MAWAIDHA YA KIISLAMU: Suala la dini halifai kupuuzwa katika mchakato mzima wa BBI
Na ALI HASSAN
KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na neema ndogondogo.
Tumejaaliwa kukutana tena leo hii, siku hii kubwa aula na tukufu, ili kukumbushana neno lake Mola wetu. Kuzidisha ibada. Kukatazana mawi na kukumbushana umuhimu wa kufanya amali za kheri.
Hakuna kingine kikubwa tunachostahili kufanya katika ardhi hii ila tu ni kumwomba na kumwabudu Mola wetu.
Mwanzo, tuufungue uwanja wetu wa mawaidha leo hii kwa kumtukuza, kumkumbuka na kumuenzi Mola wetu. Kwa maana hiyo ni kuwa kama ilivyo ada ya dini yetu hii tukufu ya Kiislamu ni kuwa hapana mwengine anayepaswa kuabudiwa ela ni Mola pekee. Yeye, Allah (SWT), ndiye ambaye anayestahili kuabudiwa, kutukuzwa na kumwaiya kila aina ya shukrani, pongezi, sifa na ahsante.
Kisa na maana? Hapana mwingine anayepaswa kuabudiwa; na yeye ndiye Muumba wa ardhi na mbingu na vyote vilivyomo.
Ama katika usanjari huo, twachukua uzito wa nafasi hii kumtilia dua na kumkumbuka kwenye maombi Mtume wetu (SAW).
Maongezi, mawaidha ama nasaha zetu za leo ukipenda ndugu yangu muumin wa dini hii tukufu ya Kiislamu, ni mwendelezo wa mawaidha tuliokuwa nayo wiki jana, siku kama ya leo, kwenye ukurasa au ukipenda ukumbi huu.
Tulichoangazia wiki jana kilihusu nafasi ya viongozi wa dini yetu kujitokeza na kuwa katika mstari wa mbele kutetea dini na maslahi ya umma. Kikubwa tulikuwa tukiurejelea mchakato mzima wa mchango mzima unaohitajika kwenye mdahalo na mikakati ya ripoti ya jopokazi la maridhiano na mapatano ya BBI.
Kisha, kwa sasa, ni kuzipata kauli za viongozi wetu wa dini kuhusiana na maoni, mapendekezo yanayohitajiwa na yanayokusanywa na kamati tekelezi ya BBI.
Kila jambo la kheri huwa na mwanzo mzuri na mwisho mzuri pia. Hivi ni kusema kuwa ili kila jambo lifaulu, muhimu na sharuti kumweka Mola mbele. Na sauti na mafunzo ya Mola yanatolewa vizuri kupitia kwa viongozi wetu wa dini. Ndio hapo basi tunazidi kuwahimiza kujitokeza.
Mikutano kadha imeandaliwa kujadili na kukusanya maoni ya BBI. Mingine mingi itaandaliwa In shaa Allah. Ndio maana hatutosita kwa uwezo wake Maulana kuhimizana ili dini ipewe kipaumbele katika mchakato mzima huu.
Mbali na viongozi wetu wa dini, katika uzi uo huo wa BBI na mikutano yake, leo hii tungependa kuzungumza na viongozi wetu wa Kiislamu, wawe wa dini au siasa. Aidha, semi zetu leo hii zinawalenga wote ambao ni viongozi. Sio tu Waislamu.
Ni ombi kuwa kwenye mikutano hii, na shughuli nyinginezo, viongozi wetu – almradi ni viongozi – waoneshe mfano mzuri kwa umma na nchi kwa ujuma. Ulimwengu mzima unawatazama. Nyie ni viongozi. Umma unawahitaji na kuwategemea kutoa mwongozo. Lakini ni kama viongozi wetu wanachupa mipaka.
Kivipi?
Lugha ambazo zinatumiwa na viongozi wetu zinasinya, kuudhi na kuchusha. Ajabu ni kuwa kauli hizi zinapeperushwa hewani katika vyombo mbali mbali vya habari na kupokelewa na waumini wa jinsia tofuati, dini tofauti, umri tofauti na misingi ya kila aina.
Mbali na matusi, lugha chafu, yapo mavazi ambayo pia si mazuri, sikwambii kukumbatiana ovyo, kukosa itifaki na kuvurugana. Cha kuudhi zaidi, Mola atuepushe In shaa Allah, ni kuwa viongozi ni kama wanaabudiana. Akishasema kiongozi wa mrengo au chama ni basi, haifai kupinga wala kutoa maoni tofauti.
Sura ya Al-Hajj aya ya 30 inasema:
“Namna hivi iwe; Na anayevitukuza vitu vitakatifu vya Mwenyezi Mungu, basi (kufanya) hivyo ni kheri yake mwenyewe mbele ya Mola wake. Na mmehalalishiwa wanyama isipokuwa wale mnaosomewa humu (katika Quran kuwa wasiliwe); Basi jiepusheni na uchafu wa masanamu na jiepusheni na usemi wa uwongo.”
Ili kushadidia umuhimu wa sisi waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu kumwabudu Mola mmoja pekee, sura hiyo ya Al-Hajj aya ya 31 inaendelea kusema:
“Mkhalisike kwa Mwenyezi Mungu, bila kumshirikisha. Na anayemshirikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka kutoka mbinguni, kisha ndege wakamnyakua au upepo kumtupa mahali pa mbali.”
Kisha aya ya 32 inamalizia kwa kusema:
“Namna hivi; anayeziheshimu alama za (dini ya) Mwenyezi Mungu, basi hilo ni jambo la utawa (ucha Mungu) wa nyoyo.”
Ijumaa Kareem!