Mjane anavyovuna hela kwa kusindika viazi asilia
MONICA Makokha alipopoteza mumewe 1994, hakujua mkondo ambao maisha yake yangechukua.
Kipenzi wake wa roho alipofariki, alimuacha akiwa na umri wa miaka 26 na watoto watano.
Licha ya upweke uliomkodolea macho, hakuwa na jingine ila kujituma kutafutia familia yake riziki.
“Mume wangu alikuwa akifanya kazi katika sekta ya umma, na pia alikuwa mkulima. Niliamua kufanya kilimo kuwa afisi yangu kutafutia wanangu unga,” Monica anasema.
Alianza mdogo mdogo, na sasa ni kati ya wakulima tajika katika Kaunti ya Kakamega.

Shamba lake la ekari 11 lililoko wadi ya Itenje, Kaunti Ndogo ya Mumias Magharibi ni uga wa mseto wa mimea.
Akiwa na tajiriba ya zaidi ya miaka 30 kwenye kilimo, amekuwa mtaalamu wa kukuza mimea asilia, akifuata nyayo za mume wake.
Sehemu ya shamba lake, limesheheni viazi vikuu. “Hulima viazi vitamu vya rangi tofauti na mihogo,” anadokeza.
Monica vilevile hukuza mboga za kienyeji kama vile managu, terere, kunde na sagaa.
Mboga zingine ni sukuma wiki, spinachi, na pia hulima matunda kama vile ndizi, matunda damu na avokado.
“Shambani mwangu hutakosa maharagwe aina ya njahi na mucuna, ambayo ni muhimu sana kurejesha na kudumisha hadhi ya udongo,” anasema.

Maharagwe hayo asilia yana virutubisho vya Nitrojini.
Ni mfugaji wa ng’ombe, kuku akiwa na zaidi ya 150 na sungura 25, mifugo ambao humpa mbolea kuendeleza kilimo na kupunguza gharama.
Kinachotofautisha Monica na wakulima wengine, ni mtandao wa uongezaji thamani anaoshiriki.
Hukausha viazi na kuvisaga kuwa unga, na pia matunda, hatua inayomuwezesha kuteka soko lenye ushindani mkuu.
“Kuuza mazao mabichi ya shambani si rahisi, hasa yanapofurika sokoni,” anasema.
Jitihada za Monica zimetambuliwa na Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa, ambaye aliwahi kumpiga jeki kwa pembejeo.
Mama huyu hodari katika shughuli za kilimo ana sola na kituo cha kukausha bidhaa, na mashine ya kusaga – kisiagi.

Alianza uongezaji thamani mwaka 2019, baada ya kukumbana na changamoto za kusaka soko na kuhangaishwa na mabroka.
“Nilikuwa nikikadiria hasara hasa wanunuzi wanapokosekana ikizingatiwa kuwa mazao ninayozalisha huharibika upesi,” anaelezea.
Kulingana na data za Wizara ya Kilimo, wakulima nchini hupoteza zaidi ya asilimia 30 haswa msimu wa mavuno na baada, kutokana na ukosefu wa miundomsingi faafu kuyahifadhi.
Baada ya kuvuna mihogo na viazi vitamu vya rangi, huvikausha na kuvisaga kuwa unga.
“Huchanganya unga huo na ule wa mahindi, na ni bora kupika uji na ugali, kwa sababu ya kusheheni virutubisho,” anafafanua.
Kwa kusindika mazao yake, huongeza mara dufu kiwango cha mapato, mfano ukiwa kipakio cha kilo mbili ambacho angeuza Sh100 huwa Sh200.
Hali kadhalika, anapokausha mboga bei huwa mara dufu. “Kilo moja ya mboga huuza Sh25, na zinapokaushwa huwa zaidi ya Sh50,” anaongeza kueleza.

Wateja wake, wanatoka masoko mbalimbali Kakamega.
Kuhakikisha ana mazao mfululizo, Monica amekumbatia teknolojia za kisasa kunyunyizia mimea na mashamba maji kwa kutumia mifereji.
Ana sola kumpa nguvu za kawi kupampu maji kutoka kwenye kisima.
Kando na mfumo wa kunyunyizia mimea maji kwa mifereji, pia amekumbatia upandaji mseto wa mimea shambani teknolojia inayojulikana kama intercropping, na pia hukuza miti yenye thamani, kudhibiti ulimaji shamba kwa trekta na matumizi ya nyasi za mtandazo, boji.
Ni teknolojia asilia ambazo SNV Netherlands Development Organisation, shirika lisilo la Kiserikali kutoka Netherlands linahamasisha wakulima kukumbatia.

Monica ni mmoja wa wakulima walionufaika kupitia shirika hilo, baada ya kukutana nalo 2019.
Aidha, lina programu kadha wa kadha nchini jinsi ya kuzalisha chakula hasa katika kipindi hiki athari za mabadiliko ya tabianchi zinatesa wakulima.
Huhamasisha teknolojia za kufufua hadhi ya udongo na mashamba, zinazojulikana kama Regenerative Agriculture Technologies kwa Kiingereza.
SNV hulenga sana wakulima hususan kina mama na vijana walio kwenye makundi.
Monica Makokha ni mwanachama wa Itenje Kilimo Biashara Farmers’ Cooperative Society, chama cha ushirika kilichoanza kama kundi la watu 10 na sasa kina zaidi ya wanachama 100.
Wanachama hao wanajishirikisha katika kilimo cha viazi vikuu, mboga, ufugaji wa kuku, ng’ombe, mbuzi na hata nyuki.
