MAZINGIRA NA SAYANSI: Mifuko yaundwa kwa mihogo katika juhudi kutunza mazingira
Na LEONARD ONYANGO
MIFUKO ya plastiki iliyopigwa marufuku na serikali mnamo 2017 huenda ‘ikarejea’ sokoni humu nchini.
Lakini mifuko hiyo mipya haitakuwa imetengenezwa kwa plastiki bali kwa mihogo.
Mifuko iliyopigwa marufuku imetengezwa kwa petrol na haiwezi kuoza hata inapozikwa ardhini au kutupwa ndani ya maji kwa zaidi ya miaka 30 na zaidi.
Watafiti kutoka Brazil wameunda mifuko ya ‘plastiki’ iliyotengenezwa kwa mihogo ambayo itatumika kufungia vyakula na kubebea bidhaa.
Kenya ilipiga marufuku utengenezaji na matumizi ya mifuko ya plastiki miaka miwili iliyopita kwa lengo la kutunza mazingira.
Mtu anayepatikana akiuza au kutumia mifuko ya plastiki yuko katika hatari ya kufungwa miezi 12 gerezani au kutozwa faini ya Sh3 milioni au vyote.
Watafiti wa nchini Brazil wanachanganya unga wa mihogo na gesi ya ozone (O3) kutengeneza mifuko hiyo.
Gesi ya ozone hubadilisha unga wa mihogo kuwa mzito mithili ya plastiki.
Kila mwaka tani milioni 300 za plastiki hutengenezwa kila mwaka kote duniani, kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (UN Environment), asilimia 14 ya plastiki hukusanywa na kutumiwa kwa mara ya pili. Kiasi kikubwa cha plastiki hutumika mara moja tu.
Kila mwaka tani milioni 8 za plastiki huingia katika vyanzo vya maji kama vile bahari, maziwa na mito.
Samaki na viumbe wengineo wa majini hufariki baada ya kula plastiki hizo.
Kulingana na UN, plastiki hutoa kemikali zinazojulikana kama phthalates na Bisphenol A (maarufu BPA).
Kemikali hizo hudhuru homoni za mwili wa wanyama na wadudu wengineo. Kemikali hizo pia husababisha mwasho wa mwili na hata kudhuru mishipa ya damu ya ubongo na hata kitovu cha mtoto aliye tumboni.
“Majaribio tuliyofanya yameonyesha kuwa mifuko iliyotengenezwa kwa unga wa mihogo inaoza inapofukiwa ardhini na wala haichafui mazingira tofauti na ile mifuko ya plastiki iliyotengenezwa kwa petroli,” akasema kiongozi wa watafiti hao Carla Ivonne La Fuente Arias wa Chuo cha Kilimo cha Luiz de Queiroz ambacho ni tawi la Chuo Kikuu cha Sao Paulo.
Kulingana na utafiti huo uliochapishwa katika jarida la International Journal of Biological Macromolecules, gharama ya kutengeneza mifuko hiyo iko juu ikilinganishwa na mifuko ya plastiki iliyotengenezwa kwa petroli.
“Mifuko hiyo ya mihogo haiharibu mazingira kwani inaweza kuoza inapofukiwa ardhini, majini,” wanasema watafiti hao.
Iwapo mradi huo utafaulu, basi mihogo huenda ikawa na umuhimu mara mbili; kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uhifadhi wa mazingira.
Mihogo ni miongoni mwa mazao ambayo Wakenya wanashauriwa kulima ili kukabiliana na ukame wa mara kwa mara unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Mihogo inaweza kukuzwa katika maeneo yaliyo na kiwango kidogo cha mvua.
Shirika la Chakula Duniani (FAO) linakadiria kuwa ukuzaji wa mihogo utazidi kuongezeka kote duniani kama njia mojawapo ya kukabiliana na uhaba wa chakula haswa katika nchi maskini.
Shirika la FAO linasema kuwa mihogo ni miongoni mwa mimea michache ambayo itastahimili makali ya mabadiliko ya tabianchi kufikia 2030.
Mihogo pia huenda ikanusuru mifugo ambayo inakabiliwa na uhaba wa nyasi kutokana na ukame wa mara kwa mara.
Kulingana na FAO, ugali wa mihogo huleta nguvu nyingi mwilini kuliko viazi vitamu. Mihogo ina kiwango kidogo cha mafuta na protini. Majani ya mihogo ni mboga iliyo na vitamini K ambavyo ni muhimu katika kuimarisha mifupa.
Mihogo ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya madini ya zinki, magnesia na chuma.
Watafiti kote duniani wamekuwa wakiendeleza ubunifu kwa lengo la kutengeza mifuko isiyodhuru mazingira.
Wiki iliyopita, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sussex, Uingereza, Lucy Hughes, 24, alishinda tuzo ya James Dyson kwa kutengeza mfuko wa kubebea bidhaa kwa kutumia magamba ya samaki.
Waandalizi wa tuzo hizo walisema mfuko huo uliotengenezwa kwa magamba ya samaki ni mgumu na unaweza kutumiwa kufungia vyakula na kubebea bidhaa. Kadhalika, walisema kuwa mfuko huo unaweza kuoza ndani ya wiki sita ukitupwa ndani ya jaa la takataka.
Kikosi cha wanasayansi kutoka nchini Peru pia wako mbioni katika kutengeneza sahani iliyotengenezwa kwa majani ya mgomba.
Wanasayansi hao wanalenga kumaliza sahani za plastiki ambazo hutumiwa mara moja na kisha kutupwa.
Kulingana na wanasayansi hao, sahani zilizotengenezwa kwa majani ya mgomba wa ndizi zinaweza kuoza siku 60 baada ya kutupwa kenye jaa la takataka.
Sahani, vikombe, vijiko vya plastiki tunavyotumia sasa vinaweza kuchukua miaka 500 bila kuoza.