Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Kadri maafa mengi yanavyotokea duniani tunafaa tuandae nafsi zetu kwa mauti

March 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na ALI HASSAN

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na neema ndogondogo.

Tumejaaliwa leo hii, siku hii kubwa ili kuambizana mawili matatu kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Awali ya yote twachukua uzito wa nafasi hii kumshukuru mno na kumpwekesha Mola wetu Muumba, Allah (SWT).

Kwa maana hiyo ni kuwa hapana Mola mwingine anayestahili kuabudiwa isipokuwa Mungu mmoja Mwenye-Enzi-Mungu.

Ni yeye pekee ndiye Muumba wa ardhi na mbingu na vyote vilivyomo, na anastahili kuabudiwa kwa kila hali. Ni yeye pekee ndiye akisema jambo kuwa linakuwa.

Ni yeye pekee ndiye ambaye anajua hatima yetu, riziki zetu na maisha yetu yote tangu mwanzo hadi mwisho.

Maisha yetu yote hayaendi ila kwa mapenzi yake na majaaliwa yake Maulana.

Katika uzi uo huo, twachukua nafasi hii pia kumtilia dua na kumtakia kila la kheri Mtume wetu (SAW).

Ili pia kufaulisha hili, ni wajibu wetu kujifunga masombo na kujikaza kisabuni ili kuona kuwa tunazingatia sunna za Mtume wetu (SAW) na pia kuishi kwa kuzingatia mafunzo yaliyomo katika kitabu chetu kitukufu cha Kurani.

Leo hii ndugu yangu mada yetu ni mada ambayo inasemwa na kuimbwa kila kukicha na mashekhe na maustadh wetu. Mada yenyewe si nyingine ila ni kifo.

Yaani kila nafsi itakuja kuyaonja mauti. Ndio maana sisi tulio hai sharuti kujipanga na kujiandaa viwavyo kwa ajili ya mauti.

Swali ambalo yafaa sisi waja-waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamua yafaa kujiuliza ni kwa namna gani, vipi na wapi malaika wa mauti atakuja kuzichukua roho zetu?

Hivi Mola wetu akiamua kuzitwaa nafsi zetu, tutakuwa katika mazingira gani?

Hapo ulipo ndugu yangu lazima unajiuliza ni kwa nini leo hii tukaamua kuangazia mada hii leo.

Kikubwa ambacho kimetufanya kuangazia mada hii leo hii ndugu zangu waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu ni kuwa bindamua ni msahaulifu.

Ndiyo maana upo umuhimu wa kukumbushana kila leo, kila nukta, kila sekunde.

Usahaulifu

Leo hii sisi waja tunashuhudia ndugu zetu, jamaa zetu, marafiki zetu, majirani zetu, wazazi wetu, kaka zetu, dada zetu na watu wa matabaka na dini mbali mbali wakiaga dunia kila leo.

Lakini ajabu ni kuwa binadamu ni msahaulifu mkubwa.

Punde baada ya kuzipokea taarifa za tanzia, au mara tu tunapomaliza kuwazika jamaa zetu, tunasahau na kuyaruidia maasi.

Dini yetu tukufu ya Kiislamu, kupitia kitabu chetu kitukufu cha Kurani na mafunzo ya Mtume wetu (SAW), imetuonesha hali halisi. Namna ya kuishi kwa matamanio ya maisha ya kudumu, maisha ya baadaye. Lakini wawapi! Ya Rabi jamani!
Ni wangapi tuliokuwa nao jana, na leo hii tunayaona makaburi yao? Kwa nini basi tusijiulize ni kwa nini sisi tungali hai? Mola ana sababu. Na kama tungali hai leo hii, kesho tutakuwa wapi?

Achia mbali mauaji ya mtu mmoja. Mauaji ambayo hushtua sana ni yale ya umati. Kutokee moto vile. Au mafuriko. Ama mashambulizi ya kigaidi tuseme.

Mbaya ni ajali. Sasa hivi kote nchini msiba umetanda kote. Hii ni baada ya ndugu zetu kuaga dunia kutokana na ajali ya ndege iliyotokea nchini Ethiopia.

Jiulize ni kwa vipi wasafiri walivyokuwa wamewaaga jamaa zao. Na kisha kuwaandaa na kuwapigia simu jamaa na marafiki zao wa kuwapokea huko walikokuwa wakielekea.

Baadhi walikuwa wakilenga makongamano. Wengine kuzumbua riziki. Na wengine wakirejea makwao baada ya kukaa nje ya nchi zao kwa muda. Lakini wako wapi?

Baadhi yao walikuwa wameandaa sherehe za makaribisho. Lakini angalia ajali ilivyowapoka wapendwa wao. Makiwa!

Watoto wameachwa mayatima. Wake wameachwa wajane. Wengine ni wafaruku. Yaani ni huzuni na kihoro tele! Makiwa!

Msiba kama huo, janga la kimataifa kama hilo hutuacha sisi wanadamu na maswali mengi. Yafaa swali kubwa tuwe tunajiuliza ni kwa vipi tumejitayarisha kuyapokea mauti. Hivi tuko tayari kukipokea kifo?

Kwake Mola ndiko tutokako na kwake ndiko yaliko marejeo yetu. Je, ni kwa vipi tuko tayari kuyapokea mauti? In shaa Allah tuwe na mwisho mwema.

 

Ijumaa Kareem

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]