Makala

NAKURU: Walevi waungana kuwakomboa wenzao

January 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

NA RICHARD MAOSI

WARAIBU wa pombe na mihadarati hatimaye wameanza kupata faraja baada ya kundi la kibinafsi lililobuniwa na walevi wenzao kuanzishwa mjini Nakuru.

Mkutano huo uliopatiwa jina  Anonymous Alcoholic (AA) huwaleta pamoja wanawake na wanaume waliogura ulevi kutoka mitaa ya Kaptembwa, Rhonda, Freearea, Kampi ya Moto na Lanet katika jukwaa la kubadilishana mawazo.

Makao yao rasmi yakiwa ni katika kanisa la Nakuru Cental, ambapo wametengewa sehemu maalum kuendesha shughuli zao.

Catherine Boyani, mwanzilishi na mwenyekiti wa kituo cha Nakuru Drop In katika kaunti ya Nakuru. Picha/Richard Maosi

Kituo cha nasaha na ushauri wa bure kilibatizwa jina Nakuru Drop In Centre.

Walevi kadhaa kutoka ngazi tofauti walioitikia wito hukita ndani ya kituo hicho kuelezea masaibu waliyopitia kabla ya kubadilika.

Nakuru Drop In imefungua milango kwa walevi na walanguzi wa mihadarati wenye azma ya kubadilisha mienendo yao.

Wakitumia sanaa ya mabango wamenakili maandishi kama vile ‘NEVER GIVE UP’ ili kutoa ujumbe wa kutia moyo na kuwafariji waliolemewa na jinamizi la mihadarati.

Monica Wanjiru 32, mama ya watoto sita anayepokea mafunzo kabla ya shughuli za kila siku. Picha/Richard Maosi.

Catherine Boyani,almaarufu kama ‘mlevi smart’ ni mfano wa kuigwa,mbali na kuwa mwenyekiti wa kituo cha Nakuru Drop In, alikuwa mlevi chakari kwa miaka 28.

Alibuni kituo hiki 2018 ili kuwasaidia vijana wa mitaani waliopoteza mwelekeo maishani.

Hili lilitokea miezi kadhaa baada ya naibu kamishna wa kaunti ya Nakuru Herman Shambi kutangaza ongezeko la idadi ya vijana waliozama katika janga la madawa ya kulevya mtaani Kivumbini.

Boyani anasema binafsi alianza kulewa akiwa katika shule ya upili kama mzaha kutokana na ushawishi wa marafiki.

Catherine Boyani na mamake katika eneo la Nakuru Central. Picha/ Richard Maosi

Alipojiunga na chuo kikuu alisomea uhasibu na kuhitimu lakini hakudumu katika taaluma yake kwenye kampuni ya Kenya Pipeline pombe ilipochochea afutwe kazi.

Familia yake hatimaye iliamua kumnusuru asije akataabika kwa kumfungulia duka wakidhani alikuwa amefundishika wasijue ndio mwanzo wa matatizo.

Baada ya miezi sita alirudia pombe kiu ilipoanza kumtatiza na akauza kila kitu kutoka kwenye duka lake kisha akatoweka na mtaji wa biashara kajivinjari Salgaa.

“Majirani walianza kujiuliza maswali mengi endapo nilikuwa nimerogwa ama nilikuwa mzima,” anasema.

Waraibu wa pombe wakipokea ushauri katika ukumbi wa Nakuru Central Jumatano katika kwenye kituo cha Nakuru Drop In. Picha/Richard Maosi

Mamake Bi Margret Mogaka anasema alimtafuta mwanawe kila mahali hadi alipompata kwenye mapango ya walevi akiwa hajitambui.

“Nilimrejesha nyumbani tukaanza kuishi pamoja isipokuwa Boyani alikuwa na mkono mrefu kwani alihitaji kunywa pombe kila siku,”alisema.

Aliacha kutumia makali akaingilia changaa hadi 2014 alipokubali kujiunga na kituo cha kurekebisha tabia na kuhitimu baada ya miezi mitatu.

Kwa ushirikiano na AA (Anonymous Alcoholic) kitabu kilichoandikwa na walevi kwa walevi alisoma na kupitia kila hatua za matibabu ua siku 90 hadi alipotibika.

Kuanzia hapo alitumia hela zake kufungua kituo cha Nakuru Drop In na kuwaalika waathiriwa kupata nasaha ya bure .

Mmoja wao ni Judy Nyawera, akizungumza na Taifa Leo dijitali alisimulia namna aliachana na taaluma yake ya uhandisi 2013.

Judy Nyawera anayeendelea kupokea nasaha katika kituo cha Nakuru Drop In. Picha/Richard Maosi

Tangu wazazi wake waage dunia miaka mitano iliyopita aligeukia pombe ili kujiliwaza.

Kulingana na Nyawera ulevi hupokezwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

“Baba yangu aliaga dunia kutokana na maradhi ya ini kupooza aliposhindwa kuzuia uraibu wake. Licha ya juhudi za daktari kumkomesha hakufuata maagizo hadi alipoaga,”alisema.

Aidha anasema dini haina nafasi kubwa katika juhudi za kumtibu mtu dhidi ya athari ya pombe.

Cha msingi ni mtu ajikubali na dini inaweza kuchukua nafasi yake kuanzia hapo.

“Niliwatimua wahubiri wengi walioalikwa nyumbani kuniombea,kwa sababu niliamini ndani kwa ndani walikuwa wakinikashifu kwa kujiletea msiba,”alisema.

Mwingine aliyefunguka ni Michael Ng’ang’a mraibu aliyebadili mienendo na kufungua kituo cha kurekebisha tabia kinachofahamika kama TARAJI.

Anasema kwa mfano jamii ya Agikuyu huwa wanawapatia watoto majina kama vile Kinywa na Munywa bila kujua ni kuchochea ulevi.

Zaidi ya mara moja amewashauri wazazi kuwabadilishia wanao majina akiamini jina lina nguvu ya kujenga au kuharibu tabia.

Michael Ng’ang’a mmiliki wa kituo cha kurekebisha tabia akiwa amejumuika na wengine kutoa ushauri katika kituo cha Nakuru Drop In. Picha/Richard Maosi.

“Licha ya kutoa ushauri ninawapatia waathiriwa ratiba na hatua za matibabu na wanapotibika wawasaidie wenzao kukabiliana na hali zao ,”alisema.

Michael amesaidia kubadilisha walevi wengi waliokuja kuwa watu wa maana kwa mfano Monica Wanjiru 32 kutoka eneo la Kiti mama wa watoto sita aliyeacha kubugia changaa 2016.

Alijifungua mtoto wa kwanza akiwa na miaka 14 na aliyeahidi kumuoa akatoroka.

Japo hutegemea vibarua kujikimu kimaisha anasema hali yake ya kawaida imerejea.

Anasema anajitegemea kuendesha maisha ya kila siku,akifarijika na ushauri anaopata kutoka kwenye kituo cha Nakuru Drop In.

Hata hivyo tulipotaka kujua mchango wa serikali ya kaunti, ilijitenga na madai kuwa haishirikiani na makundi yanayojaribu kuwasaidia walevi.

Francis Mutonya mwanachama kwenye kamati ya kushughulikia vileo na madawa ya kulevya alisema serikali iliyotangulia haikuwa na mfumo wa kabambe wa kufikia jamii.

“Hivi sasa tumeanzisha juhudi za kutenga kiasi fulani cha fedha kwa ushirikiano na NACADA ili kuwafikia vijana zaidi walioshindwa kujinasua kutokana na jinamizi la ulevi,”alisema.