Mkigusa bajeti ya Elimu tutakosana, Knut na Kuppet waambia Serikali
VYAMA vya kutetea walimu nchini vimeutaka utawala wa Rais William Ruto kuhakikisha kuwa mgao wa bajeti uliotengewa sekta ya elimu unadumishwa serikali inapopunguza fedha zilizotengewa sekta mbalimbali.
Chama cha kutetea masilahi ya walimu wa shule za upili (Kuppet) na kile cha kutetea masilahi ya walimu wa shule za msingi (Knut) zilisema kuwa Sh35 bilioni zilizotengewa uajiri wa walimu 46,000 wa vibarua, nyongeza ya mishahara na kupandishwa vyeo kwa walimu hazifai kupunguzwa.
Mwenyekiti wa Kitaifa wa Kuppet Omboko Milemba na Katibu Mkuu wa Knut Collins Oyuu pia wamewataka wabunge kudumisha ugao huo.
Viongozi hao wawili pia wameitaka serikali kuwaajiri walimu wengine 20,000 ili kupunguza athari za uhaba wa walimu katika shule za umma
“Msimamo wetu ni kwamba Sh18.5 bilioni za kuwapa ajira ya kudumu walimu 46,000 wa vibarua, Sh13.3 bilioni za kufadhili awamu ya pili ya nyongeza ya mishahara na Sh2.5 bilioni za kuwapandisha vyeo walimu zisiguswe,” akasema Bw Milemba.
Alisema hayo katika kijiji cha Ndarawetta, eneo bunge la Bomet ya Kati wakati wa mazishi ya Raeli Chepkorir Chepkwony, mamake Naibu Mweka Hazina wa kitaifa wa Kuppet Ronald Tonui.
Bw Tonui pia aliwahi kuhudumu kama mbunge wa eneo bunge hilo.
Naibu Katibu Mkuu wa Kuppet alionya kuwa huenda walimu wakagoma ikiwa matakwa yao hayatatimizwa.
“Endapo masuala ambayo tumeangazia hayatashughulikiwa walimu watapambana vikali na serikali, mambo hayatakuwa shwari,” akasema akiongeza kuwa mgao wa bajeti katika sekta ya elimu haupasi kuathiriwa na kuzimwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024.
Kwa upande wake, Bw Oyuu kwenye taarifa aliyoitoa Ijumaa alikariri msimamo sawa na wa viongozi wa Kuppet.
Aliitaka Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na Kamati ya Bunge kuhusu Elimu inayoongozwa na Mbunge wa Tinderet Julius Melly kuhakikisha bajeti ya sekta ya elimu haipunguzwi kuzuia misukosuko katika sekta hiyo.