kuchaguliwa kwake na kwa imani ambayo watu wa taifa lake wameweka kwake na chama chake,” Rais Ruto akaeleza.

“Waziri Mkuu Ramgoolam pia amethibitisha kuwa anaunga azma ya mgombeaji wa Kenya katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mheshimiwa Raila Odinga, na ninamshukuru zaidi kwa hilo,” Rais akaongeza kwenye ujumbe katika akaunti yake ya mtandao wa X (zamani, Twitter).

Wadadisi wanasema

Wadadisi wanasema kuwa mpinzani mkuu wa Bw Odinga ni Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf, kwa misingi kuwa anaungwa mkono na mataifa yanayozungumza Kiarabu na Kifaransa. Aidha, anayo tajriba kubwa katika anga ya diplomasia.

Mpinzani mwingine aliyesalia ni aliyekuwaWaziri wa Masuala ya Kigeni wa Madagascar Richard James Randriamandrato.

Bw Odinga amepata uungwaji mkono kutoka Mauritius wakati ambapo yuko katika ziara ya Mataifa ya Magharibi mwa Afrika akisaka uungwaji mkono.

Wakati wa ziara hiyo, alikutana na kufanya mashauriano na Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye, Rais wa Cote d’Ivoire Alassane Ouattara, Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu na Rais wa Gambia Adama Barrow.

Aidha, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi amethibitisha kuwa serikali inaendesha kampeni kali ya kumtafutia Odinga uungwaji mkono katika mataifa ya Kusini mwa Afrika na mataifa ya Eneo la Maziwa Makuu.

Odinga alianza kampeni kwa kuungwa na EAC

Mnamo Agosti mwaka huu, Bw Odinga alianza kampeni zake kwa kupata uungwaji mkono kutoka kwa marais mataifa matano wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mataifa hayo ni; Uganda, Rwanda, Tanzania, Sudani Kusini na Burundi.

Kulingana na kanuni za uchaguzi wa AUC mshindi katika uchaguzi wa mwenyekiti sharti apate angalau thuluthi mbili za kura za mataifa 54 wanachama wa Umoja wa African (AU).

Mwenyekiti wa sasa wa AUC Moussa Faki Mahamat anastaafu rasmi Februari mwakani baada ya kuhudumu kwa mihula miwili. Ni Waziri Mkuu wa zamani wa Chad.