Makala

MIMICA: Mshirika muhimu zaidi kwa Afrika ni bara Uropa

May 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na NEVEN MIMICA

UPEPO wa mabadiliko unavuma barani Afrika, kuanzia kwenye mikataba ya kihistoria ya amani, kikomo cha tawala za kidikteta, hadi azimio la soko huru barani. Afrika ni bara linaloinuka!

Kasi ya mwendo wa uchumi wa bara hili imeongezeka na sasa Afrika ndilo bara la pili kwa kasi ya ukuaji duniani na fursa mpya za kibiashara zimeongezeka huku uwekezaji ukipanda kwa haraka.

Katika kipindi cha zaidi ya mika mitano, nimeshuhudia mabadiliko haya nikiwa katika wadhifa wa Kamishna wa Tume ya Ulaya ya Ushirikiano na Ukuaji wa Kimataifa.

Nimeona kwa macho yangu jinsi Afrika imeimarisha nafasi yake katika jukwaa la kimataifa kwa kujiamini na kufahamu uwezo wake wa kiuchumi, kimazingira na rasilimali za watu.

Mchakato wa kufanikisha Dira ya Afrika ya 2063 unaweza kuwa mrefu na unaohitaji wahusika wote kujitolea, katika kila ngazi na nyanja zote. Vizuizi vinaweza kujitokeza na vitakuwepo.

Jambo moja la uhakika ni kuwa Ulaya ni mshirika wa muda mrefu wa Afrika na nia yetu ni kuendeleza ushirikiano huu. Afrika ni pacha wa bara la Ulaya na ndiye mshirika mkuu wa Afrika katika biashara na mwekezaji wake mkuu.

Ni imani yetu kubwa kwamba Afrika yenye nguvu ni neema kwa Ulaya na tutapata ushindi tu kwa kuimarisha jirani zetu.

Nia yetu ni kushirikishana kwenye hatari zote na kwa pamoja kukuza uwezo wa Afrika kufikia maendeleo ambayo yatadumu na kuzalisha fursa za muda mrefu kwa wote. Hii ni aina ya maendeleo ambayo yatatoa fursa mpya za kibiashara kwa Waafrika na watu wa Ulaya.

Ninatambua kwamba ushirikiano wa Afrika na Ulaya umekua na kukomaa katika miaka iliyopita. Umepitia mageuzi kutoka kuwa uhusiano kati ya mfadhili-na-mfadhiliwa, hadi kufikia ushirikiano wa pande mbili zinazotoshana na sasa unaakisi “Muungano”, aliyouzungumzia Rais Juncker alipofanya uzinduzi mpya wa Muungano wa Afrika na Ulaya kwa Uwekezaji Endelevu na Ajira.

Muungano huu utaleta matokeo thabiti kwa walengwa na uwekezaji wetu utasaidia kupatikana kwa ajira milioni 10 barani Afrika katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Kwa pamoja, Afrika na Ulaya zinaweza kuendesha ajenda ya kimataifa. Pamoja, tunaweza kuleta mabadiliko. Kama Ulaya itapoteza nafasi hii ya ushirikiano na Afrika, itapoteza nafasi yake katika historia.

Kiwango tutakachofanikisha Muungano huu kitategemea jinsi tutakavyofanikisha mipango hii na kuleta mabadiliko ya kweli na ya kudumu kwa walengwa wote.

Kufanikisha haya kutazihitaji Afrika na Ulaya zenye msimamo thabiti. Ninajua kwamba sote tuna uwezo wa kujitolea kikamilifu. Hata hivyo hatuna muda wa kupoteza: 2063 ni sasa.

Neven Mimica ni Kamishna wa Tume ya Ushirikiano na Maendeleo, Muungano wa Ulaya (EU)