Makala

Mbappe kula githeri miaka sita jela akipatikana na hatia ya ubakaji

Na GEOFFREY ANENE October 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MVAMIZI matata wa Real Madrid na Ufaransa, Kylian Mbappe anakabiliwa na kifungo cha miaka sita jela chini ya sheria za Uswidi iwapo atapatikana na hatia ya kubaka, ripoti nchini Uswidi zinasema.

Kwa mujibu wa ripoti nchini humo, mwanamke mmoja alienda katika kituo cha polisi mjini Stockholm juma hili akidai kubakwa na mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 25.

Vyombo kadhaa vya habari nchini Uswidi ikiwemo runinga ya taifa SVT, ambayo inadai kupata stakabadhi muhimu, na gazeti la Expressen, vimeripoti kuwa Mbappe anatuhumiwa kubaka baada ya kutembelea kilabu kimoja cha usiku na kulala katika hoteli moja mjini Stockholm mnamo Oktoba 10, 2024.

Kwa mujibu wa maafisa wa polisi wa Uswidi, “kuna matukio fulani ya kiwango fulani yanayoonyesha kuwa mtuhumiwa alifanya kitendo hicho”.

Mwendesha mashtaka wa serikali ya Uswidi alitangaza Jumanne kuwa ripoti ya jinai imewasilishwa kwa polisi kufuatia ripoti kwenye vyombo vya habari kuhusu dai la kubakaji mjini Stockholm.

Mbappe alijiunga na Real Madrid msimu huu bila ada ya uhamisho baada ya kandarasi yake na Paris Saint-Germain kutamatika.

Ripoti zinadai kuwa tayari Real wanajutia kusaini Mfaransa huyo ambaye amefunga mabao saba katika mechi 11 amewachezea. Mbappe alianza kukuza talanta yake katika academia ya AS Bondy kabla ya kuvutia timu nyingi kubwa kwa ustadi wake akiwa kambini mwa AS Monaco kati ya 2015 na 2018.

Klabu hiyo ilimpeleka PSG kwa mkopo msimu 2017-2018 ambapo aliridhisha kiasi cha kusajiliwa kwa Yuro 180 milioni. Ada hiyo ilifanya Mbappe kuwa tineja ghali kabisa katika soka na mchezaji wa pili ghali nyuma tu ya mchezaji mwenza Neymar.

Mbappe anatoka katika familia ya wanamichezo. Baba yake Wilfried Mbappe, ambaye alihamia Ufaransa kutoka Cameroon, alikuwa mwanasoka na pia kocha. Mama yake Fayza Lamari, ambaye ana asili ya Algeria, alicheza handiboli. Ndugu ya Kylian, Ethan Mbappe ni kiungo wa Lille inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa.

Kylian Mbappe si mwanasoka wa kwanza tajika kukabiliwa na madai ya dhuluma za kingono.

Kuna orodha ndefu inayojumuisha wanasoka waliowahi kukabiliwa na madai kama hayo wakiwemo masupastaa Cristiano Ronaldo (Ureno), Neymar, Robinho, Dani Alves (Brazil), Adam Johnson, Mason Greenwood, Ched Evans, Callum Hudson-Odoi (Uingereza), Thomas Partey (Ghana), Benjamin Mendy, Franck Ribery, Karim Benzema (Ufaransa) na Gylfi Sigurdsson (Iceland).