Mashujaa Dei 2025: Ruto ataka vijana 100,000 wenye biashara kupewa Sh50, 000 kila mmoja
RAIS William Ruto amewataka mawaziri wake, makatibu na wahudumu wa serikali kumsaidia kupata vijana 100,000 waliowekeza kwenye biashara ili kupigwa jeki.
Kiongozi wa nchi, akihutubu Jumatatu, Oktoba 20, 2025 wakati wa maadhimisho ya Mashujaa Day, alisema anataka idadi hiyo ya vijana kabla ya mwisho wa mwaka.
Aidha, watapigwa jeki kupitia programu mpya ya Nyota inayolenga vijana wenye biashara. “Serikali, kabla ya mwisho wa mwaka huu itapiga jeki vijana 100,000 walio kwenye biashara kila mmoja akabidhiwe Sh50, 000,” Rais aliahidi.
Kiongozi wa nchi alisema kutakuwa na zoezi la kuwapiga msasa mnamo Ijumaa, Oktoba 24 katika kila eneobunge, ili kutambua watakaofuzu. Dkt Ruto alielezea kwamba hatua hiyo ni mojawapo ya ahadi zake 2022, kupiga vijana jeki nchini kujiendeleza kibiashara.
Miezi michache 2022 baada ya kuchukua dhana za uongozi, Rais alizindua mpango wa Hustler Fund – mradi uliolenga kuinua wafanyabiashara. Fedha hizo za mkopo zikitolewa kwa njia ya simu, baadhi ya waliochukua wameripotiwa kukosa kurejesha.