Mwanafunzi wa zamani Alliance ashinda tuzo ya kimataifa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
MWANAFUNZI wa zamani wa Shule ya Upili ya Alliance ameshinda tuzo ya kimataifa inayotambua juhudi na mikakati kuangazia mabadiliko ya tabianchi, inayotolewa na shirika la kimataifa linaloangazia utetezi wa tabianchi.
Alexander Nyang’iti, 19, aliyehitimu KCSE 2024, aliibuka kidedea miongoni mwa wanafunzi na shule 13 kutoka maeneo mbalimbali Kenya walioshiriki shindano la ubunifu wa tabianchi la Climate Advocates Voces Unidas (CAVU) Climate Innovation Challenge (CIC) mwaka wa 2024/2025.
Mashindano hayo ya kila mwaka yanashirikisha vijana na wanafunzi wanaobuni suluhisho za kipekee kuangazia athari za tabianchi, kwa kutumia mbinu za kisasa za uandishi na utunzi wa hadithi.

Nyang’iti, ambaye alipata alama ya A-, alituzwa Dola (USD) 1,500 (sawa na Ksh193,800) kupitia mradi wa hadithi ya video kuhusu juhudi za upanzi wa miti katika Shule ya Alliance, maarufu kama ForestNukes.
Wazo la ForestNukes lilionyesha mbinu tatu za upanzi wa miti — mbegu zilizofunikwa kwa vumbi la makaa (seed balls), mbinu ya Miyawaki, na teknolojia ya ForestNukes yenyewe.
“Ukijumuisha Seed balls na Miyawaki, jawabu linakuwa ForestNukes. Tumekusanya mbinu hizi mbili na kuzifanya ziwe moja ili iwe rahisi, ya gharama nafuu na inayoweza kutekelezwa na jamii kwa njia rahisi. Lengo ni kuunda misitu asilia kwa kutumia miti ya kienyeji,” alisema Nyang’iti kwenye mahojiano ya kipekee na Akilimali.

Barobaro huyo alitangazwa mshindi wa jumla katika hafla iliyofanyika jijini Nairobi, Juni 7, 2025.
Seed balls ni mbegu zinazofunikwa kwa vumbi la makaa ili kulinda mbegu dhidi ya wadudu na mazingira mabovu, kisha zinapandwa moja kwa moja ardhini, na baada ya miaka michache, miche inastawi kuwa mti.
“Hii ni mbinu ya gharama nafuu, inayohitaji kazi kidogo, ni rahisi kusambaza, haiharibu udongo na inafaa kwa upanzi wa miti mingi,” Nyang’iti, ambaye anapanga kusomea Kozi ya Uhandisi wa Umeme, akilenga kuzamia nishati faafu kwa mazingira, anaelezea.
Mbinu ya Miyawaki nayo, iliyoanzishwa na mtaalamu wa mimea kutoka Japan, Akira Miyawaki, inahusisha kupanda miti ya kienyeji kwa kuikaribisha sana ili kuunda mazingira ya msitu asili.

Mbegu hupandwa kwa makundi ya miti mitatu hadi mitano kila mita mraba, na hufuatiliwa kwa miaka miwili.
Kulingana na Nyang’iti, mbinu hii huchochea miti kukua kwa kasi – mara kumi zaidi ikilinganishwa na upanzi wa kawaida, kwa sababu miti hushindana kupata miale ya jua.
Katika video yake ya dakika 3 na sekunde 56 aliyoitengeneza kwa kutumia picha na video alizopakua kutoka Google, Nyang’iti anaeleza kusikitishwa na jinsi watu hukata miti bilioni 15.3 kila mwaka duniani, sawa na shashi (karatasi za chooni) 3,000 kila mtu ulimwenguni.
“Tunahitaji suluhisho ambalo kila jamii nchini na duniani inaweza kutumia kwa urahisi. ForestNukes ndiyo suluhisho bora,” anasema kwa sauti tulivu, huku muziki wa kupendeza ukiambatana na video hiyo.

Akiangazia changamoto za kampeni nyingi za upanzi wa miti, anahoji zimekuwa zikikwama kwa sababu ya mbinu duni za utekelezaji, ukosefu wa ushirikiano miongoni mwa jamii na muda mrefu miti kuchukua kustawi.
Serikali ya Kenya inalenga kupanda miti bilioni 15 kufikia mwaka wa 2032, japo changamoto kufanikisha miti hiyo kuwa misitu ni tele.
Clement Kipkemoi, mwalimu wa Alliance High, kwenye mahojiano alisema shule hiyo imejitolea kuhakikisha wanafunzi wanaelewa madhumuni ya kuhifadhi mazingira na kuangazia tabianchi.

“Tumefurahia ushindi huu mkubwa. Kwa miaka saba iliyopita, tumekuwa tukielimisha wanafunzi kuhusu mabadiliko ya tabianchi na uhifadhi wa mazingira,” alisema Kipkemoi, ambaye alikuwa patroni wa mradi wa ForestNukes.
Mkurugenzi wa CAVU Afrika, Teddy Warria, naye alisisitiza umuhimu wa kuhusisha vijana kwenye kampeni za uhifadhi wa mazingira.
CAVU ni shirika kutoka Amerika linalofanya kazi nchini humo na Barani Afrika, likihamasisha vijana kupitia uandishi na ubunifu kuangazia mabadiliko ya tabianchi.
Kilimo ni mojawapo ya sekta zinazoendelea kulemewa na athari za tabianchi, hasa kiangazi, ukame, mafuriko na mkurupuko wa wadudu.
