Makala

MAZINGIRA NA SAYANSI: Umuhimu wa nyuki kwa chakula na mazingira

October 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na LEONARD ONYANGO

KUNA uwezekano kwamba serikali inachangia katika kudorora kwa uzalishaji wa chakula nchini.

Hii inatokana na hatua yake ya kuendelea kuruhusu matumizi ya kemikali za kunyunyizia mimea ambazo tayari zimepigwa marufuku katika mataifa ya Ulaya.

Kemikali hizi zenye sumu zinaathiri wadudu na ndege ambao wanahusika pakubwa katika uzalishaji wa nafaka, matunda na mboga.

Miongoni mwa wadudu walioathiriwa zaidi ni nyuki na vipepeo ambao huchangia katika kuongeza uzalishaji wa mazao mashambani.

Dawa za kunyunyizia wadudu zilizo na kemikali za Thiamethoxam, Imidacloprid na Clothianidin zilipigwa marufuku mwaka jana barani Ulaya kutokana na kigezo kwamba zinadhuru wadudu wenye manufaa kama vile nyuki.

Kemikali hizo zilianza kuwekewa vikwazo na Muungano wa Ulaya (EU) mnamo 2013.

Uchunguzi uliofanywa na Mamlaka ya EU kuhusu Usalama wa Chakula (Efsa) ulibaini kuwa kemikali hizo zinadhuru nyuki wa mwituni na wale wa kutengeneza asali.

Katika mataifa ya EU, matumizi ya kemikali hizo yameruhusiwa ndani ya mahema ya kukuzia mimea, maarufu ‘greenhouse’ ambapo nyuki hawaingii.

Mataifa ya EU yalipiga marufuku kemikali hizo baada ya kushinikizwa na wanaharakati wa uhifadhi wa mazingira.

Ufaransa ambayo ni mwanachama wa EU mwishoni mwa mwaka 2018 ulipiga marufuku matumizi ya kemikali mbili zaidi; thiacloprid na acetamiprid.

Thiacloprid hutumiwa katika kuua wadudu kwenye maua humu nchini. Acetamiprid haitumiwi kwa wingi nchini Kenya.

Uchunguzi huo pia uligundua kwamba kemikali hizo ni hatari kwa wadudu wengine wenye manufaa katika uzalishaji wa mazao kama vile vipepeo na ndege.

Kemikali za imidacloprid na thiamethoxam, kwa mfano, zinatumiwa humu nchini kunyunyizia miti ya kahawa, maharagwe, mahindi, pamba, ngano, miche, tumbako na mboga. Clothianidin hutumika kunyunyizia mbegu haswa za ngano na mahindi.

Kulingana na Silke Bollmohr, mwanasayansi wa mazingira na Mkurugenzi wa shirika la EcoTrac Consulting, asilimia 28 ya zaidi ya aina 700 ya dawa zilizoidhinishwa na Bodi ya Kukabiliana na Wadudu Waharibuo Mazao (PCPB) zimesheheni kemikali zilizopigwa marufuku barani Ulaya.

“Wakulima wengi hunyunyuzia dawa mazao asubuhi au mchana wakati ambapo kuna nyuki, vipepeo na ndege. Mazao hutegemea pakubwa nyuki, ndege na vipepeo katika uzalishaji chakula,” anasema Bi Bollmohr.

“Utafiti uliofanywa mnamo 2013 ulionyesha kuwa idadi kubwa ya wakulima hawafuati maelekezo yaliyoandikwa katika dawa bali huitumia kiholela,” anaongezea.

Nyuki huchangia pakubwa katika uzalishaji wa nafaka na matunda kwani hubeba poleni kutoka mmea mmoja hadi mwingine.

“Kuuawa kwa wadudu kama vile nyuki kunasababisha kudorora kwa mavuno ya matunda na nafaka,” anaelezea.

“Kemikali hizo pia zinaathiri afya ya binadamu zinapoingia mwilini. Tafiti ambazo zimewahi kufanywa zinaonyesha kuwa asilimia 75 ya asali inayozalishwa kote duniani ina aina zaidi ya moja ya kemikali,” anasema.

Kulingana na mhadhiri wa ufugaji wa nyuki katika Chuo Kikuu cha Egerton, Stephen Kagio, idadi ya nyuki humu nchini imepungua kwa kiasi kikubwa.

Anasema kiasi cha asali inayozalishwa humu nchini imepungua hadi tani 15,000 kwa mwaka kutoka tani 25,000 miaka ya 1980.

Inasadikiwa kuwa kuna kati ya makundi milioni 1.5 na milioni 2 ya nyuki humu nchini japo hakuna takwimu halisi.

“Kupungua kwa kiasi cha asali inayozalishwa ni ithibati kwamba nyuki wamepungua nchini,” anasema Bw Kagio ambaye pia ni mwenyekiti wa Vuguvugu la Wafuga Nyuki nchini (APK).

Mbali na kemikali, Bw Kagio anasema kuwa makali ya mabadiliko ya hali ya tabianchi pia yamesababisha kupungua kwa nyuki nchini.

“Mabadiliko ya hali ya tabianchi husababisha ukame unaofanya mimea kukauka. Mimea inaponyauka nyuki hukosa chakula hivyo kuhamia maeneo mengineyo,” anasema.

Tishio

Umoja wa Mataifa (UN) unataja kemikali, mabadiliko ya hali ya tabianchi na uchafuaji wa hewa kuwa miongoni mwa mambo yanayotishia uwepo wa nyuki.

Kuna aina 20,000 za nyuki kote duniani na wote huathiriwa na kemikali.

Lakini Shirika la Chakula Duniani (FAO) linasema kuwa idadi ya nyuki inapungua kwa kasi ya kutia hofu.

“Asilimia 40 ya aina ya nyuki na vipepeo wako katika hatari ya kutoweka,” inasema ripoti ya FAO iliyotolewa Mei 2019.

Nyuki ‘hunusa’ kufahamu palipo na mimea. Hewa inapochafuliwa kwa gesi kutoka viwandani, magari au vumbi, hushindwa kupata maua ya mimea hivyo kuathiri mazao. Baadhi ya kemikali husababisha nyuki kushindwa kutambua mizinga yao.

Asilimia 75 ya matunda, nafaka au mboga hutegemea nyuki, ndege au vipepeo katika uzalishaji wake.

“Kenya ni miongoni mwa mataifa yanayokabiliwa na baa la njaa mara kwa mara hivyo haina budi kupiga marufuku kemikali hizo zinazohatarisha nyuki ambao ni muhimu katika uzalishaji wa chakula,” anasema Bollmohr.

UN inashauri watu kuwa na mazoea ya kupanda maua nyumbani haswa yale yaliyo na utomvu wa kuvutia nyuki kama njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa nyuki hawatoweki.

Umoja wa mataifa unapendekeza matumizi ya kemikali za kuua viwavi vinavyoharibu mimea wakati ambapo hakuna upepo, mapema asubuhi au usiku. Kwa kufanya hivyo utaepuka kuua nyuki pamoja na wadudu na ndege wenye manufaa katika uzalishaji wa mazao.