Akili MaliMakala

Mtambo wa kisasa kuchoma maharagwe ya kahawa

Na SAMMY WAWERU March 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KWA muda mrefu waongezaji kahawa thamani wamekuwa wakitumia mashine za kitambo kuchoma au kukaanga maharagwe ya kahawa.

Ni mojawapo ya hatua za kutamatisha ili kahawa kuwa tayari kugeuzwa kuwa kinywaji.

Hata hivyo, mashine za zamani zimeanza kupitwa na wakati za kisasa zikitawala sekta ya kilimo kufuatia kujiri kwa teknolojia na bunifu za kileo.

Kampuni ya Linkage Africa, inaunganisha, kutengeneza na kusambaza mtambo wa kisasa kuchoma kahawa – unaorahisisha huduma.

Sehemu ambayo mbegu za kahawa huwekwa ili kukaangwa. PICHA|SAMMY WAWERU

Kampuni hii yenye afisi zake Jijini Nairobi, ilitumia jukwaa la Maonyesho ya Kahawa mwaka huu, 2025, yaliyofanyika katika Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (CRI) inayohudumu chini ya Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (KALRO).

Yakiwa na kaulimbiu ‘Kuendeleza ubunifu wa kilimo kwa mifumo ya chakula yenye ustahimilivu na maisha endelevu,’ Linkage Africa ilihamasisha wakulima wa kahawa kuhusu modern coffee roaster machine.

Josphat Kyalo kutoka Linkage Africa akielezea jinsi mtambo wa kisasa kuchoma kahawa hufanya kazi. PICHA|SAMMY WAWERU

Ni mashine ya kisasa kukaanga kahawa, ambayo, kulingana na Josphat Kyalo kutoka Linkage Africa, ni mtambo ulioundwa kwa matumizi ya kibiashara.

“Mashine hii ya kukaanga kahawa ya kibiashara ina mfumo wa kompyuta na huonyesha kiwango cha unyevuunyevu na joto la maharagwe ya kahawa,” Kyalo alieleza huku akionyesha jinsi mashine hiyo inavyofanya kazi.

Kukaanga au kuchoma, alisema mtambo huo unazalisha kilo 90 kwa kila saa.

Modern coffee roaster ni mtambo wa kisasa wenye kompyuta kuchoma kahawa. PICHA|SAMMY WAWERU

“Hata hivyo, inaweza kurekebishwa ili kuzalisha zaidi,” Kyalo alisema.

Bei, inagharimu kima cha Sh2.6 milioni.

Maonyesho hayo ya kahawa ambayo yalikuwa Makala ya 19 yalifanyika katika makao makuu ya CRI, Ruiru, Kaunti ya Kiambu na yalileta pamoja wakulima kutoka maeneo yanayozalisha kahawa nchini, wadau kama vile kampuni za pembejeo, watafiti, wataalamu, wasindikaji, wauzaji, wasambazaji, na taasisi za kifedha.

Josphat Kyalo akionyesha batoni za kazi za mtambo wa kisasa kukaanga kahawa. PICHA|SAMMY WAWERU