DimbaMakala

Mauano Barcelona, Real Madrid wakitoana makamasi

Na GEOFFREY ANENE October 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MACHO yatakuwa kwa wavamizi matata Vinicius Junior na Robert Lewandowski wakati Real Madrid na Barcelona watapimana ubabe katika mpepetano wa kwanza wa El Clasico msimu huu,  Jumamosi ugani Santiago Bernabeu.

Mahasimu hao wataingia gozi hilo lao la 258 wakikamata nafasi mbili za kwanza kwenye Ligi Kuu ya Uhispania kwa alama 27 na 24, mtawalia.

Madrid hawajapoteza ligini msimu huu baada ya mechi 10 za kwanza.

Vijana wa kocha Carlo Ancelotti wanaonekana wameshika moto sasa baada ya kuonyesha wanaweza kutoka chini na kutwaa ushindi walipochabanga Borussia Dortmund 5-2 kupitia mabao ya Vinicius (matatu), Antonio Rudiger na Lucas Vazquez kwenye Klabu Bingwa Ulaya.

Dortmund waliongoza 2-0 wakati wa mapumziko kupitia magoli ya Donyell Malen na Jamie Bynoe-Gittens kabla ya Real kuonyesha ukatili mkubwa katika dakika 45 za mwisho.

Barca pia wamejaa imani baada ya kubomoa Bayern Munich 4-1 kwenye mashindano hayo ya Ulaya, Raphinha akiona lango mara tatu naye Lewandowski akichangia goli moja.

Vijana wa kocha Hansi Flick hawana ushindi katika mechi nne mfululizo za El Clasico zisizo za kirafiki. Hata hivyo, Barca walilemea Real 2-1 katika mara ya mwisho walikutana Agosti 21 katika mechi ya kirafiki na pia Real kwa sasa wana mapigo mawili makubwa.

Wenyeji Real watamkosa kipa nambari moja Thibaut Courtois na winga Rodrygo, wachezaji ambao bila majeraha wangeanza mechi hii.

Andriy Lunin atakuwa michumani. Kutokana na Rodrygo kuumia, Ancelotti atakuwa na kibarua kigumu kupanga safu ya mashambulizi.

Jude Bellingham huenda akaungana na Vinicius na Kylian Mbappe katika mfumo wa washambulizi watatu mbele.

Ikiwa hivyo, Aurelien Tchouameni atashirikiana na Eduardo Camavinga katika safu ya kati, ingawa inaweza kuwa mapema sana kutumia Tchouameni ambaye amerejea kutoka mkekani.

Barcelona ilimwanzisha Fermin Lopez dhidi ya Bayern kupima usawa wake kimwili. Huduma za viungo Gavi na Frenkie de Jong pia zinapatikana tena naye Dani Olmo yumo mbioni kupata dakika zaidi uwanjani.

Hata hivyo, Barca bado itakuwa bila kipa nambari moja Marc-Andre ter Stegen pamoja na Andreas Christensen na Ronald Araujo walio katika chumba cha majeruhi.

Lewandowski anaongoza ufungaji wa mabao kwenye LaLiga msimu huu baada ya kuchana nyavu mara 12 akifuatiwa na Mbappe (sita) nao Raphihna na Vinicius wana mabao matano kila mmoja.