Jamvi La SiasaMakala

Muturi aanika Ruto, adai ni mfisadi mkubwa 

Na CHARLES WASONGA April 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

ALIYEKUWA Waziri wa Utumishi wa Utumishi wa Umma Justin Muturi ametaja Rais William Ruto kama mtu ambaye hafai kuliongoza taifa la Kenya huku akiendelea kuanika maovu ya utawala wake wa miaka miwili na nusu.

Alisema Dkt Ruto haheshimu taasisi za uongozi na ni kiongozi mfisadi ambaye hulenga kujitajirisha kupitia miradi na mipango ya serikali.

“Ni jambo la kusikitisha kuwa taifa hili linaongozwa na Ruto kama Rais wake. Huyu ni mtu ambaye hastahili kuwa rais wa taifa la Kenya,” Bw Muturi akasema Ijumaa asubuhi, Aprili 4, 2025 kwenye mahojiano kwenye kipindi cha “Fixing the Nation”.

Bw Muturi alidai kuwa Rais Ruto ni kiongozi mwenye sura mbili; moja akionekana kama kiongozi mwadilifu machoni pa umma na nyingine ya mtu mwovu anayeendeleza sakata za ufisadi akiwa afisini.

“Ukimwona akiwaonya mawaziri wake kwamba hataki kusikia sakata za ufisadi utadhani ni asiyetaka kuvumilia uovu huo. Lakini uhalisia wa mambo ni yeye ni mfisadi mkubwa. Yeye ndiye alikuwa mhusika mkuu katika sakata ya Adani,” akaeleza.

Ili kuhimili madai yake, Muturi alidai kuwa wakati mmoja, akiwa Mwanasheria Mkuu, Rais Ruto aliwahi kujaribu kumshawishi atie saini stakabadhi kuhusu ruzuku ya Dola milioni moja (Sh129 milioni) kutoka kwa Wahisani kutoka Urusi kufadhili mpango wa serikali wa upanzi wa miti bilioni tatu kati ya bilioni 15.

Waziri huyo wa zamani alieleza kuwa alikataa kutia saini makubaliano hayo ili pesa hizo zielekezwe moja kwa moja kwa Wizara ya Mazingira badala ya Hazina ya Kitaifa, kulingana na sheria kuhusu usimamizi wa pesa za umma (PFM Act).

“Nilikuwa nimealikwa kwa mkutano wa mazingira, COP 28, jijini Dubai. Wakati huo wafadhili fulani kutoka Urusi walitaka kutoa ruzuku ya Dola milioni moja (Sh129 milioni) kwa Kenya.

“Nilipowasili Dubai, nilipokea simu kutoka kwa Ruto aliyeniambia raia fulani wa Urusi walikuwa wakinisubiri katika uwanja wa ndege wakitaka nitie saini stakabadhi fulani. Nilikataa, na kushikilia kuwa nilihitaji muda kuchanganua stakabadhi hizo afisini mwangu,” Bw Muturi alifichua.

Mwanasheria huyo Mkuu wa zamani alieleza kuwa Rais Ruto akianzisha mradi wowote, huwa analenga kuutumia kutengeneza pesa kwa manufaa yake.

Kuhusu sakata ya Adani, ambayo iliibua joto jingi nchini Kenya mwaka jana, 2024, Bw Muturi alidai kuwa Rais alihusika moja kwa moja.

Alisema alipokuwa Dubai, kuhudhuria mkutano wa COP28, mshauri wa Rais, Adan Mohamed alimpa maelezo yaliyomhusisha Ruto na mpango huo, haswa ule wa ukodishaji wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenya (JKIA).

“Ni yeye alikuwa mhusika mkuu katika sakata ya Adani kulingana na maelezo niliyopata kutoka kwa Adan Mohamed tukiwa naye Dubai,” Bw Muturi akasema.

Hatimaye, Novemba 2024 Rais Ruto alifutilia mbali mpango huo kwa ukodishaji wa JKIA kwa miaka 30 na mpango wa kuipa kampuni ya Adani kandarasi katika sekta ya kawi.

Hii ni baada ya mmiliki wa kampuni ya Gautam Adani kushtakiwa kwa ufisadi nchini Amerika.

Bw Muturi aliyefutwa kazi na Rais Ruto wiki jana, pia alimtaja kiongozi wa taifa kama Rais asiyeheshimu uhuru wa asasi za kikatiba kama Afisi ya Mwanasheria Mkuu na Idara ya Mahakama.

“Aidha, amewatia woga mawaziri kiasi kwamba ni nadra kwao kujadili waziwazi masuala yanayohusu wizara zao katika vikao vya mawaziri. Ama kwa hakika mawaziri wako huru katika vikao vya kamati ndogo zinazoongozwa na Naibu Rais kuliko walivyo mbele yake kwenye vikao vya baraza la mawaziri,” Bw Muturi akaeleza.

Spika huyo wa zamani wa Bunge la Kitaifa alifichua kuwa, kama Mwanasheria Mkuu hakuhusishwa katika utayarishaji wa miswada mitatu ya Sheria za Afya za kufanikisha mpango wa Afya Kwa Wote (UHC).

Bw Muturi alikariri kuwa hakufutwa kazi kutokana na utepetevu au uzembe bali ni kwa sababu aliikashifu serikali kuhusiana na suala la utekaji nyara.

Hata hivyo, aliungama kuwa awali hakutaka ateulie Mwanasheria Mkuu kwa sababu kazi hiyo “inahusu shughuli nyingine za kusoma.”

“Ruto alimtuma rafiki yangu Moses Wetang’ula anishawishi nikubali wadhifa huo. Baadaye nilimwambia Ruto kwamba nitakubali cheo hicho lakini ajue kwamba sitakubali kufanya chochote kinyume cha sheria na Katiba,” akasema.

Bw Muturi ameahidi kuandika kitabu ambacho kitaelezea kwa kina tajriba yake katika Idara ya Mahakama, Asasi ya Bunge na Serikali Kuu.