Makala

'Ndoto yangu ni kutwaa tuzo za kimataifa katika uigizaji'

September 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

ANASEMA ametunukiwa kipaji tosha kufanya vizuri katika tasnia ya uigizaji na kutwaa tuzo za kimataifa kama Oscars, Emmys na Grammys kati ya zingine.

Anadai kuwa amepania kujituma mithili ya mchwa ili kutimiza ndoto yake kunasa tuzo chini ya chini ya mwavuli wa Kalasha Awards ndani ya miaka mitatu ijayo. Kadhalika analenga kutinga upeo wa kimataifa na kumpiku mwigizaji mahiri Viola Davis mzawa wa Marekani.

Pia anatamani kuibuka maarufu katika uigizaji angalau kutinga kiwango cha mwigizaji wa Hollywood mzawa wa hapa Kenya, Lupita Nyong’o.

Mwajuma ‘Belle’ Bahati ameorodheshwa kati ya msanii wa kike wanaozidi kuvumisha ulingo wa burudani ya maigizo nchini.

”Mwaka jana nilishinda tuzo kitengo cha Best Actress ‘Mwigizaji bora’ katika hafla ya Machawood kupitia filamu iitwayo ‘Whats on your mind’ hali iliyoashiria kwamba ninaweza kufanya vizuri katika uigizaji,” anasema na kuongeza kuwa

hatua hiyo ilimsaidia kupata dili nyingi za uigizaji kinyume na ilivyokuwa miaka iliyopita,” akasema.

Binti huyu amehitimu kwa cheti cha teknolojia kuhusu masuala ya uigizaji kutoka Chuo Kikuu cha Kenya College of Accountancy (KCA).

Mwigizaji ‘Belle’ Mwajuma anayelenga kutinga upeo wa kimataifa. Picha/ John Kimwere

Kando na maigizo dada huyu amekuwa mwimbaji wa nyimbo za kumtukuza Mungu kwa mtindo wa Reggae akiwa mwanachama katika kundi la Tuneden Band jijini Nairobi kabla ya kujiondoa binafsi kushughulikia uigizaji. Kadhalika anasema ingawa alianza kushiriki michezo ya kuigiza akiwa mtoto pia alitamani kuhitimu kuwa rubani.

Uigizaji umechangia kisura huyu kupata nafasi kuzuru mataifa tofauti duniani kama: Rwanda na Berlin mapema mwaka huu alikokuwa mwafrika wa pekee aliyehudhuria hafla ya maigizo.

Pia amezuru: Nigeria, Ujerumani, Australia, Ufaransa na Tanzania bila kusahau India. ”Nilikuwa nchini Nigeria mwaka 2014 nilipoalikwa kama mgeni wa heshima katika hafla ya kutuza waigizaji waliofana kwa jina ‘Africa Movies Academy Awards (AMAA),” anasema. Katika ziara hiyo alikutana na waigizaji mahiri kama: Rita Dominique, Mama G, Patience Ozokwo, Pastor Ken na Danny Glover kati ya wengine.

Msanii huyu ameshiriki filamu nyingi tu na kupeperushwa kupitia Maisha Magic East na M-Net zikiwamo: ‘Wife no2,’ ‘Siri’ ‘Tumbo Fortune’ ‘Afya Centre,’ kati ya zinginezo. Vilevile ameshiriki filamu kama:’Nairobi half life’ na ‘Nisisi.’

Anajivunia kufanya kazi na makundi ya kuzalisha filamu kama:Friends Ansemble, Festival of Creative Arts (FCA), Phoenix players kati ya mengine.

Anasema alipitia kipindi kigumu ndani ya miaka minne maana wazazi wake walikuwa wakimpiga kujihusisha na maigizo. Katika mpango mzima amepania kumiliki brandi ya kuzalisha filamu miaka ijayo ili kukuza waigizaji wanaokuja bila ubaguzi.

Kadhalika siyo mchoyo wa mawaidha anawahimiza wenzie wawe wakijifunza na kazi za wenzao pia wafanye utafiti kwa bidii ili kufahamu masuala tofauti kuhusu jinsi ya kuibuka mwigizaji bora.