Makala

MWANGI: Wanamuziki wakome kudhulumu wapamba ngoma za video

August 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA DAISY MWANGI

KATIKA maeneo ya miji mikuu nchini kama Nairobi, Mombasa na Nakuru kuna wasichana wengi sana ambao hawana ajira.

Baadhi yao wanasoma vyuo vikuu, ila wazazi wao hawana uwezo wa kifedha, na hivyo inawabidi wajaribu kujitafutia angaa pesa za matumizi ya kimsingi.

Kunao wengine waliomaliza masomo yao ya chuo kikuu lakini kwa ukosefu wa ajira hawana budi kutafuta njia mbadala za kujikimu kimaisha.

Njia mojawapo ambayo wasichana hujaribu kutafuta hela ni kuingilia upamba ngoma kwa kucheza densi za video za muziki.Kwa kawaida, kuwa mpamba ngoma huhitajika tu msichana awe mrembo na angalau awe na kipawa au uwezo wa kuigiza na kusakata densi.

Kazi hii ya ni kazi tu kama nyingine na ikifanywa kwa uadilifu na utaalamu ufaao itawafaa wasichana wenye vipawa hivi na wataweza kujikimu kimaisha.

Hata hivyo, ni dhahiri kuwa wanamuziki wengi huwa wanawatumia wasichana hawa vibaya kwa kukataa kuwalipa licha ya kuwaahdi malipo baada ya kuzifanya video.

Kuna wengine pia ambao wanawadhulumu kimapenzi.Pia inakera kuwa baadhi ya wasichana hawa hupitia magumu haya baada ya kusakata densi kwenye video wakiwa nusu uchi.

Wengi wa wanamuziki hukataa kuwalipa vidosho hawa kwa kudai kuwa wanawapa nafasi ya kujulikana kwa kuwa wataonekana kwenye mitandao na runinga, na kwa hivyo wana haki ya kutowalipa.

Wengine badala ya kuwalipa huwa wanawanunuliwa vileo. Aibu iliyoje?Ni vibaya tena sana kwa wanamuziki kuwatumia vibaya wanamitindo wapamba ngoma kwani kama wafanyikazi wengine wana haki ya kulipwa. Itakuwa ni vyema kwa wasichana hawa kukubaliana kiasi cha malipo yao mwanzo kwa kuandikiana mikataba ili wasije wakaibiwa baadaye.

Pia, wasichana hawa wanafaa kujiheshimu kwa kutokubali kutupilia mbali maadili wanapoigiza kwenye video kama vile kutokea kwenye video ya muziki ukiwa nusu uchi.

Majuto ni mjukuu, huja kinyume, na mtandao huwa hausahau hata baada ya miaka 50. Kabla ya kufanya video yoyote, ni vyema ujiulize kama miaka 20 ijayo utakuwa sawa video ile ikitazamwa na watoto wako.

Wapo wanamuziki wengine ambao wanawatumia wasichana walio chini ya miaka 18 kwenye video. Hawa wanafaa wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Sababu kuu ya wao kufanya hivi ni kuwa ni rahisi zaidi ni kukataa kuwalipa hata shilingi moja mbali na kuwadhulumu kimapenzi. Wanamuziki wanaowatumia wasichana vibaya kwa kukataa kuwapa haki yao ya malipo na kuwadhulumu wanafaa wachukuliwe.

Wazazi pia wana jukumu la kuwalea wasichana wao kwa njia ya kimaadili. Wasiwachie kazi hii viongozi wa dini na walimu pekee.

Ni sharti wazazi wawe na muda na watoto wao wa kike, waongee nao na wawasisitizie kuwa hawafai kumruhusu yeyote awatumie vibaya.