Mvutano kuhusu tohara wagawanya wazee Mlima Kenya
WAZEE wa jamii ya Agikuyu wametofautiana kuhusu umri bora kwa wavulana kutahiriw, baadhi wakisema unastahili kuwa miaka 12.
Wengine wanataka uwe miaka 14 huku wengine wakishikilia uwe miaka 16.
Upashaji tohara unaenziwa zaidi katika jamii hii na nyingine za eneo la Mlima Kenya, kwani huwawezesha wavulana kuruhusiwa kuoa na hatimaye kuingia kundi la wazee.
Tangu ujio wa elimu ya kisasa, wavulana waliokamilisha masomo ya shule ya msingi ndio walikuwa wakichukuliwa kama waliotimu umri wa kupashwa tohara.
Shughuli hiyo ilifanywa kwa njia ya kitamaduni pale wavulana walikuwa wakikabiliana na kisu cha ngariba alfajiri wakiwa kando ya mito.
Lakini siku hizi, wavulana hupelekwa hospitalini kutahiriwa, wakipewa dawa za kupunguza uchungu, baadhi yao wakiwa wameandamana na akina mama na dada zao.
Katika jamii ya Agikuyu na nyingine za Mlima Kenya, wavulana hutahiriwa mwezi wa Desemba.
Lakini wanaweza kutahiriwa katika miezi ya Aprili au Agosti, shule zikifungwa mwishoni mwa muhula.
Kulingana na mtaala wa sasa wa Umilisi na Utendaji (CBC), wavulana hujiunga na shule za sekondari msingi (gredi ya saba) wakiwa na umri wa angalau miaka 12.
Wanatakiwa kuendelea hadi gredi ya tisa ambapo umri wao utakuwa angalau miaka 16.
Hata hivyo, Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Upili (KESSHA) kinataka wanafunzi wa gredi ya nane na tisa wahamishwe hadi shule za upili zinazotambulika, hali ambayo inaelekea kusukuma umri wa upashaji tohara kuwa miaka 14.
Hii imesababisha mgawanyiko katika Baraza la Wazee wa Jamii ya Agikuyu (Kiama Kia Ma), huku mwenyekiti wake Thiong’o wa Gitau akisisitiza kuwa umri wa wavulana kutahiriwa uwe miaka 16.
Lakini mdhamini wa kitaifa wa baraza hilo, Kung’u Muigai, amejitokeza na kupinga msimamo wa Bw Gitau, akishikilia kuwa umri wa miaka 14 ndio unapaswa kuzingatiwa.
Kwa hivyo, Bw Gitau ametangaza kuwa hakutakuwa na shughuli ya kuwapasha tohara wavulana katika eneo la Mlima Kenya ilhali Bw Kung’u anashikilia kuwa itaendelea ilivyoratibiwa.
Upashaji tohara wavulana ni faida kubwa kwa ngariba, hospitali na makanisa ambayo hutoza kati ya Sh10, 000 hadi Sh50, 000 kulingana na uwezo wa kifedha wa familia.
Kulingana na Bw Kung’u, mabadiliko ya kila mara ya mtaala wa masomo yamevuruga umri wa kutahiriwa kwa wavulana “kwa hivyo tunapaswa kushikilia miaka 14 kama umri faafu kwa wavulana kupashwa tohara.”
Mgawanyiko miongoni mwa wazee wa jamii ya Agikuyu kuhusiana na suala hili umewakanganya wazazi wanaoamini kuwa wazee ndio wenye usemi mkubwa katika uwekaji mwaka wa tohara.