• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
MAZINGIRA NA SAYANSI: Vipodozi vyarembesha ila pia hatari kwa mazingira

MAZINGIRA NA SAYANSI: Vipodozi vyarembesha ila pia hatari kwa mazingira

Na LEONARD ONYANGO

IKIWA ungali unadhani kwamba kujipodoa ni kwa akina dada tu, basi hujatembea mijini.

Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la akina kaka wanaojipodoa.

Hiyo huenda ndiyo sababu ya sekta ya vipodozi kukua kwa kasi humu nchini.

Kaunti ya ya Nairobi, kwa mfano, hujipatia takribani Sh38 milioni kutokana na utoaji wa leseni kwa biashara za vipodozi na vinyozi kila mwaka.

Takwimu za serikali ya Kaunti ya Nairobi zinaonyesha kuwa kuna zaidi ya maduka ya 3,700 ya vipodozi na vinyozi jijini.

Kulingana na data za Shirika la Takwimu nchini (KNBS), kiwango cha vipodozi vinavyoingizwa humu nchini kiliongezeka kwa asilimia 95 kati ya 2010 na 2018.

Shirika la kutafiti masoko la Euromonitor International linakadiria kuwa thamani ya sekta ya vipodozi nchini Kenya ni Sh12 bilioni.

Kilo milioni 15 za vipodozi ziliingizwa humu nchini, kulingana na Mamlaka ya Kukusanya Ushuru nchini (KRA).

Aliyekuwa waziri wa Fedha Henry Rotich aliongeza kodi ya vipodozi katika bajeti yake ya 2016/2017 kwa asilimia 10 baada ya kubaini kwamba sekta ya urembo inakua kwa kasi.

Licha ya kutoa nafasi za ajira kwa maelfu ya Wakenya, wanaharakati wa kutetea uhifadhi wa mazingira sasa wanashutumu sekta ya vipodozi kwa kurejesha nyuma juhudi za kukabiliana na uchafu wa plastiki.

Je, Chupa za plastiki au mikebe ya kubebea kemikali hizo hupelekwa wapi? Uchafu huo hujipata baharini na kwenye maziwa hivyo kudhuru samaki na viumbe wengine wa majini.

Vipodozi zaidi ya bilioni 120 hutengenezwa kila mwaka ulimwenguni. Wanaharakati wa mazingira wanasema kuwa mikebe na chupa za kubebea vipodozi hivyo ni za plastiki. Kwa kawaida chupa hizo huwa ndogo sana kiasi kwamba haziwezi kutumiwa tena na badala yake hutupwa.

Watafiti wanakadiria kuwa zaidi ya tani 8.3 bilioni za plastiki zimetengenezwa tangu miaka ya 1950 na asilimia 60 zimeishia kwenye vyanzo vya maji kama vile baharini, maziwa na mito.

Umoja wa Mataifa (UN) unatabiri kuwa endapo mifuko, chupa, vijiko, sahani za plastiki hazitapigwa marufuku kufikia 2050, bahari na maziwa yatakuwa na kiasi kikubwa cha plastiki kuliko samaki.

Utafiti uliofanywa nchini Uswizi ulibaini kuwa kiwango cha gesi ya kaboni inayochafua anga kitaweza kupungua pakubwa iwapo watu watatumia vifaa vya plastiki vinavyoweza kutumika zaidi ya mara moja.

Mbali na chupa za plastiki, baadhi ya vipodozi vimetengenezwa kwa chembechembe za plastiki ambazo ni hatari kwa mazingira.

Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (UNEP) mnamo 2015 lilitoa ripoti iliyofichua kuwa baadhi ya vipodozi pia vimesheheni chembechembe za plastiki ambazo ni hatari kwa mazingira.

“Chembechembe za plastiki na viungo vinginevyo vya plastiki vimekolea katika dawa za kusugua meno, sabuni ya majimaji ya kuogea na hata rangi ya kucha,” inasema ripoti hiyo.

“Kiwango cha chembechembe za plastiki kinategemea aina ya kipodozi. Baadhi ya vipodozi vina asilimia 90 ya chembechembe za plastiki na vingine vina asilimia 1,” ikaongezea ripoti hiyo.

Kuishia baharini

Kulingana na UNEP, chembechembe hizo za plastiki hujipata baharini au ndani ya maziwa ambapo hurundikana kwa miaka mingi.

Kuongezeka kwa watu wanaohitaji vipodozi kumesabisha wafanyabiashara walaghai, kuleta bidhaa feki, haswa kutoka nchini China.

Mkurugenzi wa Utekelezaji wa Sheria wa Mamlaka ya Kukabiliana na Bidhaa Ghushi (ACA) Johnson Adera anasema kuwa tayari wameanza harakati za kutambua vipodozi feki.

Anasema ACA tayari imepeleka sampuli za vipodozi vinavyosadikika kuwa feki kwa Shirika la Kutathmini Ubora wa Bidhaa (Kebs) ili kufanyiwa uchunguzi. Kufikia sasa mamlaka hiyo haijapata majibu.

Mamlaka ya ACA mapema mwaka huu ilinasa vipodozi feki vya thamani ya Sh1.5 milioni katika duka moja mtaani Karen. Mbali na kuwa hatari kwa afya ya watumiaji, vipodozi hivyo feki pia ni hatari kwa mazingira.

Kenya ilipiga marufuku utengenezaji, uuzaji na utumiaji wa mifuko ya plastiki miaka mwili iliyopita.

Mapema mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta pia alipiga marufuku matumizi ya vifaa vya plastiki vinavyotumiwa mara moja na kutupwa, karibu na fuko za bahari, misitu na hifadhi za wanyama. Rais Kenyatta alisema marufuku hiyo itaanza kutekelezwa Juni 5, 2020.

You can share this post!

TEKNOHAMA: Simu haiathiri mtoto tumboni

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nini husababisha masikio kuziba?

adminleo