Mwalimu mstaafu anayeteka hela kama njugu kupitia kilimo cha avokado
BAADA ya kutembea kwa takriban kilomita 800 kutoka barabara ya Elburgon- Njoro, tulifika katika shamba la Bw Francis Kamau, mwalimu mstaafu eneo la Cheponde mjini Elburgon katika Kaunti ya Nakuru ambapo tulimpata pamoja na mkewe kwenye shamba lao ambapo wanakuza maparachichi ya Hass.
Kamau aliacha kilimo cha mahindi na kuanza kukuza maparachichi baada ya kugundua kuwa kilimo cha mahindi kilikuwa na kazi nyingi, uzalishaji mdogo na mauzo yaliyo na fedha chache.
Pia, asema kilimo cha mahindi kinatawaliwa na madalali wengi na mapato hayawezi kulinganishwa na yale ya maparachichi!
“Nilipanda vipande 22 vya miche ya miparachichi ya Hass mwaka wa 2017, baadhi nikinunua kutoka kwa Idara ya Kilimo na nyingine kutoka kwa mkulima wa eneo hilo ambaye alikuwa ameipanda kwenye kitalu chake. Nilichimba mashimo ya futi 2 kwa 2 na kutenganisha miche yangu kwa upana wa mita 6 kwa 6,” asema Kamau, ambaye alikuwa mwalimu wa shule ya msingi.
Kisha alichanganya mbolea na udongo wa juu na baada ya mwezi mmoja, alimwagilia miche yake maji ya mvua, kila asubuhi na jioni.
Kwa kuwa eneo hilo lina changamoto ya maji, aliweka matandazo kati ya zao la parachichi kwa kutumia nyasi kavu na mashina makavu ya mahindi ili kuhifadhi na kuzuia uvukizi wa maji.
Baada ya mwaka mmoja, baadhi ya miche yake ilivamiwa na fuko ambapo alitumia mitego kuidhibiti ila akabadilisha miche iliyoathiriwa.
Kwa bahati nzuri, asema hakuna wadudu waliovamia mazao yake lakini aliendelea kumwagilia mazao yake maji wakati mvua ilipopungua.
Mwaka wa 2020 alipata mavuno yake ya kwanza.
“Niliuza matunda yangu kwenye soko la humu nchini kupitia kwa madalali kwani hakukuwa na soko tayari. Uzalishaji haukufaa ikilinganishwa na mwaka uliofuata. Uzalishaji huongezeka kwa muda na taratibu matawi yanayozalisha matunda yakiongezeka,” alisema Kamau.
Kamau asema matunda hayo yaliongezeka katika mwaka wake wa pili wa mavuno na tangu wakulima wengine katika eneo hilo waanze ukulima wa maparachichi, waliunda kikundi na kuwa na kandarasi na kampuni ya Keitt Exporters – ya usindikaji wa matunda na mboga ambako wanauza matunda yao hadi kwa sasa.
Anasema kampuni hiyo imemsaidia yeye na wakulima wengine katika eneo kwani hawauzi matunda yao kwa wafanyabiashara wa kati.
Kwa sasa, matunda yake huyauza kwa kati ya Sh15 na Sh 20 kila moja kulingana na ukubwa na ubora wake. Baada ya kampuni kununua matunda, mabaki hutumiwa kwa matumizi ya nyumbani.
Mkulima huyu afichua kuwa alijitosa katika kilimo cha maparachichi baada ya kujua kuwa muda wake wa kustaafu ulikuwa ukikaribia.
Alichagua maparachichi aina ya Hass kwa vile yana soko bora ikilinganishwa na aina nyingine za maparachichi.
Anaongeza kwamba matunda yanaweza kukaa muda mrefu baada ya kuchumwa ikilinganishwa na mazao mengine.
“Katika siku zijazo, ninapanga kupanua sehemu yangu ya ardhi hadi ekari moja, kuongeza matangi zaidi ya maji ili kuteka maji ya kutosha wakati wa mvua na pia kununua jenereta ya kuvuta maji kutoka kwa mto ulio karibu hadi shambani wakati wa kiangazi,” asema Kamau ambaye ametoa wito kwa wakulima wengine kujitosa katika kilimo cha maparachichi.
Akizungumza wakati wa mahojiano hivi majuzi, mwalimu huyo mstaafu asema katika shamba lake, amekuza mazao ya mikunde kama maharage na mbaazi katikati ya matunda yake kwani huongeza naitrojeni ambayo ni muhimu kwa ukuaji wa maparachichi.
Yeye pia hupanda viazi vitamu kama zao la ziada.
Mwaka 2022, uzalishaji ulikuwa mzuri ambapo anasema ulichangiwa na mvua ya kutosha.
“Kutokana na miti kati ya 17 na 22 ya maparachichi, nilipata zaidi ya Sh100, 000 kwa mauzo, ambayo ilikuwa ya juu zaidi kuwahi pata tangu nianze ukulima wa matunda hayo. Kiasi hiki kilikuwa zaidi ya kile nilichopata kutoka kwa kilimo cha mahindi kwani wakati wa msimu mzuri, nilikuwa nikiweka mfukoni kati ya Sh 30, 000 na Sh 40, 000 kutoka kwa mauzo ya mahindi kavu kwa mwaka,” alisema na kuongeza kuwa mkulima anaweza kuvuna maparachichi mara mbili kwa mwaka kulingana na msimu.
Kila mti wa parachichi unaweza toa matunda kati ya 500 na 600 huku idadi hii ikiongezeka hadi matunda 1,000 kadri yanavyoendelea kukua.
Sasa anawataka wakulima kutumia samadi na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu ili kuwa na kilimo endelevu.
Mkulima huyu ambaye huhudhuria semina na vikao vingine vya siku ya shambani, pia amepata ujuzi kutoka kwa wataalamu wa kilimo na maafisa wa nyanjani wanaotembelea mashamba yao.
Alitoa wito kwa wakulima kuunda vikundi kwani vitawasaidia kupata masoko bora badala ya kutafuta kama mtu binafsi.
Alitoa wito kwa serikali ya kitaifa na kaunti kutoa mafunzo na warsha kwa wakulima ili kuwaelimisha kuhusu mbinu bora za kilimo, tiba, wadudu na udhibiti wa magonjwa.
Mkewe, Mary Maina, 60, ambaye alisema kilimo cha maparachichi hunawiri panapokuwa na maji ya kutosha, alibainisha kuwa kilimo hiki kimewasaidia kusomesha watoto wao na kukidhi mahitaji mengine ya nyumbani.
Afisa wa Kilimo wa Kaunti Ndogo ya Molo, Emma Mwangi alitoa wito kwa wakulima kuwasiliana na maafisa wa nyanjani au kutembelea afisi zao ili kupata taarifa sahihi kuhusu kudhibiti wadudu na magonjwa.
“Tunatoa wito kwa wakulima watutembelee na kupata ujuzi kuhusu mifumo sahihi ya kilimo, udhibiti wa wadudu na magonjwa miongoni mwa taarifa nyingine muhimu zitakazowawezesha kupata uzalishaji maradufu,” alisema Mwangi.